Coastal Union yashtukia ishu ikijiandaa lala salama

Muktasari:
- Coastal inayoshika nafasi ya 10 kwa sasa ikiwa na pointi 31, imesaliwa na mechi dhidi ya Fountain Gate na Tabora United, iliwapa mapumziko wachezaji, lakini benchi limewaita haraka Jumatatu ili kuanza maandalizi ya mechi hizo za kuwaepusha kuangukia katika play-off.
BENCHI la ufundi la Coastal Union, limeshtukia jambo baada ya kuamua kuwaita wachezaji wote kambini Jumatatu, tayari kwa maandalizi ya mechi mbili zilizosalia za kufungia msimu zitakazopigwa Mkwakwani, jijini Tanga.
Coastal inayoshika nafasi ya 10 kwa sasa ikiwa na pointi 31, imesaliwa na mechi dhidi ya Fountain Gate na Tabora United, iliwapa mapumziko wachezaji, lakini benchi limewaita haraka Jumatatu ili kuanza maandalizi ya mechi hizo za kuwaepusha kuangukia katika play-off.
Kaimu Kocha Mkuu wa Coastal, Joseph Lazaro amesema ameamua kuwaita mapema kwa kugundua mechi zilizopo mbele yao ni ngumu, hususani ile dhidi ya Fountain Gate inayopambana kutoka katika janga ya kucheza playoff, kwani ipo nafasi ya 14 katika msimamo.
Coastal itakutana na Fountain Gate Juni 18 mara baada ya ligi kurejea tena kupigwa baada ya kusimama kwa wiki mbili kupisha mechi za Kombe la Shirikisho (FA) na ile ya kimataifa, kisha ndipo itamalizana na Tabora inayoshika nafasi ya tano siku ya Juni 22 ambayo ndio mwisho wa msimu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lazaro alisema likizo ya siku 16 aliyowapa wachezaji itaisha Jumapili na Mei 26 kila mchezaji atatakiwa kambini na kwamba wamepanga kucheza mechi nne za kirafiki za kujipima nguvu kabla ya kuanza vita ya kumalizia Ligi Kuu.
Lazaro alisema kumekuwa na ugumu wa kuzipata timu hizo nne jijini Tanga, hivyo wanaweka mipango sawa ikiwezekana kupata timu za jijini Dar es Salaam.
“Dar ni rahisi kwa sababu kuna timu nyingi zinacheza ligi zipo huko na hata zile za Maveterani inakuwa rahisi kupata mechi za kirafiki kujipima lakini Tanga ni ngumu sana ingawa tutapambana kupata hata kama na timu za vijana,” alisema na kuongeza:
“Hapa kuna African Sports pekee sasa ukihitaji kujipima unapaswa kucheza na timu tofauti ili kujua upungufu uko wapi urekebishe na ukiingia kwenye mechi unakuwa tayari ushajipanga ila huku huwezi kupata timu unayokusudia,” alisema Lazaro beki wa zamani wa kimataifa Coastal, Yanga na Taifa Stars.
Aliongeza mechi hizo mbili ni muhimu kwa Coastal ambao bado hawako kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.
“Tunajua ugumu wa mechi hizo lakini kama Coastal tunatamani kushinda zote ili kujiweka pazuri kwa sababu timu zimepishana pointi chache kwa hiyo mipango yetu ni pointi sita.”
Coastal iliyoiwakilisha nchi msimu huu katika Kombe la Shirikisho Afrika baada ya msimu uliopita kumaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu, inalingana pointi na Namungo zikiwa na 31 ila zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
Tayari timu za KenGold na Kagera Sugar zimeshashuka daraja, na timu zilizosalia kuanzia iliyopo nafasi ya saba hadi ya 14 zinapambana kuepuka kuangukia katika play-off ili kusaka timu ya tatu ya kuungana na timu hizo zilizoshuka mapema.