Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mashabiki Man United wavamia nyumbani kwa Ed Woodward

Muktasari:

Woodward, 48, mkewe na watoto wao pacha hawakuwapo nyumbani wakati wahuni hao walipovamia na kurusha mioto hiyo ndani kupitia getini.

MANCHESTER,ENGLAND. UNAAMBIWA hivi, usithubutu watu wakuchoke hawatakuwa na uvumilivu zaidi. Kwa muda mrefu mashabiki wa Manchester United wamekuwa wakipiga kelele kuhusu bosi anayehusika na usajili kwenye timu hiyo, Ed Woodward hafai, anapaswa kufukuzwa na sasa wameamua kuchukua uamuzi wao.

Mashabiki hao wa Man United juzi Jumanne walikusanyika na kwenda moja kwa moja nyumbani kwa makamu mwenyekiti wa klabu yao, Ed Woodward kurusha mienge ya moto ikiwa ni sehemu ya maandamano yao ya kupinga umiliki wa familia ya Glazer.

Kundi la mashabiki kati ya 20 na 30 walikwenda nyumbani kwa Woodward huko Cheshire baada ya kuchukizwa na uendeshaji wa timu yao ambayo usiku wa jana Jumatano ilitarajia kumenyana na Manchester City katika mechi ya pili ya marudiano ya nusu fainali.

Mienge kadhaa ya moto ilirushwa kwenye nyumba hiyo iliyowekewa uzio na kuripotiwa kulikuwa na baruti pia zilizolipuka huku ikielezwa michoro mbalimbali ilichorwa kuzunguka uzio wa nyumba ya bosi huyo anayelipwa karibu Pauni 3 milioni kwa mwaka.

Woodward, 48, mkewe na watoto wao pacha hawakuwapo nyumbani wakati wahuni hao walipovamia na kurusha mioto hiyo ndani kupitia getini.

Kundi hilo la mashabiki wa Man United linalotambulika kwa jina la ‘The Men in Black’ lilidaiwa kufanya tukio hilo huku wakiwa wamevaa nguo nyeusi. Man United ilitoa taarifa: “Klabu ya soka ya Manchester United inafahamu usiku mmoja kulitokea tukio la uvamizi kwenye moja ya makazi ya waajiri wake. Tunafahamu wapenda soka wote duniani wataungana na sisi na tunaamini polisi wa Manchester watawatambua watu waliohusika na tukio hilo.

“Yeyote atakayekumbwa na hatua kwenye jambo hilo, atafungiwa maisha kuhudhuria mechi za Man United na atafunguliwa mashtaka. Mashabiki kuwasilisha maoni yao ni jambo jingine na kufanya uhalifu wenye lengo la kuharibu mali na maisha ya wengine ni jambo jingine. Hakuna huruma kwenye hili.”

Huu ni mwendelezo wa mashabiki kupingana na umiliki wa familia ya Kimarekani katika timu hiyo ya Man United na walianza kupinga tangu mara ya kwanza walipokuja na wazo la kuinunua karibu miaka 15 iliyopita.

Man United inaripotiwa kuwa na madeni zaidi ya Pauni 200 milioni licha ya kutangazwa kupata faida kila mwaka tangu Woodward alipochukua kiti hicho cha ubosi kutoka kwa David Gill mwaka 2013.

Inaalezwa familia hiyo ya Glazer imechukua zaidi ya Pauni 1.3 bilioni kutoka Old Trafford kwenda kulipia madeni yao binafsi.

Mashabiki hao wa Man United walisikika wakiimba nyimbo za vitisho vya kumuua Woodward kwenye mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Tranmere wikiendi iliyopita.

Wimbo wa kwanza ulikuwa na maneno ya kutengeneza tanuru la moto, kisha kumweka Glazers juu na Ed Woodward katikati ili kuwachoma kabisa, wakati mwingine ulikuwa na maneno ya Ed Woodward anapaswa kuuawa, atakufa vipi bado haieleweki, pengine ya kumnyofoanyofoa kuanzia kichwa hadi vidole, lakini Woodward lazima auawe.

Hayo ni baadhi ya maneno yaliyokuwa kwenye nyimbo za mashabiki hao wakati Man United ilipocheza na Tranmere.

Tangu mwaka 2013, Man United imetumia Pauni 850 milioni kwenye usajili, lakini kitu ambacho imefanikiwa ni kubeba tu Kombe la FA, Europa League na Kombe la Ligi.

Kutokana na hilo, lawama zote anafikishiwa Woodward kwa kushindwa kuleta wachezaji wa maana kwenye timu ili kuwa na ushindani mkali katika ligi mbalimbali. Wanalaumu pia uongozi wa Man United kwa sasa umekuwa ukifanya mambo kwa kuwafurahisha wenye hisa zao kuliko kutafuta mafanikio ya ndani ya uwanja.

Timu hiyo yenye maskani yake Old Trafford bado haijafanya usajili wowote ndani ya dirisha hili la Januari huku wakielezwa ipo kwenye hatua za mwisho za kumnasa Bruno Fernandes wakati dirisha linatarajia kufungwa kesho Ijumaa.

Fernandes jana Jumatano alitarajia kuwasili England kwenda kufanyiwa vipimo vya afya baada ya Man United kufika makubaliano na klabu yake ya Sporting CP.