Mangungu ndiye Mwenyekiti mpya Simba

Murtaza Mangungu amechaguluwa kwa kishindo kuwa mwenyekiti mpya wa klabu ya Simba akimbwaga mpinzani wake, Juma Nkamia.
Mangungu amepata kura 802 kati ya 1140 zilizopigwa kwenye uchaguzi mdogo wa klabu uliofanyika leo Jumapili jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Simba, Boniface Lihamwike amesema Mangungu amepata asilimia 70.35 ya kura zilizopigwa.
"Waliopuga kura ni wanachama 1140, kura nane zimeharibika na Juma Nkamia amepata kura 330 sawa na asilimia 28.95," amesema Lihamwike.
Amesema mchakato wa uchaguzi huo ulifanyika vizuri na wagombea wote wameridhishwa na matokeo.
Nkamia alimpongeza Mangungu kwa ushindi na kueleza kwamba pamoja na wajumbe 'kumtosa' ataendelea kuwa mwanachama ndani ya klabu hiyo.
"Nimuombe tu Mangungu kusimamia ipasavyo mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji, akifanya hivyo na mchakato ukakamilika hata mimi nitaingia kununua hisa,".
Mangungu aliwashukuru wapiga kura na kutaka waliokuwa wapambe wake na wale wa Nkamia kwenye mchakato wa uchaguzi kuungana na kuwa kitu kimoja kwa maslahi ya klabu.