Mambo ya kufanya kabla msimu wa ligi haujaanza

Muktasari:
Lakini kumekuwa na mkanganyiko wa yapi ni mazoezi sahihi katika hatua ya awali kabisa mara baada ya wachezaji kutoka katika kipindi cha mapumziko.
MAANDALIZI kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara yameanza na tayari timu zinazoshiriki ligi hiyo zimeanza programu mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kujiweka sawa.
Lakini kumekuwa na mkanganyiko wa yapi ni mazoezi sahihi katika hatua ya awali kabisa mara baada ya wachezaji kutoka katika kipindi cha mapumziko.
Hii ni baada ya kuona wachezaji wengi wanakuwa na matatizo ya kuchanika nyama za paja, magoti na vifundo vya miguu na wengine wakilalamika na kukosoa wakuu wao wa ufundi. Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na baadhi ya waalimu na wachambuzi wa soka ili kufahamu ukweli juu ya programu hizo mbalimbali zinazofanywa na timu zinazoshiriki Ligi Kuu.
Mshindo Msolla
Dk. Msolla amewahi kuwa kocha wa Taifa Stars anasema kwamba mchezaji anatakiwa kuanza na mazoezi mepesi mara anapotoka kwenye kipindi cha mapumziko vinginevyo mchezaji anaweza kupata matatizo ya misuli, goti au kifundo cha miguu.
“Kitaalamu kocha anatakiwa kuanza kumpa mchezaji wake mazoezi mepesi ili kujua afya yake ikoje, anaanza kwa dakika chache na kadiri siku zinavyosonga anaongeza muda, hiyo ni kwa kupasha na kupiga mipira pamoja na mechi zisizokuwa rasmi.
“Hapo kocha atagundua kama wachezaji wake wanatakiwa kufanyiwa nini, baadaye ndipo wapelekwe mazoezi ya gym au ufukweni, mazoezi ya sehemu hiyo nayo yana programu yake ingawa binafsi naona mazoezi ya ufukweni ni bora kuliko gym.
“Ufukweni au gym ni hatua ya pili baada ya hayo ya uwanjani, kocha asipokuwa makini anaweza kusababisha timu yake kuwa na wachezaji wengi majeruhi, kipindi cha mapumziko hawafanyi mazoezi binafsi hivyo, ukiwapeleka moja kwa moja kwenye mazoezi magumu unaweza kuwaua.
“Na kabla ya yote wanatakiwa kufanyiwa vipimo vya afya jambo ambalo kwa hapa ni tatizo ndiyo maana hivi sasa kuna wachezaji wengi wanakumbwa na matatizo ya nyama za paja, vifundo na magoti chanzo ni mazoezi kama hayo,” anasema Msolla.
Joseph Kanakamfumu
“Wachezaji wetu wa Kibongo wanapokuwa likizo ni watu wa kula bata tu, hawajishughulishi kufanya mazoezi binafsi, hivyo si vyema kuwapeleka gym au beach mara tu watokapo mapumzikoni, huko ni kuwaumiza.
“Angalau wafanye mazoezi mepesi hata siku tatu na daktari awapime afya kabla ya kuwabadilishia mazoezi hayo magumu, mazoezi ya ufukweni ni mazuri kuliko gym kwani hata enzi zetu tulikuwa tukifanya, wanapokuwa ufukweni nako kocha anatakiwa ajue si kuwakimbiza tu, wakimbie kwa kiwango ama wabebane au waogelee.
“Wanapokuwa gym kocha anatakiwa kuwa karibu sana na mtu anayewapa mazoezi hayo kwani yana hatua zake na mchezaji hapaswi kunyanyua vyuma kwani uzito wa juu na chini utakuwa tofauti,” anasema Kanakamfumu.
Tom Olaba
Kocha Olaba anasema kwamba baada ya wiki mbili mchezaji ndipo anapopaswa kupelekwa gym ama beach na hatakiwi ykufanywa yote kwa wakati mmoja, ila kikubwa ni kuanza na mazoezi mepesi.
“Mazoezi magumu yana madhara makubwa kwa afya za wachezaji hasa misuli, kitaalamu wanatakiwa kufanyiwa vipimo na kupewa mazoezi mepesi napo yafanyike polepole kwa maana ya kuanza na dakika chache na kuongeza dakika kadiri siku zinavyokwenda.
“Hata vifaa wanavyotumia huko beach hasa viatu sivyo hivyo vinavyotakiwa kutumika, hilo linaweza kusababisha matatizo kwa wachezaji. Wataalamu wanatueleza hivyo kwa sababu asilimia kubwa ya wachezaji wetu hasa Afrika Mashariki ni wavivu wanapokuwa likizo hawana muda wa kufanya mazoezi binafsi,” anasema Olaba.
Sekilojo Chambua
Yeye anasema anavyofahamu kitaalamu mchezaji hapaswi kupelekwa gym au ufukweni, kwani ni lazima mwili ushituliwe kwa mazoezi mepesi ili uwe na utayari wa kupokea kitu kizuri na akili kukaa kimchezo.
“Maandalizi ya mwanzo ni kufanya mazoezi mepesi kwani si kila mchezaji anapokuwa likizo anafanya mazoezi, hivyo lazima wapashe misuli kwa mazoezi hayo hata kwa siku chache ndipo wapelekwe gym au ufukweni.
“Vinginevyo unaweza kusababisha madhara makubwa kwa wachezaji hasa misuli kwani yale ni mazoezi magumu, kila kocha ana taratibu zake lakini kitaalamu hivyo ndivyo mchezaji anatakiwa kuanza, mazoezi ya kujenga mwili ni lazima yafanyike baada ya hayo mepesi,” anasema Chambua.
Boniface Pawasa
“Unapompa mazoezi magumu mchezaji si rahisi kugundua madhara mara moja mpaka baadaye, ndiyo maana wachezaji wengi wanaweza kuanza kwa kasi kwenye ligi lakini wakifika katikati kiwango kinashuka ni kwa sababu wanakuwa wametumia nguvu nyingi mwanzo.
“Mpira umebadilika lakini kwa kawaida mchezaji anatakiwa apewe mazoezi mepesi kwanza na afanyiwe vipimo ndipo apelekwe gym au ufukweni, wengi wanakumbwa na matatizo ya misuli au nyonga bila kujua sababu ni nini.
“Siku hizi makocha wanataka kufundisha soka la kisayansi zaidi lakini wanatakiwa watumie vizuri taaluma zao ili kulinda viwango vya wachezaji vidumu kwa muda mrefu, vinginevyo ni kuuwa viwango vyao wangali na umri mdogo,” anasema Pawasa.
Zdravko Logarusic
“Mazoezi ya awali wakati wachezaji wanatoka katika mapumziko yanatakiwa kulenga kujenga mwili. Wachezaji wanatakiwa kufanya mazoezi yatakayojenga kila kiungo kisha ya mpira yatakuja baadaye.
“Siwezi kusema kuwa tunatakiwa kufanya mazoezi ya aina moja ila kwangu naonelea kuwa wanatakiwa kufanya mchanganyiko wa mazoezi ya ufukweni na yale ya gym ili kujiweka sawa,”
Ally Mayay
Mayay ni miongoni mwa wachezaji wakongwe na wachambuzi wa soka ambao wanadai kuwa mchezaji ni lazima aanze kwa kujenga mwili hivyo mazoezi ya gym au ufukweni ndiyo yanapaswa kuwa ya kwanza.
“Mchezaji anatakiwa apimwe afya yake na kuanza mazoezi magumu baada ya hapo ndipo apewe mazoezi mepesi na mbinu za kiufundi,” anasema Mayay.