Mamluki waziponza Mwanza JIJI, Dodoma Shemisemita

Muktasari:
- Akifunga mashindano hayo yaliyoshirikisha halmashauri 100 kati ya 184, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda alisikitishwa na kitendo cha jiji la Mwanza na Dodoma kuondolewa kwa kukiuka taratibu yakichezesha wachezaji siyo watumishi wao.
MASHINDANO ya 39 kwa Watumishi wa Halmashauri za Serikali za Mitaa Tanzania (Shemisemita) yalihitimishwa juzi kwa timu ya soka ya Geita kuichapa Ifakara mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Nyamagana, huku Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam (Dar City) ikiibuka mshindi wa jumla ikibeba vikombe 10.
Akifunga mashindano hayo yaliyoshirikisha halmashauri 100 kati ya 184, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda alisikitishwa na kitendo cha jiji la Mwanza na Dodoma kuondolewa kwa kukiuka taratibu yakichezesha wachezaji siyo watumishi wao.
Mtanda aliyemwakilisha Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa alisema kitendo hicho ni cha kupigwa vita, huku akiwataka wakurugenzi wa halmashauri hizo kuchukua hatua dhidi ya waliohusika na udanganyifu.
“Watu wangu wa Mwanza Jiji wametia dosari kwa kuleta mamluki. Nalaani kitendo hiki ni kitu kibaya si cha kufurahia na naamini mkurugenzi wa jiji atachukua hatua kwa waliohusika. Nawapongeza Ilemela wamekuwa mfano mzuri na wenyeji wema kulinganisha na wenzenu wa jiji naamini wataiga,” alisema.
“Na zile halmashauri 84 (ambazo hazikushiriki) nitamjulisha waziri kwamba wapo wakaidi wachache hawataki kwenda sambamba na wengine, sasa yeye ni mamlaka yake anajua taratibu za kufuata. Ni vizuri tutakapokwenda Tanga halmashauri zote 184 zijipange kwenda huko.”
Mtanda aliwataka wakurugenzi kumuiga Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa wabunifu na kuanzisha ‘Goli la Mkurugenzi’ katika matamasha na michezo inayofanyika watumishi wakitakiwa kushiriki ili kujenga afya, ukakamavu na umoja.
Mwenyekiti wa Mashindano ya Shimisemita, Godfrey Lupembe, alisema michezo hiyo imekuwa na mwitikio mkubwa huku akiwaomba wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuwaruhusu watumishi kushiriki katika mashindano yajayo yatakayofanyika jijini Mwanza.
Kocha wa mabingwa soka, Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Benald Simon alisema siri kubwa ya ushindi wao ni morali kubwa ambayo wachezaji wameonyesha na wachezaji wake kufuata maelekezo ambayo aliwapa.