Mastaa Ihefu waiteka Kyela

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Kyela. Wakati michuano ya Samia pre season ikianza leo Alhamisi, nyota wa Ihefu leo wameonekana kuteka uwanja wa Kipija uliopo wilayani hapa mkoani Mbeya kutokana na kushangiliwa na wadau na mashabiki waliojitokeza kushuhudia mashindano hayo.

Michuano hiyo inashirikisha timu saba ikiwa ni Tanzania Prisons, Mbeya City, Ihefu, Ken Gold, Kyela DC, Mbeya DC na Rungwe DC ambazo zimegawanywa makundi mawili.

Lengo la mashindano hayo ambayo ni msimu wake wa pili, yanalenga kuzipa muda wa kujipima na kujiandaa timu zote na mashindano yake hususani zile za Ligi Kuu na Championship.

Tofauti na mapokezi ya timu zingine haswa Prisons na Ken Gold ambazo zilitangulia, lakini shangwe na hamaki vilitawala kwa wadau na mashabiki ilipoingia Ihefu.

Mzuka ulionekana kuwapanda mashabiki huku wakitaja baadhi ya nyota wake wakiwamo Papy Tshishimbi, Nicolas Wadad, Juma Nyoso na Obrey Chirwa.

Hata walipoingia uwanjani kupasha misuli, mashabiki hao walijikusanya kushuhudia matizi ya nyota hao wakiwa chini ya Kocha wao Mkuu, Zuberi Katwila.

Wachezaji hao walionekana kuwa na ari, morari lakini pia kuonesha sura za tabasamu muda wote hali iliyowavutia mashabiki ambao wamejazana uwanjani hapo.


Prisons, Ken Gold hakuna mbabe Samia Pre Season

Timu za Tanzania Prisons na Ken Gold zimeshindwa kutambiana baada ya kutoshana nguvu ya bila kufungana katika mashindano ya Samia Pre Season yaliyoanza leo Alhamisi katika uwanja wa Kipija.

Mchezo huo ulikuwa wa kwanza katika kundi B yenye timu hizo sambamba na Rungwe DC na Mbeya  DC ambazo zitachuana kusaka mbili pekee kuungana na za kundi A kutinga nusu fainali.

Katika mchezo huo makocha wa timu zote waliingiza vikosi vyao kuona uwezo, ubora na mapungufu na kufanya dakika 45 za kwanza kumalizika kwa nguvu sawa bila kufungana.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Kipindi cha pili pia licha ya Prisons kubadili kikosi chake kwa kuingiza sura mpya, hakuna kilichobadili matokeo na kufanya mechi kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana.

Katika mechi hiyo, Prisons ilishusha silaha zake mpya nane ikiwa ni Kipa Mussa Mbisa, Hamis Mcha, Michael Masinda, Yusuph Mlipili, Zabona Hamis, Ismail Mgunda, Edwin Charles na Ahmad Maulid.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Prisons, Patrick Odhiambo amesema hajaona mapungufu yoyote kwa nyota wake badala yake michuano hiyo itawaweka fiti na kwamba hadi Ligi kuanza watakuwa tayari kwa kazi.

"Usajili tayari tumemaliza, sijaona mapungufu japokuwa hii michuano itatusaidia kujiweka vizuri kabla ya Ligi na tuko tayari kwa msimu mpya, ratiba nimeiona" amesema Odhiambo.