Mastaa Simba na jicho la Gomes

UZOEFU wa mastaa wa Simba ndio uliowabeba dakika 45 za kipindi cha kwanza, kwani mbinu na akili ziliwafanya wafike mara kwa mara langoni kwa African Lyon.

Japokuwa African Lyon wachezaji wake walikuwa wanatumia nguvu na mbio lakini mipango ya kutengeneza nafasi za kufunga ilikuwa hafifu.

Mastaa wa Simba walionekana kujinafasi na mpira wao wa pasi, huku Lyon wakionekana muda mwingi kupambana kuwakaba.

Pamoja na Simba kumiliki mpira kwa kiasi kikubwa, udhaifu wao ulionekana kwenye umaliziaji kwani kuna nafasi za wazi walizikosa.

Kocha wa Simba, Didier Gomes alipanga kikosi mchanganyiko wachezaji wanaopata nafasi kikosi cha kwanza kama Aishi Manula, Larry Bwalya na Hassan Dilunga ambaye alianza dhidi ya Al Ahly mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, timu hiyo ikishinda bao 1-0.

Mwanaspoti linakuletea uchambuzi wa mastaa wa Simba ambao wanapaswa kumhakikishia kocha Gomes kuanza kuwaamini kuwapanga kikosi cha kwanza mechi za Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

IBRAHIM AJIBU

Ajibu hana nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Gomes,katika mechi ya leo Ijumaa ya Februari 26, 2021anacheza kwa kujituma ingawa hajafikia kile kiwango chake.

Ndiye aliyefunga bao dakika ya 10 baada ya kuunganisha kwa kichwa kona iliyochongwa na Bwalya.

Anapambana kupiga pasi tulivu na wakati mwingine anafika ndani ya 18 kutaka kufunga.

Dakika ya 44 Ajibu amefunga bao la pili baada ya Bwalya kupiga shuti kipa wa Lyon alipangua, Ajibu akaiunga hadi kwenye nyavu.


LARRY BWALYA

Bado anaendeleza kiwango chake kinachomfanya aminiwe na kocha kwenye mechi za Caf na ligi kuu.

MEDDIE KAGERE

Wimbi la kukosa penalti bado linaendelea kumtesa Meddie Kagere, raia wa Rwanda mwaka 2021, alianza katika mashinda ya Kombe la Mapinduzi, kipa Farouk Shikalo aliidaka, ilikuwa fainali yao na Yanga.

Katika mechi ya leo, Kagere amekosa penalti dakika ya 21 aliupiga mpira pembeni, ilitokana na Chikwenda kuchezewa rafu na mabeki wa Lyon.


GADIEL MICHEAL

Akipata mechi zaidi Gadiel anayekalishwa benchi na Mohamed Hussein 'Tshabalala' anaweza akarejea kwenye kiwango chake kama alivyokuwa Yanga misimu miwili iliyopiga.

Amefanikiwa kupeleka mashambulizi ya upande wake wa kushoto,pia anapanda na kushuka kukaba kwa wakati.

PARFECT CHIKWENDE

Bado hajawa kwenye kiwango kile kinachotarajiwa na wengi ingawa anapambana kuonyesha mchongo wake katika mechi hiyo.

JONAS MKUDE

Anaonekana kama hayupo mchezoni kutokana na eneo lake kutopata usumbufu kutoka kwa viungo wa Lyon.

IBRAHIM AME

Hajapata kashikashi za washambuliaji wa Lyon, japokuwa hata mashambulizi ya kushitukiza aliyaokoa kwawakati.