Maximo: Tatizo ni uteuzi wa Scolari

Kocha Mkuu wa Yanga, Marcio Maximo ‘The Chosen One’ .PHOTO|FILE
Muktasari:
“Sasa ameona ubishi wake ndiyo umelitia taifa letu aibu ambayo hatukuwahi kuota kuipata, sawa tumefungwa lakini si kama vile, huo ni mzigo wake hatakiwi kujitetea.”
KOCHA Mkuu wa Yanga, Marcio Maximo ‘The Chosen One’ na msaidizi wake, Leonardo Neiva, juzi Jumanne hawakupata usingizi kisa kikiwa ni Brazil kupokea kipigo cha aibu cha mabao 7-1 mbele ya Ujerumani, lakini wamembebesha lawama Mbrazili mwenzao, Felipe Scolari.
Wakizungumza na Mwanaspoti jana Jumatano asubuhi, walisema ni makosa kuwaacha viungo Kaka na Robinho kutokana na uzoefu wao.
“Unajua nilikuwa mchambuzi katika michuano hii kwenye televisheni ya Mexico, lakini pia niliwahi kumpatia maoni yangu Scolari kuwa bado hao wachezaji walikuwa wanahitajika,” alisema Maximo.
“Sasa ameona ubishi wake ndiyo umelitia taifa letu aibu ambayo hatukuwahi kuota kuipata, sawa tumefungwa lakini si kama vile, huo ni mzigo wake hatakiwi kujitetea.”
Neiva alisema: “Hili alilolifanya Scolari ni janga kubwa kwetu hasa kwa taifa, ni wazi atasababisha matatizo makubwa Brazil.
“Hata kikosi alichokianzisha alikikosea, ni wazi kwa kupambana na timu kama Ujerumani unawezaje kumuanzisha Bernard? Nadhani alitakiwa kuwatanguliza Poulinho, Gustavo na Oscar. Ametuaibisha.”