Matteo, Adam wakiri mambo magumu

Muktasari:
- Adam ambaye msimu uliyopita akiwa na Mashujaa alimaliza na mabao saba, jambo lililoishawishi Azam kumrejesha kikosini kabla ya kumtoa kwa mkopo Prisons ambako kabla ya mechi ya mwisho ya jana dhidi ya Singida Black Stars alikuwa akimiliki bao moja tu.
BAADHI ya washambuliaji wa Ligi Kuu Bara, Adam Adam wa Tanzania Prisons, Matteo Antony wa JKT Tanzania na Tariq Seif wa Kagera Sugar, wamekiri msimu huu haukuwa mzuri kwa upande wao.
Adam ambaye msimu uliyopita akiwa na Mashujaa alimaliza na mabao saba, jambo lililoishawishi Azam kumrejesha kikosini kabla ya kumtoa kwa mkopo Prisons ambako kabla ya mechi ya mwisho ya jana dhidi ya Singida Black Stars alikuwa akimiliki bao moja tu.
"Baada ya kusajiliwa na Azam sikuwa na nafasi ya kucheza, ambapo nikajiunga kwa mkopo wa miezi sita na Prisons na nimeshindwa kutupia za kutosha, kitu ambacho hakina afya kwa upande wangu," alisema Adam na kuongeza;
"Mpira wa miguu ni kazi yangu, najipanga msimu ujao kwa mapambano zaidi, siwezi kukata tamaa kwani kwa mchezaji kuna kipindi kiwango chake kinakuwa juu na wakati mwingine kinashuka."
Kwa upande wa Matteo anayehusishwa kutakiwa na timu za Mtibwa Sugar na Mbeya City kwa msimu ujao, msimu uliyopita alimaliza na mabao manne kabla ya mechi ya jana JKT Tanzania kucheza dhidi ya Mashujaa, mshambuliaji huyo hakuwa na bao.
"Kwanza sikuwa na nafasi ya kucheza mara kwa mara,hata hivyo mechi ambazo nilipata nafasi sikufunga, hivyo nakiri wazi haukuwa msimu mzuri kwangu," alisema Matteo aliyewah kuichezea KMC, Mtibwa Sugar na Yanga, huku Tariq alisema: "Acha msimu huu upite najipanga upya, soka halihitaji kukata tamaa badala yake linahitaji kujituma bila kukubali changamoto zikutoe mchezoni."