Mamelodi yawapiga Warundi 4-0 jijini Dar

Muktasari:
- Wawakilishi wa Burundi waliomba mechi hiyo ipigwe Chamazi kutokana na viwanja vya nchini kwao kushindwa kukidhi vigezo vya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na kujikuta akienda mapumziko ikiwa imeshafungwa mabao matatu.
MABINGWA wa soka wa Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns jioni ya leo imeanza vyema mechi za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuifumua Bumamuru ya Burundi kwa mabao 4-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamazi, jijini Dar es Salaam.
Wawakilishi wa Burundi waliomba mechi hiyo ipigwe Chamazi kutokana na viwanja vya nchini kwao kushindwa kukidhi vigezo vya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na kujikuta akienda mapumziko ikiwa imeshafungwa mabao matatu.
Bao la kwanza liliwekwa kimiani na kiungo Mbrazili wa Mamelodi, Lucas Costa Ribeiro dakika ya 12 kabla ya kuongeza jingine dakika ya 37 na wakati Bumamuru ikijiuliza ikajikuta ikipachikwa bao la tatu lililowekwa kimiani na Lesiba Nku.
Mamelodi iliwaanzisha benchi nyota wake kadhaa akiwamo mkali wa mabao raia wa Namibia, Peter Shalulile ambaye aliingizwa kwenye kipindi cha pili sambamba na Lebohang Maboe, Bongani Zungu na Khuliso Mudau ili kuchukua nafasi za Teboho Makoena, Rivaldo Coetzee, Lucas Costa na Bathusi Aubaas.
Mabadiliko hayo yaliiongezea kazi wageni hao kutoka Sauzi kwa kuandika bao la nne kupitia Shalulile dakika ya 77 na kuifanya Mamelodi kuwa na kibarua chepesi kwenye mchezo wa marudiano itakayochezwa wiki ijayo huko Sauzi ili kujihakikisha kutinga makundi ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa.
Kesho kwenye Uwanja wa huo wa Azam Complex kutapigwa mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Arta Solar ya Djibouti itakayoikaribisha Zamalek ya Misri.