Picha nzima Benchikha kusepa Simba ilianzia hapa

Muktasari:

  • Tetesi za kuondoka kwa Benchikha zilianza kuzagaa kwa muda mrefu, huku mara chache uongozi wa timu hiyo ukikanusha kuhusu suala hilo.

Baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha kuondoka, hatimaye timu hiyo sasa imebaki chini ya Juma Mgunda na Selemani Matola, lakini kuna maswali mengi ya kujiuliza ambayo yanatia shaka juu ya muenendo wa kikosi hicho.

Tetesi za kuondoka kwa Benchikha zilianza kuzagaa kwa muda mrefu, huku mara chache uongozi wa timu hiyo ukikanusha kuhusu suala hilo.

Benchikha mwenye wasifu mkubwa kuliko makocha wote ambao wamewahi kuifundisha timu hiyo, ameondoka kwenye timu hiyo baada ya kudumu kwa siku 157 pekee, akiwa ndiye kocha kwa miaka ya hivi karibuni aliyekaa kwenye timu hiyo kwa muda mfupi zaidi.

Taarifa ya klabu hiyo imesema kuwa kocha huyo aliomba kuvunja mkataba kutokana na kusumbuliwa na matatizo ya kifamilia, huku ikienda mbali zaidi ikisema anakwenda kumuuguza mke wake.

Hata hivyo, kumekuwa na maswali mengi kuhusu taarifa hiyo ya Simba, kwa kuwa wengine wanaamini kuwa suala la kumuuguza mke wake lilikuwa linaweza kubaki kwa kocha mkuu peke yake, kama ana mapenzi na Simba wasaidizi wake wangebaki hadi atakapomaliza matatizo yake na kurejea.

Lakini swali lingine ni je? Wakati Benchikha anauguza wasaidizi wake watakuwa hawana kazi na atauguza kwa muda gani? Kinachoonekana ni kwamba Simba na Benchikha walishindwana kwa mambo mengine na suala la kuuguza ni ishu ya ziada kabisa kwa kuwa angeweza kuondoka baada ya kumalizika kwa msimu jambo ambalo lingeisaidia timu hiyo kutafuta kocha bora sokoni.

Moja ya jambo linalotajwa kumuondoa kocha huyo ni gharama kubwa ambazo wamekuwa wakitumia kwa kocha huyo ikiwemo kuishi hotelini, lakini mshahara mkubwa aliokuwa analipwa wakati ambapo hakuna chochote Simba wanatarajia kuvuna kwa sasa hadi mwisho wa msimu.


DALILI KWAMBA ATAONDOKA:

SIMBA VS AL AHLY

Katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali kati ya Simba na Al Ahly, uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, Benchikha alionyesha hadharani kutoridhishiwa na kikosi cha timu hiyo baada ya kulala kwa bao 1-0.

Kocha huyo raia wa Algeria baada ya mchezo huo alisema: “Ninasikitika kwa kuwa Simba ina kikosi kidogo sana, ni wachezaji wachache ambao wana uwezo wa kuitumikia timu hii.” Kauli hii ambayo ilitolewa na kocha huyo ilionyesha kuwa ameshakata tamaa na kikosi hicho chenye makombe 22 ya Ligi Kuu Bara.


IHEFU VS SIMBA

Huu ulikuwa mchezo mwingine wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Liti Singida, Aprili 13, baada ya kubaki uwanjani peke yake kwa zaidi ya dakika saba baada ya mchezo kati ya timu hizo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Hali hii ilionyesha dalili kuwa kocha huyo ameshaanza kukata tamaa juu ya mwenendo wa timu hiyo na baada ya kuhojiwa alijibu:

“Ni hali ya kawaida, kubaki mwenyewe ni kitu cha kawaida kabisa kwangu nilikuwa natakafakari kwa kuwa sikuridhishwa na safu yangu ya ushambuliaji, tulikosa mabao mengi, nafikiri wakati mwingine tunatakiwa kuwa makini, lakini mwenendo wetu kwenye eneo hilo siyo mzuri, tazama tunatengeneza nafasi lakini tunashindwa kuzitumia,” hii ilikuwa kauli ya kocha huyo ya kuonyesha kukata tamaa.


MAZOEZINI MKIMYA SANA:

Taarifa zinasema kuwa wiki mbili za mwisho kocha huyo alionyesha mabadiliko makubwa sana mazoezini, akiwa haongei kama kawaida yake na wakati mwingine anafika na kuwapa programu wasaidizi wake na kukaa kwenye kiti nje.

“Alianza kuonyesha dalili kuwa hana furaha, kama ni ishu ya mke wake au hakuridhishwa na timu sijui, lakini tofauti na awali alikuwa anafika mazoezini muda mwingi anakaa nje na kuwapa programu ya mazoezi wasaidizi wake na Matola wasimamie.

“Wakati mwingine mwanzoni alikuwa anafanya hivyo, lakini anakuja uwanjani mara moja moja kuelekeza jambo, dakika za mwisho alikuwa hafiki kabisa kwenye uwanja hadi wakati ambapo wachezaji wamemaliza mazoezi, ikiwemo kambi ya Zanzibar na maandalizi ya Kombe la Muungano,” kilisema chanzo.


HISTORIA YAKE KWENYE TIMU:

Rekodi zinaonyesha kuwa Benchikha hana rekodi ya kukaa kwenye timu moja kwa muda mrefu, lakini pia kusema kuwa anaondoka kwa ajili ya matatizo ya kifamilia ni jambo la kawaida kwake.

Inaonekana kuwa pamoja na wasifu mkubwa alionao lakini hana uwezo sana wa kuishi kwenye presha kubwa au timu ikianza kuyumba.

Mwaka 2011, akiwa kocha mkuu wa Algeria alijiuzulu saa chache baada ya timu hiyo kufungwa mabao 4-0 na Morocco, jambo ambalo liliwashangaza wengi kutokana na jinsi alivyokuwa ameitengeneza timu hiyo.

Lakini pia mwaka jana akiitumikia USM Algier, ambayo aliipa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuitoa Yanga na kuipa timu hiyo ubingwa wa African Super Cup, alijiuzulu baada ya mashabiki kumzomea kwenye mchezo wa ligi, jambo ambalo wengi hawakuwa wanalitarajia kutokana na umaarufu na rekodi ambazo alikuwa ameziweka kwenye timu hiyo kwa muda mfupi.

Hapa pamoja na mambo mengine alisema anataka kwenda kushughulikia matatizo ya kifamilia yanayomkabili.