Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo 10 yaliyoiua Yanga Morogoro

Baada ya kazi salamu.

Muktasari:

Ushindi huo wa Mtibwa unaifanya Yanga kushindwa kupata ushindi wowote mjini hapa kwa miaka sita sasa.

MTIBWA Sugar imeendeleza ubabe wake dhidi ya Yanga mkoani Morogoro baada ya juzi Jumamosi kuwafunga mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Ushindi huo wa Mtibwa unaifanya Yanga kushindwa kupata ushindi wowote mjini hapa kwa miaka sita sasa.

Imefungwa mara mbili na kutoka sare mara tatu.

Mchezo wa Jumamosi ulitarajiwa kuleta mabadiliko baada ya vijana hao wa Jangwani kuwa na rekodi nzuri ya ushindi katika mechi zake za kirafiki na ile ya Azam wikiendi iliyopita.

Yanga hakufungwa hata mchezo mmoja katika mechi nne za kirafiki na ilifanikiwa kuifunga Azam mabao 3-0 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii.

Mwanaspoti linakuletea mambo 10 yaliyoiua Yanga Morogoro.

Kuumia kwa Oscar Joshua

Kuumia kwa beki wa kushoto Oscar Joshua kuliharibu mipango yote ya kocha Maximo katika mchezo huo. Kutokana na Yanga kukosa beki mwingine wa kushoto, Maximo alilazimika kumtoa Oscar na kumwingiza Omega Seme, ambaye ni kiungo.

Mabadiliko hayo ya kipindi cha kwanza yalibadili mfumo wa timu kwani Mnyarwanda Mbuyu Twite alilazimika kuhamia beki ya kushoto na Omega kucheza nafasi ya kiungo mkabaji aliyokuwa akicheza Twite.

Mabadiliko hayo yalionekana kuzaa matunda kwa kuimarisha beki ya kushoto lakini hali ilikuwa mbaya katikati kwani Omega si mzuri anapocheza kama kiungo mkabaji, alizoea kucheza kama kiungo mshambuliaji na ndiyo nafasi aliyocheza mwaka mzima alipokuwa kwa mkopo Prisons.

Mabadiliko hayo yalisababisha Yanga kushindwa kupiga mipira mirefu kutokea katikati kwenda kwa washambuliaji wa timu hiyo na kusababisha timu hiyo kupandisha mashambulizi yake kupitia pembeni kwa Mrisho Ngassa na Simon Msuva.

Uwanja mgumu

Ni kweli, Uwanja wa Jamhuri ni mgumu, kuanzia kwenye majukwaa hadi kwenye pichi. Yanga walishindwa kucheza mipira ya chini ya pasi fupi kama wanavyoweza kufanya wakiwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Ni uwanja mgumu kupiga pasi ya chini ikafika kwa mlengwa.

Wakati Yanga wakipambana kupata matokeo kiwanjani hapo hali ilikuwa tofauti kwa wachezaji wa Mtibwa ambao walionekana kuuzoea uwanja huo.

Aina ya wachezaji wa Yanga pia si watu wa kupambana, ni walaini kucheza kwenye viwanja vigumu hivyo kupata matokeo mazuri lilionekana kuwa jambo gumu sana.

Penalti ya Jaja

Baada ya kwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao 1-0, Yanga walirejea kipindi cha pili wakiwa na kasi kubwa. Mabadiliko ya kumtoa Hamis Kiiza na kumwingiza Msuva yalionekana kuongeza kasi kwa vijana hao wa Maximo.

Dakika ya 46 ya mchezo Yanga walipata penalti, ambayo straika wao Mbrazili Genison Santos ‘Jaja’ alishindwa kuikwamisha wavuni.

Penalti hiyo ilikuwa ndiyo nguzo ya Yanga kubadili matokeo lakini baada ya Jaja kushindwa kuifunga mambo yalionekana kuwa magumu kwa Yanga kwani wachezaji wa Mtibwa walikuwa makini zaidi na kupunguza makosa yao.

Kipa wa Mtibwa

Kipa wa Mtibwa, Said Mohamed ndiye shujaa wa mchezo huo wa juzi Jumamosi. Kipa huyo wa zamani wa Yanga na Majimaji ya Songea alionekana kuwa kikwazo kikubwa kwa klabu yake hiyo ya zamani kupata matokeo.

Mohamed alionekana kuwa makini hususani kwa mipira mirefu iliyokuwa ikienda kwenye kichwa cha Jaja.

Mbali na kuokoa mkwaju wa penalti, aliondoa hatari mbili zilizokuwa zizae mabao kutoka kwa Jaja na pia kufanikiwa kucheza kichwa hatari tena kutoka kwa beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Hakika Yanga watamkumbuka kipa huyo kama kipa wao mwingine wa zamani Shaban Kado, ambaye alikuwa kikwazo kikubwa kwa timu hiyo ilipochapwa mabao 3-0 na Mtibwa Uwanja wa Manungu, Morogoro mwaka 2012.

Utulivu wa Nditi

Kiungo mkongwe wa Mtibwa, Shaban Nditi alipewa kadi nyekundu wakati timu hizo zilipokutana Machi mwaka huu. Hakuwa na utulivu kwenye mechi hiyo. Hali ilikuwa tofauti juzi Jumamosi. Nditi alicheza kwa utulivu wa hali ya juu.

Alifanikiwa kuwapunguza kasi Haruna Niyonzima na Hassan Dilunga. Alikuwa makini pia kuwasaidia mabeki wake Salim Mbonde na Andrew Vicent. Hakika kiungo huyu alikuwa chachu ya ushindi wa Mtibwa.

Kujisahau kwa mabeki wa Yanga

Mabao yote mawili waliyofungwa Yanga yalitokana na uzembe wa mabeki wa timu hiyo. Bao la kwanza alilofunga Mgosi lilionekana kuwa jepesi baada ya mabeki Kelvin Yondani na Cannavaro kupoteza umakini.

Bao la pili lililofungwa na Ame Ally lilioneka pia kuwa jepesi baada ya beki ya kushoto ya Yanga kupotea huku Cannavaro na Yondani waliokuwa wamepanda kusaidia mashambulizi kwa timu yao wakidhani kuwa Ally alikuwa ameotea kitu ambacho hakikuwa sahihi.

Kumtegemea Jaja

Ni ukweli usiopingika kwamba Maximo anamwamini Jaja asilimia 100. Anaamini kuwa ni mtu ambaye anaweza kubadili matokeo muda wowote wa mchezo. Hilo ni tatizo.

Timu inatakiwa kuwa na mpango wa pili endapo wa kwanza ukionekana kushindwa kuleta matunda. Baada ya mabeki na kipa wa Mtibwa kumkamia Jaja sikuona haja ya Maximo kuendela kumtegemea straika huyo wakati ana Hussein Javu nje ambaye ameuzoea Uwanja wa Jamhuri kama sebuleni kwake.

Aina ya wachezaji kama Javu wanaweza kukupatia matokeo kwenye viwanja kama vya Jamhuri hususani timu inapoonekana kumkamia zaidi straika wako tegemeo.

Maximo alijaribu kumchezesha Saidi Bahanuzi kipindi cha pili lakini bado haikuwa tija sana kwani Bahanuzi wa sasa si yule wa Kagame.

Maxime kumfahamu Maximo

Taifa Stars iliondoshwa na Msumbiji kwenye hatua za awali za kuwania kufuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwakani nchini Morocco.

Msumbiji iliyoifunga Stars inafundishwa na kocha Joao Chissano ambaye alikuwa kocha msaidizi wakati kocha wa sasa wa Stars, Mart Nooij akiifundisha Msumbiji. Chissano alikiri kuwa kumfahamu Nooij na mbinu zake kulimrahisishia kazi ya kuifunga Stars.

Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Yanga. Maxime alikuwa nahodha wa Stars wakati ikifundishwa na Maximo. Alipata fursa nyingi za kufahamu mbinu zinazotumiwa na kocha huyo hivyo kwake ilikuwa ni kazi rahisi kummaliza Mbrazili huyo kama alivyofanya Chissano kwa Nooij.

Kumtoa Twite

Mtibwa ilipata bao la pili baada ya Maximo kumtoa Twite na kumwingiza Bahanuzi. Twite alikuwa akicheza beki ya kushoto wakati Bahanuzi aliingia kama straika. Mabadiliko hayo yalisababisha Omega kurudi kucheza kama beki wa kushoto kuziba nafasi ya Twite.

Huku ndiko walikopita Mtibwa na kupata bao la pili ambalo pia likichagizwa na mabeki wa kati ambao walidhani mfungaji wa bao hilo alikuwa ameotea na kushindwa kurudi kwenye nafasi kwa wakati huo ili kukaba.

Omega si mzuri katika kukaba hususani kumchezesha kama beki hivyo ni dhahiri kuwa presha ya Maximo ya kutaka bao la kusawazisha iliyosababisha kumtoa beki na kumwingiza straika wa pili yaliigharimu klabu hiyo.

Ushindi dhidi ya Azam

Baada ya kuifanyia Azam mauaji kwa kipigo cha mabao 3-0 kwenye mechi ya ngao ya Jamii, Yanga waliamini kuwa hakuna timu nyingine inayoweza kuwazuia.

Ni kweli Yanga walipata ushindi katika mchezo ule lakini hawakucheza katika kiwango cha juu sana. Unapokuwa na timu ambayo haikucheza katika kiwango chake na ukapata matokeo ni dhahiri kuwa huwezi kutambua makosa yako makubwa na kuyafanyia kazi. Hiki nacho kilichangia kuiangusha Yanga Morogoro.