Manula: Nina jambo langu Afrika

Wednesday July 21 2021
manula pic
By Thomas Ng'itu

KIPA wa Simba, Aishi Manula ameweka wazi kwamba kipa bora wa msimu kwa misimu mitano inatosha na sasa anafikiria zaidi kuwa kipa bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Licha ya Manula kuchukua mara tano - akichukua mara mbili akiwa Azam na mara tatu akiwa na Simba, lakini bado anatazamiwa kuchukua mara ya sita akiwa na Wekundu hao msimu huu baada ya kumaliza Ligi Kuu Bara akiwa hajafungwa takribani mechi 18.

“Nadhani niwe muwazi kitu ambacho nafikiria kwa sasa ni kuwa kipa bora wa Afrika, kuchukua mara sita mfululizo (Bara) najua hata wewe ukisikia nimechukua tena wala hautashtuka,” alisema Manula ambaye ni mchezaji wa zamani wa Azam.

“(Wachezaji) tunashirikiana vizuri kuanzia mazoezini mpaka kwenye mechi, ligi ilikuwa ngumu, ukiangalia tulikuwa na msimu ambao ulikuwa na corona pia, ila kama wachezaji tulipambana na kuchukua ubingwa.”

Manula aliongeza kuwa: “Makipa wapo wengi, lakini kutoruhusu (bao) ni kitu kigumu, binafsi sio kwamba napanga kuwa hivyo, lakini Mwenyezi Mungu ananisaidia. Kuna muda unaweza ukasema ngoja nikapambane nisiruhusu bao, lakini ukienda unaruhusu, kikubwa tuendelee kupambana.”

Manula ameendelea kushikilia nafasi ya kipa namba moja katika kikosi cha Simba kwa misimu minne mfululizo, huku makipa mbalimbali wakishindwa kufua dafu mbele yake.

Advertisement
Advertisement