Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Manqoba Mngqithi afunguka alivyotua Yanga, benchi jipya analounda lipo hivi

KOCHA Pict


KOCHA mpya wa Yanga, Manqoba Mngqithi amesema amevutiwa na maono makubwa ya mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akisisitiza kuwa sababu kubwa iliyomfanya akubali kazi hiyo ni dhamira ya klabu ya kutaka kufanya makubwa zaidi katika Ligi ya Mabingwa Afrika.


Mngqithi ambaye ametangazwa rasmi kuwa mrithi wa Pedro Goncalves, ametoa kauli hiyo kwa mara ya kwanza akiwa Afrika Kusini, ikiwa ni siku chache kabla ya kutua nchini kuanza maandalizi ya msimu mpya yatakayofanyika Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam.


Kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa wa soka la Afrika, alisema kurejea katika mazingira ya ushindani wa Ligi ya Mabingwa Afrika ni jambo ambalo amekuwa akilitamani kwa muda mrefu.

“Ninafurahia changamoto hii mpya. Nilikuwa natamani kurejea kwenye mazingira ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuona tunaweza kufika wapi. Yanga ni klabu yenye malengo makubwa na inaendelea kusajili wachezaji watakaotusaidia kutimiza malengo yetu,” alisema Mngqithi katika mahojiano na SABC Sport.

Alisema kilichomvutia zaidi ni namna Yanga ilivyojengwa kitaalamu na jinsi viongozi wake walivyowasilisha mpango wa maendeleo ya timu.

“Ni klabu yenye mfumo wa kitaalamu sana, jambo ambalo limenipa moyo mkubwa. Hii ni nafasi ambayo nilikuwa naisubiri kwa muda mrefu, kurejea tena kwenye ushindani wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Sasa tusubiri tuone nitafika mbali kiasi gani katika soka la Afrika Mashariki,” alisema.

KOCH 01

JINSI ALIVYOTUA YANGA

Akizungumza na Soccer Laduma, wakala wa Mngqithi, Mike Makaab, alisema viongozi wa Yanga walikuwa wazi tangu mwanzo katika mazungumzo ya kumchukua kocha huyo.

“Mambo yalikwenda kwa haraka sana. Nilipata taarifa kwamba walikuwa na nia ya kupata huduma zake. Nilizungumza moja kwa moja na rais (Hersi Said) pamoja na Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu (Andre Mtine).

“Hii ni klabu ambayo imeshinda ubingwa mara tano mfululizo (Ligi Kuu) na lengo lao kubwa ni kuboresha rekodi yao katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Huu ulikuwa mradi uliomvutia kocha na sasa atarejea tena kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Makaab.

Makaab aliongeza kuwa, huu ni mwanzo wa safari ya Mngqithi nje ya Afrika Kusini, na waliamini Yanga ndiyo mahali sahihi pa kuanzia.

“Hii ni mara yake ya kwanza kufanya kazi nje ya nchi na tulihisi Yanga ndiyo sehemu sahihi kwake kuanza. Ni klabu yenye weledi mkubwa. Nimefanya nao mikutano kadhaa kwa njia ya mtandao na nimevutiwa sana na namna walivyo wa kitaalamu na walivyo wazi katika mazungumzo yao. Hakukuwa na ajenda zilizofichwa, jambo ambalo nimelifurahia sana. Uzoefu wangu wa kwanza kufanya kazi na Yanga umekuwa wa kufurahisha na wa kitaalamu.”

Mngqithi anawasili Yanga akiwa na wasifu mkubwa katika soka la Afrika. Aliwahi kuwa msaidizi wa kocha maarufu Pitso Mosimane katika kikosi cha Mamelodi Sundowns kabla ya baadaye kupandishwa kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo, ambako alichangia mafanikio kadhaa ikiwemo kutwaa mataji ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Baada ya kuondoka Sundowns, alipata nafasi ya kuinoa Lamontville Golden Arrows, lakini sasa ameamua kuanza ukurasa mpya nchini Tanzania akiwa na jukumu la kuendeleza ubabe wa Yanga ndani ya nchi na kuipa ushindani mkubwa barani Afrika.

Ujio wake pia unaongeza ushindani wa makocha kutoka Afrika Kusini katika Ligi Kuu Tanzania Bara, kwani watani wa jadi wa Yanga, Simba, wanaongozwa na kocha mwingine kutoka taifa hilo, Steve Barker.

Katika miaka ya karibuni Yanga imekuwa ikivutia makocha waliowahi kufanya kazi Afrika Kusini, akiwemo Nasreddine Nabi, Miguel Gamondi, Luc Eymael, Sead Ramovia, Patrick Mabedi na Romain Folz, hali inayoonyesha klabu hiyo imeendelea kujenga hadhi yake katika soka la ukanda huu.

Mngqithi anarithi kikosi kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya Simba msimu uliopita, lakini matarajio makubwa ya viongozi na mashabiki ni kuona timu hiyo ikivuka hatua ambazo imekuwa ikikwama katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

KOCH 02

BENCHI JIPYA

Baada ya Mngqithi kutambulishwa, pale Yanga kumeanza kuchomoza ‘thank you’ wakiaga makocha wawili wa kigeni waliomaliza msimu na mabingwa hao.

Hivi karibuni, kuna makocha wawili wameaga ndani ya Yanga akiwemo aliyekuwa msaidizi wa kwanza wa Pedro Goncalves, Mathew Silva ambaye alimaliza msimu wakati Mreno huyo akiondoka Mei 6, 2026.

Baada ya Silva, akafuata kocha wa makipa, Fernando Perreira ambaye awali alikuja na Perdo wakati anatua Yanga, na hata alipoondoka bosi wake akasalia akimaliza msimu na klabu hiyo. Makocha hao wote wameshukuru maisha ya ndani ya timu hiyo.

Kuondoka kwa makocha hao, Mwanaspoti linafahamu kwamba, Mngqithi anakuja na makocha watakaoziba nafasi hizo mbili na wengine wawili katika kuliunda benchi lake la ufundi mara tu baada ya kuatua nchini.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinabainisha kwamba, Mngqithi amekubaliana na mabosi wa klabu hiyo kuwa ataendelea kufanya kazi na Abdihamid Moallin ambaye alikuwa kama kaimu kocha mkuu akiwapa ubingwa timu hiyo baada ya kuondoka kwa Pedro.

Licha ya kumbakisha Moallin, kocha huyo raia wa Afrika Kusini anakuja na kocha mwingine ambaye atakuwa msaidizi wake wa pili kwenye benchi hilo na kufanya kuwa na wasaidizi wawili wa kwanza.

Ukiacha msaidizi huyo wa kwanza, kocha huyo anakuja na mtaalam wa kutunza taarifa za ubora na viwango wa wachezaji wa timu (Perfomance analyst).

Mtu wa tatu ambaye ataungana na kocha huyo ni mchambuzi wa video ambaye atafanya wataalam hao kuwa wawili kwenye kikosi hicho, akiungana na Msauzi mwingine Thulani Thekiso ambaye anabaki kuendelea na majukumu hayo.

Kocha Mngqithi pia analeta kocha mwingine wa makipa kwenye kikosi hicho ambaye sasa atakuja kuchukua nafasi ya Perreira aliyeaga juzi kuwa anasepa kupisha watu wapya.

Aidha, kocha huyo amembakisha kocha wa mazoezi ya viungo, Chyna Mokaila raia wa Botswana akiwathibitishia mabosi wa klabu hiyo kuwa anamjua jamaa huyo na kazi yake ni nzuri.

Awali upepo haukuwa vizuri kwa Mokaila wakati Yanga ikiwa haifanyi vizuri chini ya Pedro msimu uliopita, ilibaki kidogo atolewe kabla ya uamuzi huo kusitishwa na sasa kocha mpya amembakisha zaidi.

Bosi mmoja wa juu wa Yanga ameliambia Mwanaspoti kuwa, watu hao wanne ni ujio wa awali na kwamba Mngqithi anaweza kuja kuongeza wengine kulinagana na majukumu ambayo atayaona mara baada ya kuanza kazi.

“Nikweli kuna hao watu wanne anakuja nao lakini ninachofahamu hao ni watu wa awali, kuna uwezekano akaongeza wengine lakini atafanya hivyo mara baada ya kuanza kazi na kuangalia majukumu ya ndani ya timu,† alisema bosi huyo wa juu wa Yanga.

Wakati huohuo, taarifa zinabainisha kwamba, performance analyst ambaye anatarajiwa kutua na kocha mpya ndani ya Yanga ni Yardaan Valodia naye ni raia wa Afrika Kusini.

Valodia aliwahi kufanya majukumu hayo katika Klabu ya Golden Arrows ambayo pia Mngqithi ameifundisha, jambo linaloonyesha uhusiano mzuri kwa makocha hao wanaotaka kuungana tena wakiwa na Yanga.

Mtaalamu huyo amewahi kufanya pia kazi Moroka Swallows na Mamelodi Sundowns zote za Afrika Kusini na umahiri wake mzuri wa utendaji umesaidia benchi la ufundi la timu za vijana za Afrika Kusini chini ya miaka 17 na 20 na kuchangia kutwaa ubingwa wa AFCON 2025.

Valodia aliisaidia timu ya vijana ya Afrika Kusini chini ya miaka 20 kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika (CAF U-20 AFCON) mwaka 2025, baada ya kikosi hicho kuifunga Morocco bao 1-0, katika mechi ya fainali iliyochezwa Misri, Mei 18, 2025.

Taarifa kutoka Afrika Kusini zinaeleza kuwa: “Inaaminika tayari amejiunga. Ninayemfahamu ni Yardaan Valodia, lakini kocha pia anatarajiwa kuja na baadhi ya watu wake wa benchi la ufundi, wakiwemo kocha wa viungo, mchambuzi wa video, kocha wa makipa na kocha msaidizi,” chanzo hicho kilisema.

Iwapo hatua hiyo itakamilika, itakuwa ni mwendelezo wa ushirikiano kati ya Mngqithi na Valodia, ambao waliwahi kufanya kazi pamoja katika Mamelodi Sundowns kabla ya kuungana tena Golden Arrows.

Valodia anamiliki leseni ya ukocha ya CAF C Licence, huku pia akiendelea kujiendeleza kupitia programu za mafunzo ya ukocha zinazohusishwa na FC Barcelona.

KOCH 05

DANI CADENA NDANI

Taarifa zinabainisha kwamba, mabosi wa Yanga wamefungua mazungumzo na aliyekuwa Kocha wa Makipa wa Simba, Dani Cadena raia wa Hispania, huku pia akiwahi kuwanoa makipa wa Azam.

Akizungumza na Mwanaspoti, Cadena licha ya kutotaka kueleza zaidi juu ya hilo, aliliambia Mwanaspoti ni kweli kuna ofa ya kujiunga na kikosi hicho, ingawa bado hawajafikia makubaliano ya mwisho, kwani anachoangalia ni machaguo yake.

Cadena aliyefanya pia kazi akiwa Kaimu Kocha Mkuu wa Simba baada ya Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kuondolewa, aliondoka ndani ya kikosi hicho Mei 20, 2024, kufuatia kukitumikia kwa siku 319, tangu alipojiunga nacho Julai 6, 2023.

Kocha huyo anayefanya kazi Hatta Club ya Falme za Kiarabu (UAE), alijiunga na Simba akirithi nafasi ya aliyekuwa kocha wa makipa Mmorocco, Chlouha Zakaria aliyeondolewa ndani ya kikosi hicho, ambapo kwa sasa Yanga inataka kumleta Tanzania.

Kocha huyo aliyezaliwa Januari 3, 1978 katika kisiwa cha Baleares Mallorca, Hispania ni msomi wa mpira wa miguu mwenye leseni ya Uefa Pro ambayo ndio kubwa zaidi barani Ulaya na amewahi kufanya kazi katika klabu za Sevilla, Real Betis na Recreativo Huelva.

Mara ya kwanza kwa Cadena alitua nchini kujiunga na Azam Julai Mosi, 2022, huku akifanya kazi pia klabu za Guangzhou Mingtu na Shanghai Jiading za China akiwa na uzoefu mkubwa na elimu ya juu ya Shirikisho la Soka la Barani Ulaya (UEFA).

KOCH 04

WASIKIE YANGA

Uongozi wa Yanga, umeweka wazi mpango wake wa kuboresha benchi la ufundi kuelekea msimu ujao, ukieleza kutakuwa na mabadiliko kadhaa yatakayolenga kuendana na mahitaji ya soka la kisasa.

Akizungumzia muundo wa benchi la ufundi, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, alisema msimu uliopita walitumia mfumo wa makocha wenza baada ya aliyekuwa kocha mkuu, Pedro Goncalves kuondoka Mei 6, 2026.

Katika mfumo huo, badala ya kuwa na kocha msaidizi mmoja na mwingine mkuu, waliwatumia Abdihamid Moallin na Patrick Mabedi kufanya kazi kwa pamoja kama makocha wenza.

Aidha, Matthew Silva alipewa jukumu maalum la kusimamia mipira iliyokufa (set pieces).

Kuelekea msimu ujao, Yanga inambakisha Moallin ambaye anakuja kufanya kazi katika benchi jipya la ufundi litakaloongozwa na Mngqithi, huku mazungumzo ya kuongeza mkataba wake yakiwa katika hatua nzuri.

“Moallin atabaki kwenye klabu yetu. Tunafanya mazungumzo naye na matarajio ni kwamba ataendelea. Hatutakuwa na kocha msaidizi namba moja wala kocha msaidizi namba mbili, bali tutakuwa na makocha wasaidizi wawili watakaomsaidia kocha mkuu,” alisema.

Aliongeza kuwa, kocha mkuu mpya atakuja na msaidizi wake pamoja na mchambuzi wa video (video analyst), huku Yanga pia ikiendelea kubaki na mchambuzi wa video aliyekuwepo msimu uliopita. Kutokana na hatua hiyo, Yanga itakuwa na wachambuzi wawili wa video kwa mara ya kwanza.

“Watu wanaweza kushangaa kwa nini tuna video analyst wawili, lakini ukiangalia soka la kisasa na uzoefu tulioupata, hata Afrika Kusini kuna idara maalum ya uchambuzi wa video yenye wataalamu wengi. Nasi tumeona ni muhimu kuwa na wawili ili kuongeza ubora wa maandalizi ya timu,” alieleza.

Kuhusu kocha wa viungo, Kamwe amethibitisha kuwa kocha mkuu mpya ameridhishwa na uwezo wa Chyna Mokaila na amependekeza aendelee kubaki.

“Kocha anamfahamu Chyna na ameomba tuzungumze naye kuhusu kuongeza mkataba. Tukikubaliana ataendelea, lakini kama hatutafikia makubaliano tutamjulisha kocha mkuu ili atuletee chaguo lingine,” alisema.

Mbali na hilo, Yanga inapanga kuanzisha nafasi maalum ya mtaalamu wa mipira iliyokufa, hatua inayolenga kuongeza makali ya timu kwenye maeneo hayo muhimu.

“Soka limebadilika sana. Sasa timu kubwa duniani zina wataalamu wa set pieces (mipira iliyokufa), nasi tunafuata mwelekeo huo. Kwa hiyo msimu ujao tutakuwa na mtu maalum wa kazi hiyo. Mkiona Yanga inaanza kufunga mabao mengi kupitia mipira iliyokufa kama Arsenal, msishangae,” alisema.


KAMBI AVIC TOWN

Wakati huo huo, Kamwe alisema maandalizi ya msimu ujao wa 2026-2027 yataanza rasmi Julai 20, 2026 katika kambi ya Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam, mara baada ya kocha mpya kuwasilisha mpango wake wa maandalizi kwa uongozi wa klabu.

Kamwe alisema siku ya kwanza itahusisha vipimo vya afya kwa wachezaji kabla ya kuanza mazoezi rasmi.

“Tarehe 20 timu itaripoti kambini. Baada ya vipimo vya afya tutaingia Avic Town na kuanza maandalizi rasmi. Safari hii hatutakwenda nje ya nchi kwa sababu muda uliobaki kabla ya msimu kuanza ni mfupi,” alisema Kamwe.

Aliongeza kuwa kambi hiyo itakuwa ya siri na yenye ulinzi mkali ili kuwapa benchi la ufundi mazingira bora ya kuijenga timu.