Prime
Kocha Simba afichua walivyofurahia Azizi Ki kutimka

Muktasari:
- Kingine ni kwamba mkataba wa Aziz KI na Wydad utakuwa wa miaka miwili akianza kucheza michuano ya Klabu Bingwa Dunia itakayofanyika Juni 15, 2025 hadi Julai 13, 2025, huko Marekani.
KITENDO cha Aziz KI kukubali dili la kutua Wydad, atakuwa anaweka kwenye waleti mshahara wa Sh72.3 milioni kwa mwezi. Ni mara mbili ya aliokuwa akilipwa Yanga.
Kingine ni kwamba mkataba wa Aziz KI na Wydad utakuwa wa miaka miwili akianza kucheza michuano ya Klabu Bingwa Dunia itakayofanyika Juni 15, 2025 hadi Julai 13, 2025, huko Marekani.
Sasa kuna habari mpya. Kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliviera 'Robertinho' amefichua kwamba klabu hiyo itakuwa imefurahia kwa kiasi kikubwa kuuzwa kwa staa huyo kwani enzi zake kulikuwa na jitihada za makusudi za kumsajili kwa namna yoyote ile ikashindikana.
Na ameweka wazi kwamba ni mchezaji aliyekuwa akiwanyima raha zaidi Simba na hata kwenye vikao vikubwa enzi zake alikuwa akijadiliwa sana kutokana na madhara yake uwanjani.
Robertinho aliyetimuliwa Simba baada ya kichapo cha mabao 5-1 cha mechi ya Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Novemba 5, 2023, alisema kama kuna timu itakayokuwa imefurahi kuondoka kwa Aziz Ki ni Simba,kwani enzi akiinoa ilikuwa ikimpigia hesabu kumng'oa Yanga ili wapate utulivu.
Robertinho ambaye ni raia wa Brazili, alisema; "Simba ilikuwa na mkakati mkubwa wa kumuondoa Aziz KI Yanga, kwa namna yoyote ile hata kumsajili, lakini ilikuwa inashindikana kutokana na msimamo na mkataba aliokuwa nao Yanga."
"Yanga imepoteza nguvu kubwa, lakini kwa kuwa wamefanya biashara hakuna shida na ninaamini mbadala wake utakuwa umepatikana ndio maana wamechukua maamuzi hayo,"aliongeza Kocha huyo aliyepigwa chini baada ya kipigo cha mabao 5-1 kwenye dabi.
"Kwa bidii na uwezo wa Aziz KI hakuna timu atakayokwenda asipate namba ya kucheza, kwani kocha wa klabu yake mpya atakuwa amemsoma vyema, Waarabu wanapenda sana mchezaji mwenye akili ya kufunga na kutengeneza nafasi,"aliongeza.
Robertinho ni mmoja ya makocha aliyelizwa na Aziz KI, kwani katika Dabi iliyomtibulia kibarua kiungo huyo alifunga mabao mawili na kuasisti bao moja, lakini alifunga pia katika ushindi wa 2-1 katika mechi ya marudiano ya msimu huo Simba ikiwa chini ya Abdelhak Benchikha na pia katika sare ya 1-1 kabla ya Robertinho kutoa Msimbazi akitokea Vipers ya Uganda.
Pia alifunga bao wakati Simba ikishinda 3-1 na ilipolazwa 3-0 na Asec Mimosas katika mechi za Shirikisho Afrika 2022.
Yanga imekubali kumuuza Aziz KI kwa kiasi cha Sh 2Bilioni, lakini mkataba ukiwa na kipengele cha kwamba kama atachemsha na kutaka kuondoka Wydad, basi Yanga itapewa kipaumbele.
MISIMU MITATU YA AZIZ
2022/23-Mabao 09
2023/24-Mabao 21
2024/25-Mabao 09
Katika misimu hii yote Aziz amefikisha jumla ya asisti 32.