Mashujaa v Dodoma, wanaanzia walipoishia

Muktasari:
- Sasa basi baada ya kupita takribani miezi mitatu tangu tushuhudie mtanange huo, leo Jumamosi timu hizo zinaingia tena dimbani hapo kucheza mechi ya ligi lakini sasa ni msimu wa 2024-25. Unaweza kusema wawili hao wanaanzia walipoishia.
Si unakumbuka Mei 28, 2024 ndiyo msimu wa Ligi Kuu Bara 2023-2024 ulifikia tamati? Basi siku hiyo zilipigwa mechi nane zikihusisha timu 16 zilizoshiriki ligi msimu huo, na kati ya mechi hizo, Mashujaa iliichapa Namungo mabao 3-0 kwenye Dimba la Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Sasa basi baada ya kupita takribani miezi mitatu tangu tushuhudie mtanange huo, leo Jumamosi timu hizo zinaingia tena dimbani hapo kucheza mechi ya ligi lakini sasa ni msimu wa 2024-25. Unaweza kusema wawili hao wanaanzia walipoishia.
Katika mechi za leo, Relliants Lusajo ambaye ni mshambuliaji mpya ndani ya Dodoma Jiji, ana kazi ya kupambana na waajiri wake wa zamani Mashujaa mechi ikitarajiwa kuanza saa 10:00 jioni
Lusajo anarejea Dimba la Lake Tanganyika ambapo msimu uliopita alifanya vizuri akiwa na jezi ya Mashujaa akifunga mabao sita huku akimaliza ligi na mabao manane kutokana na mawili kuyafungia akiwa Namungo kabla ya dirisha dogo kuhama.
Ukiachana na ishu ya Lusajo kupambana na waajiri wake wa zamani, mchezo huo unatukumbusha kilichotokea Mei 28, 2024, siku ya kufunga pazia la Ligi Kuu Bara msimu uliopita 2023-24 ambapo timu hizo zilikutana uwanjani hapo na wenyeji kushinda mabao 3-0, wafungaji wakiwa ni David Ulomi na Reliants Lusajo aliyehamia Dodoma Jiji akifunga mawili.
Rekodi zinaonyesha kwamba, Mashujaa ambayo huu ni msimu wa pili kucheza Ligi Kuu Bara, imekutana mara mbili na Dodoma Jiji iliyopo katika Ligi Kuu tangu msimu wa 2020-21. Dodoma Jiji inakumbuka katika mara mbili ilizocheza dhidi ya Mashujaa haijaambulia ushindi zaidi ya kufungwa na sare.
Hata hivyo, katika mchezo wa leo tutashuhudia mabadiliko makubwa ya timu hizo mbili kuanzia wachezaji hadi benchi la ufundi kwani Dodoma Jiji imebadilisha kocha mkuu na wasaidizi wake jukumu akipewa Mecky Maxime akisaidiwa na Nizar Khalfan, lakini pia imewasajili wachezaji kama Ibrahim Ajibu, Wazir Junior na Lusajo.
Mashujaa ambao ni wenyeji wa mchezo wa leo, nao wamefanya mabadiliko ya kikosi chao kwa kusajili wachezaji kama Mohamed Mussa aliyetokea Simba na Crispin Ngushi aliyewahi kucheza Yanga na Coastal Union.
ILIVYOKUWA
Mashujaa 3-0 Dodoma Jiji
Dodoma Jiji 1-1 Mashujaa
NAMUNGO VS FOUNTAIN GATE
Timu hizi zimekutana kwa misimu miwili tangu Fountain Gate ikiitwa Singida Big Stars na kisha Singida Fountain Gate. Leo, saa 1:00 usiku Namungo itaikaribisha Fountain Gate kwenye Dimba la Majaliwa mkoani Lindi.
Kocha wa Namungo, Mwinyi Zahera ana kazi ya kufanya katika mchezo wa leo kuhakikisha Wana Ruangwa wanapata furaha baada ya msimu uliopita kuwa na huzuni katika mechi zote mbili walizocheza dhidi ya Fountain Gate kwenye Ligi Kuu.
Ukichana na msimu uliopita, rekodi za jumla zinaonyesha kwamba timu hizo zimekutana mara nne katika Ligi Kuu Bara kuanzia msimu wa 2022-23 ambapo Fountain Gate imeshinda mechi tatu na sare moja, hivyo leo kuna kazi kwenye Uwanja wa Majaliwa.
Mara ya mwisho katika ligi zilikutana Machi 16, 2024, bao la Nicholaus Gyan liliamua ushindi kwa wenyeji Fountain Gate wakishinda 1-0, lakini kwenye Dimba la Majaliwa, Namungo walikandwa 2-3, huku Marouf Tchakei akitupia kambani mara mbili na Habib Kyombo mara moja. Mabao ya Namungo yalifungwa na Derrick Mukombozi na Emmanuel Charles.
Katika maandalizi ya msimu huu, timu hizo zilicheza mechi ya kirafiki wakati Namungo akiwa imepiga kambi Karatu na kushinda bao 1-0.
WASIKIE MAKOCHA
Kocha wa Namungo, Mwinyi Zahera amesema kuelekea mchezo wa leo wanamshukuru Mungu kikosi chao kipo salama hakuna mchezaji mwenye tatizo lolote.
“Tulikuwa Karatu kwenye maandalizi ya msimu na tangu turudi Ruangwa tumeendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi dhidi ya Fountain Gate. Kila kitu kipo sawa, afya za wachezaji wote 28 zipo sawa.
“Fountain Gate tulicheza nao mechi ya kirafiki ambayo ilikuwa ya mwisho, nimeona wamesajili wachezaji wazuri na wazoefu, itakuwa mechi ngumu, tunajua malengo yetu na nini cha kufanya ili kupata ushindi mechi ya kwanza nyumbani.
“Morali ya wachezaji ni nzuri, nimeona hilo kupitia maandalizi tuliyofanya wakiwa na njaa ya kuona siku ya mechi inafika tucheze. Naomba mashabiki waje kwa wingi kesho (leo) kwani hakuna kiingilio, tunataka sapoti yao tufanikishe kutimiza malengo katika mchezo wa kwanza,” alisema Zahera.
Kocha wa Fountain Gate, Mohamed Muya, amesema maandalizi yamekamilika na kilichobaki ni kuingia uwanjani kusaka ushindi.
“Tunajua dhamana tuliyo nayo, vijana tumewaandaa vizuri wakiwa na afya njema, wanasubiri kesho ifike tufanikishe kilichotuleta.
“Malengo yetu msimu huu ni kumaliza nafasi kuanzia ya nne kwenda juu, tuna kikosi kizuri na tunaamini melengo yatakwenda kufikiwa.”
Kocha wa Mashujaa, Abdallah Baresi alisema: “Tumesajili vizuri kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye msimu mpya wa mashindano, tuna imani pale tulipomalizia ndipo tutakapoanzia kwenye mchezo wa kesho (leo).”