Mashabiki wampa mzuka Kimenya Lesotho

Muktasari:

  • Kimenya anayechezea Tanzania Prisons ni miongoni mwa nyota wachache wa Stars wenye uwezo wa kucheza zaidi ya nafasi moja uwanjani.

Kiraka wa timu ya taifa 'Taifa Stars', Salum Kimenya amekoshwa na hamasa kubwa ya mashabiki Watanzania kuelekea mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani dhidi ya Lesotho utakaochezwa Jumapili, Novemba 18 huko Maseru, Lesotho.

Zaidi ya mashabiki 50 wamesafiri kwa basi kutoka Tanzania kwenda Lesotho kuipa sapoti Stars ambao wataungana na wenzao watakaosafiri kwa usafiri wa anga na wengine ni wale waishio nchi za Afrika Kusini, Swaziland na Lesotho ambao wamejipanga kujitokeza uwanjani, Jumapili.

Kimenya alisema hamasa ya Watanzania inawapa deni wachezaji la kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mchezo huo muhimu kwa timu na nchi kiujumla.

"Tunawakaribisha kwa mikono miwili Watanzania wenzetu wanaokuja kutuunga mkono na tunawaombea wasafiri salama. Nimesikia kuna wengine watatokea huku Afrika Kusini kwenda Lesotho kutushangilia.

Watu wanavyotumia gharama zao kusafiri umbali mrefu kuipa sapoti timu, sisi wachezaji nadhani tunapaswa kuwapa furaha kwa kuhakikisha tunashinda," alisema Kimenya

Iwapo Stars ikiibuka na ushindi kwenye mchezo huo inaweza kufuzu moja kwa moja AFCON lakini pia ni iwapo Uganda itaifunga Cape Verde kwenye mechi itakayochezwa Kampala, Jumamosi Novemba 17.