Mastaa hawa watafunika Yanga

ACHANA na Simba Day na Azam Festival. Kesho Yanga wana jambo lao katika kilele cha Wiki ya Mwananchi kwenye Uwanja wa Mkapa.
Ndiyo gumzo kubwa miongoni mwa mashabiki wa soka sasa.
Katika kuhakikisha hilo wiki nzima mashabiki wa Yanga ambao ndio wananchi wenyewe wameamua kwenda kuwapokea wachezaji wao wa kigeni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuwaonyesha kabisa kwamba ni timu ya wananchi.
Kwa upepo ulivyo mitaani kesho kuna wachezaji ambao wanatarajiwa kufunika kutokana na aina ya uchezaji pamoja na namna ambavyo mapokezi yao yalivyokuwa. Watacheza mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Aigle Noir ya Burundi;
TUISILA KISINDA/ MUKOKO TONOMBE
Usajili wao ulishtua kwani sio jambo dogo kutoka As Vita na kutua Yanga huku wakiwa na mikataba, ni kitu kikubwa kwa Yanga kukifanya.
Mapokezi ya wachezaji hawa kutoka Uwanja wa Ndege, yalikuwa ni makubwa na kufikia hatua ya kufunga barabara kwa muda fulani kisa tu wachezaji hao.
Tonombe na Kisinda wana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha kwamba wanarejesha furaha kwa mashabiki wa Yanga.
BAKARI MWAMNYETO
Beki huyu alikuwa anahitajika na Simba hivyo kutua kwake katika kikosi cha Yanga ni jambo ambalo mashabiki wa wanajivunia na kupita kifua mbele.
Ni usajili mkubwa kwa Yanga na kishabiki ni pigo kwa Simba hali ambayo iliwafanya waende kumsajili Ibrahim Ame ambaye alikuwa pacha wa Mwamnyeto walipokuwa wakicheza Coastal Union.
Mwamnyeto ni mchezaji ambaye anatajwa kufanya makubwa kutokana na aina ya uchezaji wake, hivyo hata katika mchezo wa kilele cha Wiki ya Mwananchi anatarajiwa kufanya vizuri.
WAZIRI JUNIOR
Msha-mbuliaji huyu licha ya kwamba hazungumziwi sana lakini Yanga walihakikisha kwamba wanampata na sio kwenda Azam ambao walikuwa wameanza kumnyatia.
Junior ni mchezaji ambaye analijua goli na hilo lipo wazi baada ya kuifungia timu yake ya zamani Mbao FC mabao 13 msimu uliopita akiwa na wachezaji wa kawaida.
Ametua katika kikosi ambacho kina viungo wengi wenye ubora hivyo anaweza kuanza kuwashangaza wananchi kupitia kilele cha siku yao kwani sio mtu mwepesi kukosa mabao anapokuwa kwenye nafasi ya kufunga.
FARID MUSSA
Winga huyu alikuwa anacheza soka la kulipwa nchini Hispania katika klabu ya Tenerife, usajili wake nao ulitikisa kutokana na mabosi wake wa zamani Azam FC kutaka arejee lakini alifanya uamuzi ya kwenda zake Yanga.
Ni winga ambaye ana uwezo mkubwa wa kukaa na mpira pamoja na kukimbia kwa kasi kama ambavyo imezoeleka kwake katika kufanya hivyo kuanzia Azam mpaka Taifa Stars.
Farid anasubiriwa kuonyesha mbwembwe zake na kile alichojifunza Ulaya.
CARLOS FERNANDEZ ‘Carlinhos’
Wakongo walikuwa na nyomi lakini mapokezi ya Carlinhos yalifunika zaidi, hakuna mchezaji ambaye alipata mapokezi makubwa vile mpaka sasa.
Kiungo huyu kutoka Angola ni ishara kabisa kwamba mashabiki wa Yanga wana jambo lao kesho na watataka kwa vyovyote vile kujazana kwenda kuona miguu yake ina nini.
Carlinhos ni kiungo ambaye anasifika kwa kupiga pasi zenye macho na mshambuliaji anakuwa na kazi nyepesi tu katika ufungaji, hivyo washambuliaji wa Yanga wanakuwa na kazi moja tu ya kutupia wavuni.
YASSIN MUSTAPHA
Inawezekana sasa ndio safari ya beki huyu wa kushoto kwenda Taifa Stars. Yuko vizuri katika ulinzi, kumiliki na mpira na anatisha anapopanda mbele kusaidia mashambulizi.
Yassin kwa misimu miwili akiwa na Ndanda mpaka Polisi Tanzania, alikuwa akipata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza na kuonyesha uwezo mkubwa.
Beki huyu mwenye mapafu ya mbwa, anaweza kuwateka Yanga kwani walikosa mchezaji wa aina yake.