Maua Sama ataja sifa ya mwanaume wa kumuoa

MWANADADA anayeendelea kushika rekodi ya video ya wimbo wake wa Iokote kutazamwa sana na kuwa na watazamaji wengi zaidi kuwahi kutokea kwa wasanii wa kike, Maua Sama ametaja sifa za mwanaume anayeweza kumuoa.
Tangu ameachia video hiyo ina mwaka mmoja sasa imetazamwa na watu million 17, mwanadada huyo ameweka wazi kuwa sifa za mwanaume ambaye anaweza kumuoa ni yule ambaye ana imani ya dini 'mcha Mungu'.
Amesema hayo alipokuwa anazungumzia wimbo wake mpya wa Nionyeshe na kutolea ufafanuzi jina la wimbo huo kuwa ni namna anavyotakiwa kuonyeshwa mapenzi ya kweli na mpenzi wake.
"Sijaolewa ila sifa za mwanaume ninayetamani anioe ni lazima awe mcha Mungu sichagui rangi akiwa mzungu au Mwafrika kama mimi hakuna tatizo kikubwa anatakiwa kuwa mcha Mungu hiyo ndio sifa pekee ambayo itampa nafasi kuhusiana na mambo mengine namuachia Mungu kwani hakuna mkamilifu," amesema.
Akizungumzia changamoto ya kazi zao hasa kipindi hiki cha janga la Dunia la ugonjwa wa virusi vya corona, Maua amesema kama wasanii wanapitia wakati mgumu kutokana na majukumu yao kusimama na kukosa matamasha ambayo ndio yanawaingizia fedha.
"Michongo mingi imesimama tunapitia hali ngumu sana tunamuomba Mungu atuepushie janga hili ambalo linaweza kuondoka kwa sisi wenyewe pia kufuata masharti kwa kunawa mikono," amesema.
Amesema ni janga la kidunia halijawakumba wao tu hivyo ni vyema kila mmoja akafuata taratibu zinazotolewa na Serikali ili kuepukana na ugonjwa huo ambao umekuwa kikwazo katika majukumu yote.