Mastaa wapya Simba fiti kuwavaa Al Ahly

Monday February 22 2021
simba pic
By Ramadhan Elias

KUELEKEA kwenye mchezo wa kesho wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi kati ya Simba ya Tanzania na Al Ahly ya Misri nyota wapya wa Simba waliosajiliwa kwaajili ya michuano hiyo mikubwa wapo tayari kwa mchezo huo unaotarajiwa kupigwa kesho kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa.

Wachezaji waliosajiliwa na Simba kwenye dirisha dogo la usajili kwa ajili ya michuano ya kimataifa ni mshambuliaji, Junior Lokosa raia wa Nigeria na Peter Muduhwa raia wa Zimbambwe ambao kwenye mchezo wa kwanza wa Simba ilioshinda bao 1-0 dhidi ya AS Vita ugenini DR Congo hawakuweza kucheza kutokana na kutokuwa fiti.

Akizungumza kwenye mkutano na wandishi wa habari, kocha msaidizi wa Simba Seleman Matola amesema kuwa wachezaji wake wote wapo fiti kwa ajili ya mechi hiyo wakiwemo hao wawili na kazi imebaki kwa makocha kuamua wamuanzishe nani.

"Tumejiandaa vyema kwa mchezo huo, hatuna majeruhi yeyote na wachezaji wote waliosajiliwa kwaajili ya michuano hii wako fiti na wamefanya mazoezi salama tayari kuwakabili Ahly.

"Tunatambua ubora wa mpinzani wetu (Al Ahly) ni timu ambayo inaongoza kwa ubora Afrika pia ni mabingwa watetezi wa michuano hii, tunawaheshimu lakinin kutokana na mpira ni mchezo wa wazi tumejipanga kupambana nao ili tuweze kuibuka na ushidi muhimu kwenye uwanja wa nyumbani," amesema Matola.

Sambamba na Matola, pia nahodha wa timu hiyo John Bocco amezungumza kwa niaba ya wachezaji ambapo ameweka wazi kuwa wamejiandaa vyema kisaikolojia kuwakabili Ahly.

Advertisement

"Tunaheshimu ukubwa wa wapinzani wetu, tumejiandaa kisaikolojia kuwakabili pia tunaimani katika maandalizi tuliyofanya kuelekea mchezo huu, tunaenda kupambana nao huku tukimuomba mwenyezi Mungu atujalie tupate ushindi ambao ndio lengo letu sote kwenye mechi hii," amesema Bocco.

Kwa mara ya mwisho timu hizi mbili kukutana ilikua Februari 12, 2019 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa wakati huo ukiitwa Taifa na Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0, liliofungwa na mshambuliaji Meddie Kagere dakika ya 65.

Advertisement