Mashabiki Mbeya City, Yanga wavimbiana

Wakati mashabiki wa Yanga wakisisitiza kushinda mechi ya leo ili kuendeleza furaha, wapinzani wao Mbeya City wamesema mchezo wa leo ni fainali kwao kukwepa kushuka daraja.

Timu hizo zinakutana saa chache zijazo kwenye uwanja wa Sokoine jijini hapa, ikiwa wa raundi ya 29 na kila upande unatamani ushindi.

Yanga ndio vinara wa ligi kwa pointi 74 akiwa tayari ameshatwaa ubingwa, huku City akiwa na pointi 30 katika nafasi ya 12.

Samson Daud shabiki wa Mbeya City amesema ana matumaini timu hiyo itashinda kutokana na mahitaji yao katika kukwepa kushuka daraja.

Amesema kinachowapa matumaini zaidi ni kutokana na wapinzani kuchoka kwani hata mazoezi hawakufanya akibainisha kuwa leo ni fainali kwao.

"Hata mabao mawili yatatosha kimsingi tupate ushindi na leo ni fainali kwetu ukizingatia matokeo tuliyonayo tunaamini vijana wetu watafanya kweli" amesema Daud.

Kwa upande wake Hanifa Jason shabiki na mkereketwa wa Yanga tawi la Uyole amesema wanachotaka wao ni ushindi ili kuendeleza furaha licha ya kuwa wameshatwaa ubingwa.

"Sisi hatujui cha kushuka au kutoshuka Mbeya City, tunachotaka ni ushindi ili tukabidhiwe kombe kwa heshima hii ni timu kubwa na ina hadhi yake" ametamba Hanifa.