MARA PAAP!! Wema sepetu azidi kunoga

ACHANA na ile video yake iliyozagaa mitandaoni hivi karibuni akiimba wimbo wa msanii wa Hip Hop anayetamba na wimbo wa Wowowo, Zaiid akiwa ndani ya Bwawa la kuogelea. Ikaushie kwanza hiyo.
Wema Sepetu amezidi kuwa mtamu unaambiwa na sasa ndiyo gumzo la mjini huko kwenye tasnia ya Filamu za Bongo.
Mrembo huyo mwenye mvuto wa ajabu na anayekubalika kila pembe ya nchi hii, hivi karibuni amechukua tuzo mbili na kuwaacha Bongo Muvi wote midomo wazi.
Tuzo ya kwanza kunyakua ni ile ya Mwigizaji kipenzi cha watazamaji (Best Viewers Choice) na nyingine ni ya Mwigizaji Bora wa Kike. Kwa nini wasanii wenzake wasibaki midomo wazi.
Tuzo hizo alizichukua wikiendi iliyopita kwenye usiku wa tuzo za Ziff zilizoandaliwa na Azam TV ambacho ndicho kituo bora cha Televisheni kwa sasa hapa nchini.
Mara tu baada ya kushinda tuzo hizo, Mwanaspoti lilipiga stori mbili tatu na Wema na mbali na kuzizungumzia tuzo hizo, pia alizungumzia mambo mengine kumhusu.
Mwanaspoti: Mambo vipi Wema?
Wema: Nzuri, uko poa wewe?
Mwanaspoti: Niko poa na hongera sana kwa kunyakua tuzo mbili.
Wema: Asante sana, nawashukuru mashabiki wangu kwa kunipigia kura na nawahidi sitawaangusha kwani huu ni mwanzo tu.
Mwanaspoti: Unachukuliaje baadhi ya wasanii wenzako kukukaushia na kuacha kukupa hongera na baadhi ya watu kusema umependelewa kupewa tuzo hizi?
Wema: Hiyo ya wasanii wenzangu kutokuniposti mie naona kila mtu na roho yake maana kama unavyojua ya moyoni mwa mtu huwezi kuyajua.
Pia inawezekana wako bize hivyo hawana muda wa kuingia kwenye mitandao na hata hivyo haijaandikwa kuwa lazima ipostiwe mtu akishinda, ila upendo ni kitu kizuri sana katika maisha yanayotuzunguka.
Kuhusu hiyo ya baadhi ya watu kusema mimi nimependelewa, mie naona hao hawafuatilii kazi zangu na ukute sio kati ya watu walionipigia kura.
Mwanaspoti: Huko kwenye mitandao ya kijamii na nje ya mitandao watu wanadai hukupenda kitendo cha Diamond Platinumz kumkumbatia Hamisa Mobetto pale jukwaani wakati wa utoaji tuzo za Sinema zetu pale Mlimani City.
Wema: Unajua nawashangaa sana watu wanaosema eti nimechukia kuona vile, kwanza kwa nini nichukie wakati wale ni wazazi, wana mtoto wale, mie kwanza nimefurahi kuona vile sababu mabifu sio mazuri na hasa mkiwa wazazi.
Mwanaspoti: Inasemekana umerudiana na Diamond na ndio maana kila sehemu ya starehe mnakuwa pamoja.
Wema: Hapana, sijarudiana na Diamond na kuwa pamoja katika sherehe ni moja ya kazi, yaani Diamond kwa sasa amekuwa rafiki yangu tu wa kawaida. Ningerudiana nae wewe ungejua na ningekwambia dada yangu.
Mwanaspoti: Hivi karibuni kuna kipande cha video kilikuwa kina sambaa katika mitandao ya kijamii kinakuonyesha ukiwa unaogelea, lakini kimezua sana mjadala wengi wakidai usingeacha wazi maumbile yako vile, we unasemaje kwa hilo?
Wema: Mimi nawashangaa sana watu wanaojadili mimi kuogelea, hivi watu walikuwa wanataka mimi niogelee na suti? Japo najua wangesema pia hata kama ningefanya hivyo.
Mwanaspoti: Ni kweli umetumia dawa kukuza makalio?
Wema: Sio kweli, watu wanaosema hivyo hawaijui familia yetu. Nikuze makalio sasa ili iweje? Tena wangejua watu hili umbo nalichukia balaa.
Mwanaspoti: Umekuwa na sifa ya kubadilisha marafiki yaani hukai nao muda mrefu, kwa nini?
Wema: Hilo nimeshaliona siku nyingi, sina bahati kabisa kwa kweli, yaani hata nimpende vipi rafiki hata nikiwa na marafiki nawapenda itafikia muda tunakuja kukorofishana tena kwa kitu kidogo tu au utakuta mtu anakununia bila sababu. Sasa kwa aliyembali na sisi anaona mimi ni tatizo.
Mwanaspoti: Kwa sasa unaonekana umerudisha urafiki na Aunt Ezekiel ambaye mliwahi kugombana hadi mkaapizana na kuandikwa katika vyombo vya habari, imekuwaje?
Wema: Yaa nipo na Aunt kwa sasa, tumeamua tuwe pamoja sababu tumekua na kila mmoja alishatambua kosa lake, hivyo tumeanza upya.
Mwanaspoti: Nipe ratiba yako ya kila siku.
Wema: Huwa naamka saa mbili au saa tatu asubuhi, inategemea nataka kufanya nini siku hiyo.
Kitu cha kwanza nafanya kazi za nyumbani kama mwanamke mwingine, pia napika chakula kwani napenda sana kupika kama nikiwa nyumbani, na kwa kuwa sipendi sana kutokatoka huwa napenda kuangalia movie.