Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kinachomsubiri Manqoba Jangwani kinatisha

HISIA Pict


JINA lake ni gumu kutamkika lakini kazi kubwa inayomkabili mbele yake haitaangaliwa kwa jina lake. Kocha mpya wa Yanga, Manqoba Mngoithi ana kazi nzito ambayo inamkabili mbele yake.


Nilihesabu kwa vidole nahisi Yanga wanaweza kusajili hata wachezaji nane wa kigeni katika dirisha hili. Sioni jina la Pacome likiwekwa katika orodha ya wachezaji wapya. Prince Dube amerudi kwao.


Frank Assinki na Mohamed Damaro sidhani kama watendelea kuwa wachezaji wa Yanga tena. Lassine Kouma ni wazi kwamba ataondoka. Chadrack Boka pia anaweza kwenda zake. Injinia Hersi Said na genge lake wana nafasi kubwa ya kuisuka Yanga mpya.

Hata kwa wachezaji wa ndani kocha huyu anaweza kuwa katika bahati mbaya ya kutokuwa na mastaa wawili tegemeo kikosini ambao hatujui kama watakuwa tayari kwa msimu mpya. Mlinzi Dickson Job na mshambuliaji, Clement Mzize.

HISI 01

Yanga wanaweza pia kuchukua wachezaji wapya wazawa katika nafasi hizo. Wanaweza pia kuchukua wachezaji wengine wa kigeni katika nafasi hizo kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao.

Hapa ndipo Manqoba atakapojikuta kuwa kocha mpya katika Kundi la wachezaji wapya. Bahati mbaya kwake ni kwamba hatapewa muda. Hii sio tabia ya Yanga tu. Ni tabia ya mpira wa Afrika. Hakuna kitu kinachoitwa ‘project’.

Na timu zetu kubwa ndio hazina kabisa kitu hiki. Watu wanataka matokeo bora kwa muda huo huo. Hawana muda wa kusubiri. Muulize Roman Folz. Alidhani Yanga wangempa muda wa kutosha kutengeneza timu. Siku za mwanzo tu wakaachana naye.

Bahati mbaya kwa Manqoba ni kwamba hatapewa muda huo. Ametangulia kutangazwa katika timu huku rundo kubwa la wachezaji wapya likiwa njiani kutua jangwani. Na mechi yake ya kwanza atacheza na Simba.

HISI 02

Yote haya yanatokea wakati msimu ukiwa umebakiza siku chache uanze. Hatujui Yanga wataingia lini kambini lakini kinachoonekana ni kwamba Manqoba atakuwa na kazi nzito ya kuwafahamu wachezaji wake na pia kutumbukiza staili yake ya uchezaji ndani ya muda mfupi.

Yanga walichukua ubingwa msimu ulioisha lakini katika jicho la wazi hata mashabiki wa timu yao wanaamini kwamba timu yao imeshuka kiwango. Sio Yanga ile ya Miguel Gamondi iliyokuwa inashinda mabao Matano Matano kwa urahisi dhidi ya wapinzani wake.

Bahati mbaya msingi wa kikosi kile unazidi kumung’unyuka pale Jangwani. Ndio hawa akina Pacome ambao wameumia. Katika msingi ule wa mashambulizi amebakia Maxi Nzengeli pekee. Labda pia unaweza kumchomeka Mudathir Yahaya ambaye amekuwa na tabia ya kufunga.

HISI 03

Manqoba ana kazi kweli kweli kuirudisha Yanga ile. Hapa Katikati makocha wengi wameishia kufukuzwa tu. Hawakufikia kile kiwango kilichotakiwa. Akina Folz walifukuzwa, akina Pedro Concalves walipita kama upepo. Mitaani mashabiki wanaidai timu yao irudi.

Hayo yote yanatokea wakati kule kwa mtani kumeanza kwenda sawa. Watani walifika juu wakaanza kwenda chini. Wakampisha Yanga katika utawala. Na kinachoelekea sasa hivi wanataka kurudisha utawala wao. Tayari wamechukua kombe la Shirikisho ambalo walilikosa kwa miaka minne.

Manqoba anaingia katika mtihani mmoja na mabosi wake. Kuhakikisha timu haitoki katika utawala. Katika uhalisia ni kitu kigumu kuendelea kubakia katika namba moja kwa muda mrefu. Kuna wachezaji wanaondoka, wengine wanaumia, wengine wanachoka tu. Hapo ndipo unapolazimika kutengeneza timu mpya ndani ya timu ya zamani.

Hii ni kazi ngumu. Liverpool walishindwa. Walipoondoka akina Sadio Mane na Roberto Firmino huku miguu ya Virgil van Dijik ikianza kuchoka tuliona namna ambavyo waliterereka. Msimu uliopita Liverpool wamefungwa zaidi ya mechi 20. Isingekuwa hivyo katika zama za Jurgen Klopp.

HISI 04

Manqoba ana kazi ya kutengeneza timu mpya ndani ya timu ya zamani. Kitu kingine ambacho atakumbana nacho ni namna ambavyo kwa mara ya kwanza baada ya misimu minne, Yanga itakuwa inacheza mechi zake bila ya Pacome. Mchezaji kama Pacome wazungu huwa wanamuita ‘talisman’. Timu imeundwa kumzunguka yeye. Yeye ndiye ana maamuzi mengi uwanjani kwa niaba ya timu.

Bahati nzuri kwa Manqoba ni kwamba langoni ana mmoja kati ya makipa bora wanaocheza ndani ya bara la Afrika, Djigui Diarra. Bila ya kipa huyu wa Mali sidhani kama Yanga wangekuwa mabingwa msimu uliopita. Kifupi alikuwa mchezaji wao bora wa msimu. Na hii ni dalili la anguko la timu. Timu bora upumzisha kipa wao. Kama kipa ana mahangaiko mengi basi kuna udhaifu umejitokeza.

Presha itakuwa kubwa pia kwa Manqoba ni pale atakupokuwa analinganishwa na kocha mwingine kutoka Afrika Kusini. Steve Berker. Kwa mara ya kwanza katika historia yetu timu zote mbili zinafundishwa na makocha kutoka Afrika Kusini. Mechi ya kwanza tu watakutana uso kwa uso na lazima kutakuwa na presha kubwa kwa kila kocha. Watu watataka kufahamu ni nani hasa amelamba dume kutoka Afrika Kusini.

Karibu Tanzania Manqoba. Muda utamuhukumu vizuri tu. Kuna wachambuzi wamekuwa wakitofautiana kuhusu wasifu wake wa alikotoka lakini hilo sio jambo la msingi kwa sasa. Tutamuhukumu kwa kile ambacho atakwenda kukifanya Jangwani.