Prime
Mastaa wanne wapishana Yanga

Muktasari:
- Hiyo imewapa kiburi cha kuanza harakati za kufumua kikosi na kupanga hesabu mpya tayari kwa michuano hiyo mikubwa inayotabiriwa kuwa na presha kubwa kwao msimu ujao.
KITAKWIMU ni rasmi kuwa, Yanga imeshafuzu Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ikiwa imesaliwa na mechi nne mkononi.
Hiyo imewapa kiburi cha kuanza harakati za kufumua kikosi na kupanga hesabu mpya tayari kwa michuano hiyo mikubwa inayotabiriwa kuwa na presha kubwa kwao msimu ujao.
Mwanaspoti linajua, mastaa wanne wakiwamo viungo wawili Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Farid Mussa watapisha mashine nyingine klabuni hapo. Sure Boy na Farid huenda wakapelekwa kwa mkopo Singida Black Stars kama mipango itabaki kama ilivyo sasa.
Kisha kiungo wa Singida BS, Josephat Arthur Bada huenda akapishana nao ikielezwa anatarajiwa kutua Yanga kwa msimu ujao kuongeza nguvu katika timu hiyo yenye nafasi kubwa ya kuleta kocha mpya mwisho wa msimu, pamoja na straika Jonathan Sowah pia anayekipiga katika timu hiyo ya Ligi Kuu.
Watetezi hao wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA), wamejihakikishia kucheza michuano hiyo ya CAF, baada ya kukusanya pointi 70 katika mechi 26 walizocheza hadi sasa ikiwa na uhakika wa kumaliza ndani ya nafasi mbili za juu za ligi hiyo.
Chanzo cha kuaminika kutoka Yanga kimeliambia Mwanaspoti kuwa, uongozi wa timu hiyo umeanza kusajili tayari kujiweka mguu sawa kwa msimu mpya huku kiungo wa Singida BS akiwa miongoni mwa nyota watakaocheza Yanga.
Staa huyo mwenye mabao matatu na asisti nane msimu huu ameanza mazungumzo na Yanga kwa ajili ya kujiunga nayo msimu ujao na ataungana na Sowah ambaye alikaririwa akisema: “Viongozi wa Singida waliponifuata, niliwaambia nyumbani kwangu ni Yanga. Rais wa Yanga (Injinia Hersi Said) ni kama malaika kwa aliyonifanyia katika maisha yangu. Ni suala la muda tu kabla sijajiunga nao (Yanga).”
Chanzo chetu kuhusu usajili wa nyota hao kilisema: “Ni kweli mazungumzo ya kunasa saini ya kiungo huyo yameanza na yapo katika hatua nzuri nafikiri kama mambo yataenda sawa atakuwa sehemu ya kikosi chetu msimu ujao kama mchezaji wa ndani baada ya kubadili uraia.
“Tumezingatia mambo mengi kutamani kuwa na mchezaji huyo ni moja ya wachezaji walioonyesha uwezo mkubwa kwenye ligi yetu lakini pia tunaamini anaweza kuongeza nguvu kwenye kikosi chetu kutokana na aina yake ya uchezaji.”
Bada anamudu kucheza eneo la kiungo mshambuliaji namba (10) na nane, kutua kwake ndani ya kikosi hicho itakuwa sehemu ya kuwa mbadala wa Stephane Aziz Ki ambaye anatajwa kuwa katika mipango ya kuondoka Jangwani.
Lakini ataongeza pia kasi ya kuwania namba kikosini kama timu hiyo itafanikiwa kumbakiza Pacome Zouzoua anayecheza eneo hilo akiwa amefunga mabao manane na asisti tisa akihusika katika mabao 17 kati ya 68 yaliyofungwa na timu hiyo.
Yanga inatajwa pia ipo mbioni kumrejesha aliyekuwa kiungo wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyepo Azam FC kwa sasa akiwa na rekodi nzuri tangu amejiunga na timu hiyo msimu uliopita.
Ukiondoa kiungo huyo sambamba na mshambuliaji waliotajwa kujiunga na Yanga timu hiyo pia ipo kwenye mazungumzo na beki wa zamani wa Simba ambaye sasa anakipiga AS FAR, Henock Inonga.
SURE BOY, FARID
Wakati Bada akitajwa kuwa mbioni kuibukia Yanga, nyota viungo wawili wa timu hiyo, Farid Mussa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ hawatakuwa sehemu ya kikosi hicho kwa msimu ujao kwa kilichoelezwa kuwa watatolewa kwa mkopo dirisha kubwa la usajili kwenda Singida Black Stars.
Wawili hao wote wamebakiza mkataba wa mwaka mmoja baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kila mmoja mwanzoni mwa msimu huu.
Chanzo cha kuaminika kutoka Yanga kimeliambia Mwanaspoti, nyota hao wa zamani wa Azam FC, licha ya kuwa na uwezo mkubwa wanakosa nafasi ya kucheza mara kwa mara hivyo ili kulinda vipaji vyao wameona ni bora wawatoe kwa mkopo ili kwenda kuongeza ubora.
“Hadi mwisho wa msimu kila kitu kitajulikana kwasababu timu sasa inapambana kuwa na wachezaji wachache ambao wote watapata nafasi ya kucheza kulingana na ubora,” alisema mtoa habari huyo na kuongeza;
“Nafasi moja inatakiwa kuwa na wachezaji wawili hadi watatu ambao wote watakuwa na ubora unaofanana ili kupishana kulingana na uhitaji wa mchezaji husika na mechi husika na sio kama ilivyo msimu mzima mechi 30 kati ya hizo mmoja anacheza 20 hadi 25 wengine wakitumika kwenye mechi tatu hadi tano.”
Ukiondoa wachezaji hao Yanga ina kibarua cha kubakiza baadhi ya mastaa muhimu wa kikosi cha kwanza ambao mikataba yao inaelekea ukingoni ikiwa ni pamoja na kiungo fundi wa boli Khalid Aucho, Duke Abuya, Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Yao Kouassi na wengine ni wale ambao hawana namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza kama fundi mwingine Clatous Chama, Jonas Mkude na kipa Abuutwalib Mshery.