Mastaa Yanga wataka Guede aombwe radhi

Muktasari:

  • Guede ambaye alisajiliwa katika dirisha dogo la usajili msimu huu, alionekana kuwa na mwanzo mgumu katika kikosi hicho kilichopo chini ya kocha Miguel Gamondi, huku wachezaji wenzake wakisema lilikuwa ni suala la muda hivyo mashabiki watulie.

NI kama gari limewaka kwa mshambuliaji wa Yanga, Joseph Guede ambaye hivi sasa namba zake zinambeba na kumfanya kuwa mchezaji hatari katika kikosi hicho, lakini huku nyuma mastaa wa kikosi hicho wamewageukia mashabiki wakitaka wamuombe radhi nyota huyo.

Guede ambaye alisajiliwa katika dirisha dogo la usajili msimu huu, alionekana kuwa na mwanzo mgumu katika kikosi hicho kilichopo chini ya kocha Miguel Gamondi, huku wachezaji wenzake wakisema lilikuwa ni suala la muda hivyo mashabiki watulie.

Lakini, kadri muda ulivyokuwa ukisonga ameonekana kubadili upepo wa mambo kiasi cha kuwazidi kete mastraika aliowakuta kikosini hapo, Clement Mzize na Kennedy Musonda na sasa amekuwa akigombania nao namba.

Mshambuliaji huyo aliyetua Yanga akiwa na rekodi ya kukaa nje ya uwanja kwa miezi mitatu tangu alipoachana na Tuzlaspor ya Uturuki, mpaka sasa ana mabao sita Jangwani na asisti moja katika michezo saba ya mashindano yote. 

WASIKIE MASTAA
Akizungumzia Guede, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz KI amesema kuwa hakuwa na shaka na Guede kuhusu makali ambayo anayaonyesha hivi sasa na kwamba lilikuwa ni suala la muda  kuanza kuonekana.

Aziz Ki ambaye ndie kinara wa mabao amesema anamfahamu Guede tangu yupo Ivory Coast, ndio maana hakupata mashaka nae wakati alipokuwa hafanyi vizuri kipidi cha mwanzo.

"Mashabiki wamuombe radhi Guede kwani ndio kwanza ameanza na ni mchezaji mwenye uwezo na uzoefu mkubwa, hivyo wasije wakadhani atarudi nyuma na balaa zaidi litakuja msimu ujao kwani atakuwa tayari ameshakaa kwenye fomu zaidi.

"Kama sasa ameshafunga mabao ya kusaidia timu na kushinda bao la pekee katika mechi dhidi ya Mashujaa, huyo ni mshambuliaji mwenye uwezo usio wa kawaida na watu wasimuone ni wa kawaida bali waheshimu sana uwezo wake," amesema Aziz.

Aziz KI amesema bado kuna mambo makubwa zaidi ambayo Guede ataendelea kuyaonyesha ndani ya timu yao.

"Huyu ni mtu sahihi kwa kujua kufunga wakati ule nasema yale sikuwa nasema kwa kuwa ni mchezaji mwenzangu hapa Yanga nilikuwa namzungumzia mchezaji ambaye namfahamu kabla ya kukutana naye hapa na anajua kweli kufunga," amesema Aziz KI ambaye ni kinara wa mabao ndani Yanga na Ligi Kuu msimu huu.

"Atafunga sana hapa Yanga ndio kwanza ameanza na ukitaka kujua ni suala la ubora wake mkubwa angalia namna ya utulivu alionao anapokuwa ndani ya eneo la hatari huyu ni mshambuliaji wa kuweka mpira wavuni alizaliwa kwa kazi hiyo."

Naye Dickson Job ameeleza kuwa, wakati Guede anasajiliwa mashabiki hawakumwelewa japokuwa aliwaambia kuhusu ubora aliokuwa akiuonyesha mazoezini tangu siku ya kwanza alipomuona.

"Guede ni miongoni mwa washambuliaji bora sana, na uwezo wake haujaanza hivi karibuni kwani tangu alipofika alikuwa akifanya vizuri mazoezi na ndio maana kocha alimpa nafasi kila mara," amesema Job.

"Ni mzuri wa kufunga mipira ya vichwa na hata ndani ndani ya boksi. Ana sifa zote za mshambuliaji na nachokiona sasa kwa Guede tayari ameshazoea mazingira na ushindani wa ligi, hivyo anacheza kwa utulivu ndio maana amekuwa akitumia nafasi na kupata matokeo."