Matola: Tutawakimbiza Al Ahly kwa dakika 90

SIMBA imerejea Dar es Salaam leo ikitokea Zanzibar kwa ajili ya mechi ya kwanza ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri itakayopigwa Ijumaa wiki hii.

Mechi hiyo itaanza saa 3:00 usiku katika uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo benchi la ufundi la timu hiyo kupitia kwa kocha Msaidizi Seleman Matola limeweka wazi mipango kuwa ni pamoja na kuwakimbiza Waarabu hao kwa dakika zote 90 za mchezo.

Matola aliyewahi kuwa nahodha wa Simba, amesema chama lake linatambua vyema umuhimu wa kuanzia nyumbani kwenye michuano hiyo na wanaendelea kuandaa timu ambayo itakuwa fiti kwa dakika 90 za mchezo huo ambao wamepanga kushinda kuanzia mabao mawili na kuendelea.

"Faida ya kuanzia nyumbani ni ukishinda mabao mengi utampa presha zaidi mpinzani kwenye mechi inayofuata kwani anakuwa anawaza kurudisha mabao na kushinda," amesema Matola.

"Lengo letu ni kupata mabao zaidi ya mawili, tumedhamiria kutowapa Ahly nafasi ya kuwa na mpira hata kidogo. Tunafanya mazoezi hilo ambapo wakiwa hawana mpira hatutaki waupate na wakiupata basi tuwapokonye na kuwashambulia kwa kasi na umakini wa hali ya juu katika dakika zote 90."

Kocha huyo anayeungana na kocha mkuu Mualgeria Abdelhak Benchikha na msaidizi wake mwingine Farid Zemiti, amesema wanaijua vyema Al Ahly kwani wamecheza nayo zaidi ya mara tatu, hivyo itakuwa njia bora ya kuwakabili huku wakisisitiza kutaka kombe hilo msimu huu.

"Tunaijua vyema Al Ahly na tumecheza nayo mara nyingi. Nao pia wanatujua hivyo wanakuja kwetu wakituheshimu jambo litakalotupa faida ya kufanya vizuri zaidi," amesema.

"Wachezaji wote wana hamu na mechi hizi wakitaka kuweka historia pia tumekuwa tukifanya nao vikao kwa lengo la kuvuka hapa kwani ni eneo ambalo tumelizoea tayari."

"Hata kocha mkuu (Benchikha) amekuwa akiwaambia wachezaji kuwa ameshinda makombe makubwa hivyo analitaka na hili," amesema Matola aliyeeleza anatamani Simba imuondoshe bingwa mtetezi Al Ahly kwenye michuano hii kwani itakuwa rekodi kweke baada ya kuwaondosha Zamalek 2003 wakati akiwa nahodha wa timu hiyo.

Hii itakuwa mara ya nne kwa miaka ya hivi karibuni timu hizo mbili kukutana kwenye michuano ya CAF, kwani zilishapangwa mara mbili katika makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kila moja kushinda mechi mbili za nyumbani kwake na kupoteza ugenini na mwaka jana zilikutana tena kwenye mechi mbili za mashindano mapya ya African Football League ambapo mechi zote mbili zilimalizika kwa sare ambapo Kwa Mkapa ngoma ililala 2-2 na Cairo mechi ikaisha 1-1.

Huu ni wakati wa Simba kuonyesha ubabe wake kwani katika misimu saba mfululizo tangu 2018/2019 hadi sasa 2023/2024, imeingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara nne, mwaka katika misimu ya 2018/2019, 2020/2021, 2022,2023 ambapo zote imeishia hapo hivyo msimu huu ni wa kujitutumua kuvuka.