Mayanga rasmi Mtibwa Sugar, kutangazwa muda wowote

Muktasari:

  • Mayanga alikuwa akiinoa Tanzania Prisons kabla ya kuikacha Desemba mwaka jana na leo huenda akatamburishwa rasmi Mtibwa Sugar.

Baada ya tetesi nyingi hatimaye Mtibwa Sugar wamethibitisha kukamilisha mazungumzo na Kocha wake wa zamani, Salum Mayanga na leo Alhamisi huenda akatangazwa rasmi na kuanza kibarua chake.

Mayanga kabla ya kutua kwa Wakata miwa hao, alikuwa akiinoa Tanzania Prisons yenye maskani yake mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Hata hivyo kama ambavyo Mwanaspoti iliwahi kuripoti Kocha huyo kujiunga na matajiri hao wa mkoani Morogoro, habari ilizopata leo zimethibitishwa rasmi kuwa mazungumzo yamekamilika.

Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Swabri Aboubakari amesema tayari wamemalizana na nyota huyo wa zamani wa timu hiyo na Taifa Stars na huenda akatangazwa rasmi leo.

Amesema wanaamini kurejea kwa Kocha huyo inaweza kusaidia timu kupata matokeo mazuri na kwamba mbali na Kocha huyo mazungumzo yanaendelea kwa baadhi ya wachezaji waliopendekezwa ili kuongeza nguvu.

"Kwa upande wa Kocha tumemalizana naye kila kitu Mayanga na leo jioni tunaweza kumtangaza rasmi, lakini wakati huohuo tunaendelea na kukamilisha utaratibu wa wachezaji wengine kama wanne ili kuungana na wenzao kikosini" amesema Aboubakari.

Hata hivyo habari kutoka ndani ya klabuni hiyo ni kuwa baada ya kumalizana na nyota wa kigeni raia wa DR Congo, Deo Kanda tayari wamemalizana pia na Kipa, Jeremia Kisubi aliyeomba kuondoka Simba iliyomsajili msimu huu kutoka Tanzania Prisons ambaye inadaiwa amesaini kandarasi ya mwaka mmoja na nusu.