Manyama aikacha Namungo

DIRISHA dogo la usajili limefungwa rasmi huku beki Edward Charles akiachana na Namungo FC inayoshiriki michuano ya kimataifa ambapo amejiunga na Ruvu Shooting ya Pwani.

Manyama ameichezea Namungo FC msimu mmoja pekee ambapo timu hiyo inashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi.

Imeelezwa kuwa mchezaji huyo ambaye aliwahi kuzichezea Yanga, JKT Tanzania, Oljoro, Kanembwa ameamua kujiunga na Ruvu Shooting baada ya mkataba wake kumalizika na kushindwa kufikia makubaliano ya kimkataba na viongozi wake.

Ruvu Shooting umetangaza rasmi wachezaji watano wapya waliowasajili katika dirisha dogo akiwemo Manyama aliyekuwa akitajwa kuwaniwa Yanga na kutua kwake Ruvu itakuwa ni mara ya pili kuichezea timu hiyo.

Nyota hao ni Adam Stanley Kiondo (Yanga), Haruna Hamis Fadhir (huru), Haji Mwinyi Mngwali (KMKM), Manyama (Namungo) na James  Msuva (KMC).

Katika taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa timu hiyo, Masau Bwire ilidaiwa kuwa usajili huo ni mapendekezo ya Benchi la Ufundi chini ya kocha wao Charles Boniface Mkwasa.