MAVUGO? THUBUTUU!

Muktasari:
Lakini kwa hapa Bongo presha iko juu kwa timu 14 ambazo leo Jumamosi na kesho Jumapili zitaingia uwanjani katika mechi saba tofauti za ufunguzi wa msimu mpya baada ya miezi mitatu ya mapumziko, usajili na maandalizi ya jumla.
MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) Bara unaanza wikiendi hii wakati Yanga akili zao zikiwa bado kwenye michuano ya kimataifa. Jumanne ijayo watakamilisha ratiba ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kucheza ugenini na TP Mazembe ya DR Congo.
Lakini kwa hapa Bongo presha iko juu kwa timu 14 ambazo leo Jumamosi na kesho Jumapili zitaingia uwanjani katika mechi saba tofauti za ufunguzi wa msimu mpya baada ya miezi mitatu ya mapumziko, usajili na maandalizi ya jumla.
Gumzo kubwa leo ni mechi ya mabingwa wa zamani wa ligi, Simba ambayo ikiwa na wachezaji 12 wapya, kocha mpya na meneja mpya itakuwa nyumbani Uwanja wa Taifa, kucheza na Ndanda FC ya Mtwara.
Ni mtihani wa kwanza kwa kocha Mcameroon Joseph Omog ambaye anaamini kikosi chake kipo tayari kwa mapambano baada ya kufanya maandalizi ya kutosha ikiwemo kucheza mechi mbili za kimataifa za kirafiki dhidi ya AFC Leopards ya Kenya na URA ya Uganda tena bila kupoteza.
MAVUGO? ANACHEZA
Hadi jana Ijumaa jioni Simba ilikuwa ikipambana kukamilisha uhamisho wa straika wao tegemeo, Laudit Mavugo ili aweze kucheza leo Jumamosi watakapoikabili Ndanda. Viongozi wamesisitiza kwamba, lazima mchezaji huyo acheze na mambo yote wataweka freshi.
Mmoja wa viongozi Simba jana Ijumaa alisema: “Mavugo hachezi?thubutuu..anacheza.”
Licha ya kusajili wachezaji wengi, Mavugo ameonekana kukamata hisia za wengi.
Nyota wapya wa Simba wanaosubiriwa kulianzisha leo ni Shiza Kichuya na Blagnon Frederick ambao wataongoza mashambulizi huku katika safu ya kiungo Mdhamir Yasin, Mohammed Ibrahim na Jamal Mnyate wakitarajiwa kufanya yao. Wachezaji wengine wapya wa Simba ambao pengine wanaweza kucheza ni Ame Ali ‘Zungu’ na mabeki Method Mwanjali raia wa Zimbabwe, Emmanuel Semwanza na Hamad Juma.
Nguvu kubwa ya Simba ipo katika soka lao la kasi na pasi nyingi ambalo mara nyingi limekuwa likiwapa shida wapinzani wao, huku ikitumia mashambulizi ya pembeni hasa upande wa kushoto ulioshikwa na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Matarajio makubwa ya Simba ambayo iliweka kambi Morogoro mwezi mzima ni kwamba watarejea katika makali yao na kuwinda taji lao la 19 la ligi kuu baada ya kulikosa kwa miaka minne mfululizo.
Kikosi cha Simba kinachotarajiwa kuanza leo ni kipa Vincent Angban, mabeki, Hamad Juma, Tshabalala, Novatus Lufunga, Method Mwanjali, viungo Jonas Mkude, Mdhamir Yasin na Mussa Ndusha na washambuliaji ni Shiza Kichuya, Blagnon Frederic na Ibrahim Ajib. Endapo usajili wa Mavugo utakamilika kwa wakati ataweza kuanza badala ya Blagnon.
NDANDA NAO VIPI?
Wakali wa Mtwara, Ndanda Kuchele, wanatua Uwanja wa Taifa kusaka ushindi wao wa kwanza tangu wapande ligi kuu miaka miwili iliyopita. Ndanda imewahi kucheza mechi nne kwenye uwanja huo na kupata sare moja na vipigo vitatu.
Timu hiyo ya Mtwara inanolewa na Kocha Joseph Lazaro ambaye alitumia muda mwingi Dar es Salaam kufanya maandalizi, haijafanya usajili wa kutisha msimu huu, mchezaji wao nyota ni Salum Telela tu aliyetokea Yanga.
CHAMAZI KUNANI?
Punde baada ya kutwaa taji la Ngao ya Hisani, Azam inarejea kwenye ngome yake ya Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam kucheza na African Lyon iliyopanda ligi kuu msimu huu.
Azam imekisuka upya kikosi chake; mabeki Ismail Gumbo na Bruce Kangwa tayari wameifumua safu ya ulinzi ya timu hiyo kufuatia wakongwe, Aggrey Morris, Erasto Nyoni na Sergie Wawa kuwa majeruhi. Shomari Kapombe tayari amejiunga pia na kikosi hicho baada ya kukosekana kwa zaidi ya miezi minne.
Matajiri hao wa Ligi Kuu Bara pia wameifumua pia safu yao ya ushambuliaji ambapo nyota watatu wapya, Fransisco Zekumbariwe aliyetokea City Boy ya Zimbabwe, Gonazo Bi YA Thomas aliyetokea Club African ya Ivory Coast na Shaaban Iddi aliyepandishwa kutoka timu yao ya vijana chini ya miaka 20 wameingia katika kikosi kusaidiana na mkongwe, John Bocco.
Nguvu kubwa ya Azam inaonekana kuwepo katika safu ya kiungo ambapo viungo wao sita Jean Mugiraneza ‘Migi’, Himid Mao, Kipre Bolou, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya na chipukizi Abdallah Masoud wanaonekana kuwa katika kiwango bora kabisa.
Kwa upande wa African Lyon haijaonekana kuwa na maandalizi makubwa kuelekea msimu mpya. Lyon haijafanya pia usajili wa majina makubwa kama zilivyofanya timu nyingine shiriki za ligi kuu.
MOROGORO, SONGEA
Umbali wa kilometa 189 kutoka jijini Dar es Salaam hadi Morogoro, halafu umbali tena wa kilomita 50 kutoka Morogoro mjini hadi Manungu, Turiani kutakuwa na mchezo mwingine wa kuvutia ambapo Mtibwa Sugar itakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting ya Pwani.
Mtibwa ambayo kikosi chake kimepata mapengo kadhaa baada ya kuondokewa na nyota wao kadhaa wakiwemo Andrew Vincent, Mdhamiru Yassin na Shiza Kichuya inatarajiwa kuanza maisha mapya chini ya kocha wao wa zamani, Salum Mayanga kwa kuijaribu Ruvu ambayo imefanya usajili wa nyota kadhaa wakiwemo Jabir Aziz ‘Stima’, Abdulrahman Mussa na Fully Maganga aliyetokea Mgambo JKT.
Mtibwa imewaongeza Haruna Chanongo, Cassian Ponera na Rashid Mandawa ambao wanaungana na wakongwe Shaaban Nditi, Henry Joseph na wengineo kuanza maisha mapya klabuni hapo.
Mechi nyingine leo Majimaji itakuwa wenyeji wa Prisons mjini Songea, Stand United itakuwa wenyeji wa Mbao FC mjini Shinyanga wakati kesho Jumapili Mbeya City itasafiri kwenda Shinyanga kucheza na Kagera Sugar.
REKODI KUWANIWA
Wakati pazia la ligi kuu likitarajia kufunguliwa leo, rekodi kadhaa zinatarajiwa kuwaniwa kuanzia kwenye upachikaji wa mabao hadi idadi ya mataji.
Rekodi ya kwanza kubwa ni ile ya mabao 26 kwa msimu mmoja ambayo inashikiliwa na nyota wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein maarufu Mmachinga.
Rekodi ya kufunga ‘hatrick’ mbili kwa msimu mmoja inayoshikiliwa na Amissi Tambwe inatarajiwa pia kuvunjwa huku Tambwe akiendelea kukimbiza na ‘hatrick’ zake sita alizofunga katika misimu yake mitatu nchini.
NANI KUUNGANA
NA WATEULE?
Tangu kuanzishwa kwa Ligi Kuu Bara mwaka 1965 9 (ingawa wakati huo haikuwa ligi kuu) timu za Simba, Yanga, Cosmopolitian, Mseto, Pan African, Tukuyu Stars, Coastal Union, Mtibwa Sugar na Azam ndizo zilizowahi kutwaa taji.
Yanga ndiyo inayoongoza kwa kutwaa taji hilo mara 26 ikifuatiwa na Simba yenye mataji 18 kisha Mtibwa yenye mataji mawili na zilizosalia zimeambulia kutwaa taji hilo mara moja moja tu.
MAKOCHA WANENA
Makocha wa timu shiriki wametoa kauli kuashiria kwamba msimu huu hawana utani zaidi ya kulitaka taji, ingawa ukweli wa kauli zao utathibitishwa mwishoni mwa msimu wakati klabu moja itakaponyanyua juu kombe na kusherehekea ubingwa wao.
Asilimia kubwa wa makocha hao wakiwamo waliokuwapo msimu uliopita katika timu zao mpaka wale wageni na waliowapokea wenzao wamejitapata kuwa watapata ushindi katika mechi zao za ufunguzi kwa vile wanaamini wamefanya usajili nzuri.
Hata hivyo kwa kuwa soka ni mchezo unaochezwa hadharani na matokeo yake huwa hayajifichi, tusubiri kuona baada ya kipyenga cha mwisho cha mechi zao za ufunguzi kuanzia leo Jumamosi na zile za kesho Jumapili kujua ukweli ulivyo kama kweli wataanza vizuri au yatashuhudiwa maumivu.