HISIA ZANGU: Rafiki zetu Mamelodi ni Simba na Yanga waliochangamka zaidi?

TULISHAMALIZANA na cheche za Abdelhak Benchikha. Ameondoka Msimbazi. Tuliambiwa juzi usiku na jana tumejadili suala lake. Labda jambo ambalo mashabiki wamekuwa wakijiuliza ni namna gani kocha anayekwenda kumuuguza mkewe aondoke na benchi lake lote la ufundi.

Jibu ni rahisi tu, kocha huwa anaondoka na benchi lake lote la ufundi kwa ajili ya kumpisha kocha ajaye aje na benchi lake la ufundi. Kusiwe na kisingizio. Kule England rafiki yetu, Jurgen Klopp amechoka na anataka kupumzika msimu wote ujao. Anaondoka na benchi lake lote la ufundi Liverpool hata kama wenzake hawajachoka.

Nawageukia rafiki zangu Mamelodi Sundowns. Wameondolewa na Esperance katika pambano la robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika. Kwa mara nyingine tena wamecheza dakika 180 bila kufunga bao lolote katika pambano la mtoano la michuano hii.


Walicheza dakika 180 dhidi ya Yanga isiyokuwa na Pacome Zouazoua, Yao Kouassi na Khalid Aucho. Dakika 90 za Dar es Salaam ilikuwa hivyo na walipokwenda Pretoria katika pambano la marudiano walicheza dakika 90 ikawa hivyo huku Yanga wakiendelea kuwakosa mastaa hao watatu. Sana sana ni wao ndio ambao walifungwa bao la Aziz Ki pale Pretoria mwamuzi akakataa. Waamuzi wa VAR wakakataa. Vinginevyo Ijumaa jioni Yanga wangekuwa wanacheza pambano la marudiano dhidi ya Esperance pale Temeke.

Mamelodi wanatisha sana? Ndio. Wanatisha sana lakini ni pale Afrika Kusini. Wametwaa taji la Ligi Kuu Afrika Kusini mara nane katika miaka tisa iliyopita. Kule wanaburuza na wamejitenga mbali na Kaizer Chiefs na Orlando Pirates ambazo zinaonekana uwekezaji umezidiwa na ule wa tajiri Patrice Motsepe. Huku Afrika? Huku kwingine nadhani tulikosea sana kuigopa Mamelodi kuliko Al Ahly. Sawa Mamelodi wametwaa taji hilo mara moja kitu ambacho Simba na Yanga hawajawahi kufanya lakini siku ile ambayo Mamelodi alipangwa kucheza na Yanga ilichukuliwa kama vile Mamelodi anabadilishana taji la Afrika na Al Ahly kitu ambacho si kweli.


Mamelodi imefika fainali mbili tu za Afrika. Ya kwanza ilikuwa 2001. Miaka 23 iliyopita.Ilifungwa na Al Ahly. Fainali za pili ni hizi alizocheza mwaka 2016 na kutwaa kombe chini ya Pitso Mosimane. Kufika fainali hizi Mamelodi alikuwa anashiriki kombe la Shirikisho lakini kwa bahati akachukua nafasi ya AS Vita ambayo ilishutumiwa kumchezesha mchezaji asiye halali katika pambano dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar.

Kuanzia hapo mwaka uliofuata 2017 akaishia robo fainali. Mwaka 2018 akaishia makundi. Mwaka 2019 kaishia nusu fainali. Kuanzia 2020 mpaka mpaka 2023 akaishia robo fainali. Mwaka huu ameishia nusu fainali.


Lazima tukubali kwamba kwa kufika fainali hizi mara mbili tayari ana rekodi nzuri kuliko Simba na Yanga. Kufika nusu fainali mara nne tayari ana rekodi nzuri kuliko Simba na Yanga. Hata hivyo kuna pengo kubwa kati ya Mamelodi na Al Ahly. Kuna pengo kubwa kati ya Mamelodi na wakubwa wengine wa Afrika ambao inawezekana kwa sasa wamelala.

Kuna pengo kubwa kati ya Mamelodi na TP Mazembe, Waydad Casablanca, Zamalek na Esperance. Wanaweza kuwa kiboko kwa Simba na Yanga lakini wapo daraja la kati halafu kuna wengine wapo daraja la juu zaidi. Tatizo walipopangwa na Yanga walionekana kuwa daraja la juu zaidi wakati sio kweli. Kwa mfano, wakati Simba akiishia katika robo fainali nyingi hapa miaka ya karibuni kumbe hata wao walikuwa wanaishia robo fainali. Ni mwaka mmoja tu walikwenda hatua ya mbele ya Simba mwaka 2019 wakati walipokwenda nusu. Na hizi ni nyakati ambazo Simba na Yanga zimeanza kuwekeza kwenye wachezaji wenye ubora zaidi kutoka nchi za kigeni tofauti na ilivyokuwa awali. Kumbe tukienda kuwekeza kwa wachezaji wenye ubora zaidi basi tunaweza kufika pale ambapo Mamelodi wanafika.


Kwa mfano, nimetazama mechi zote mbili za Mamelodi na Esperance nimegundua kwamba Yanga wangeweza kufika fainali hizi za Ligi ya mabingwa msimu huu. Zilikuwa mechi mbili za kawaida za soka ambazo Yanga angezimudu. Ni vile tu bao la Aziz Ki lilikataliwa Pretoria. Nimeitazama Al Ahly ya nyakati hizi wakati ilipocheza mechi nne dhidi ya Simba. Mbili za Super League ambazo zote ziliisha kwa sare na mbili za robo fainali. Sawa Al Ahly ni timu nzuri lakini Simba hii ingekuwa ile ya akina Louis Miquissone, Clatous Chotta Chama, Hassan Dilunga, Larry Bwalya, Chris Mugalu, John Bocco, Meddie Kagere, Bernard Morrison katika ubora wao hadithi ingeweza kuwa tofauti. Kwani Al Ahly hawa ndio akina Barakat?

Wachezaji wa bei ghali? Ni kweli wapo. Pale Mamelodi wapo kina Gaston Sirino, Marcelo Alliende na wengineo. Wamenunuliwa kwa bei ambayo inaweza kuwa bajeti ya kuendesha Simba na Yanga kwa msimu huu. Ni kweli wanaleta tofauti lakini subiri kwanza. Kuna jambo ambalo mashabiki wengi hawalielewi. Hawa wachezaji huwa wananunuliwa kutoka katika nchi ambazo pesa zao ziko juu na wanakwenda katika nchi ambayo pesa yao ipo juu. Mchezaji kununuliwa kwa dola milioni moja ya Marekani ambayo ni sawa na Bilioni 2.5 za Kitanzania. Hata hivyo ni sawa na Rand milioni 18 ambazo uchumi wa Motsepe ni pesa ya kawaida.

Ni sawa na kunywa bia moja Pauni 3 katika baa moja pale London. Pauni 3 ni bei ya kawaida Uingereza, lakini huku ni zaidi ya Sh10,000. Ukitafsiri pesa kwa namna hii lazima utaona Simba na Yanga zipo bado kwa matumizi. Hata hivyo sio lazima mchezaji wa bei hii awe wa ajabu uwanjani. Ndio dau lake. Simba inawezekana imempata Ayoub Lakred bure lakini Ayoub akirudi kwao akacheza Berkane kisha akauzwa kwenda USM Alger dau lake utasikia dola milioni mbili. Hapa kwetu dau lake linaweza kuwa Sh200 milioni kama Azam watamtaka. Ni kutokana na thamani ya pesa yetu. Wakati mwingine unazitazama Mamelodi na Al Ahly zinacheza na Simba na Yanga na hauoni mchezaji wa Sh6 bilioni uwanjani. Ni kutokana tu na thamani za pesa zao zilivyo. Hawawezi kuuziana mchezaji kwa dola laki mbili kwa sababu thamani hiyo kwao ilikuwa miaka 20 iliyopita.