Mambo matano hatari kwa uhusiano

Haya haya tunakutana tena katika jamvi la Anti K kwa ajili ya kupeana haya na yale, lengo likiwa ni kuimarisha uhusiano wetu wa kimapenzi.
Licha ya migogoro ya mahusiano ya mapenzi kutajwa kuwa ni kitu cha kawaida na ni sehemu ya maisha, ipo haja ya kuimaliza na wapendanao kubaki salama.
Ili uhusiano wako ubaki salama epuka mambo haya matano:
Kupoteza uaminifu
Jitahidi kwa kadri uwezavyo kuepuka mambo yatakayokufanya upoteze uaminifu. Ikiwamo
Kushindwa kutimiza ahadi, kusema uwongo au kufanya usaliti wa kimapenzi.
Hayo ni mambo ambayo humuondolea mtu uaminifu kwa asilimia 100, haya huchangia kwa kiasi kikubwa kuvunjika kwa ndoa au uhusiano.
Usawa wa uongozi nyumbani
Kwa kawaida siku zote mwanaume anabaki kuwa baba wa familia, bila kujali ana upungufu gani.
Hivyo kila mmoja alitambue hilo, ingawa wakati huu wanawake wamejua haki zao na wanahitaji usawa kwa kila hali.
Badala ya mume kuwa mtawala anapaswa kuwa kiongozi akishirikiana kwa karibu na mwenza wake.
Ikitokea mmoja kati yenu ndiyo anakuwa mwamuzi wa kila jambo ndani ya nyumba ikiwamo masuala ya kifedha, malezi, marafiki mwingine atachukulia maisha hayo kama utumwa hivyo ndoa au uhusiano utakuwa kwenye hatari ya kuvunjika.
Kuuweka rehani uhusiano
Ikitokea mmoja kati yenu hawezi kufanya jambo bila kusikiliza maoni ya watu kutoka nje, bila shaka atakuwa ameliweka penzi lenu katika wakati mgumu.
Haijalishi hayo maoni yanatolewa na nani, kwa sababu kuna baadhi ya familia zimeathirika na tabia hii ya kutofanya maamuzi hadi mama atoe kauli au baba.
Tabia hii ni ya kuepuka, maana ya kuwa mke na mume ni pamoja na kutoa maamuzi sahihi kwa wakati muafaka kama familia, badala ya kuishi kwa kutegemea akili za watu wengine.
Kubaguana kati yenu
Wapo wenza wanaojiona bora kuliko mwingine, hili limekuwa gonjwa sugu.
Wenza wenye malengo ya kufika mbali na kuwa na familia imara mnapaswa kuthaminiana na kuheshimiana baina yenu.
Hata kama mmoja kati yenu ana mapungufu, jukumu lenu ni kurekebishana kwa huruma na upendo , badala ya kukemeana.
Mkiwa wawili mnakuwa wa thamani zaidi, kuliko mkitengana.
Wivu kupitiliza
Wivu ni mojawapo ya sababu kuu za kuvunjika kwa uhusiano wa kimapenzi au hata ndoa. Wivu wa kupindukia unaweza kusababisha ugomvi ambao wakati mwingine ni wa hisia tu.
Wengi waliokutanishwa kwenye mabaraza kwa kesi za wivu uliopitiliza wakiulizwa wachache wanaokuwa na ushahidi wa moja kwa moja , walio wengi ni hisia tu.
Wivu ukizidi ni chanzo cha umasikini ndani ya nyumba, kwa sababu mume mwenye wivu hatamani mkewe afanye kazi wala biashara, huku mke mwenye wivu hataki mumewe azoeane na watu hata kama ni wateja au watu anaofanya nao kazi/biashara.
Ndoa au mahusiano mengi huvunjika kwa sababu ya wivu uliopitiliza.