Prime
Mfungaji bora Ligi Kuu 2025/26 anukia Kariakoo
HAIJAWAHI kuwa ngumu kwa Simba na Yanga kugonga hodi Singida Black Stars kwa ajili ya kusaka wachezaji wa kuimarisha vikosi vyao
Singida Black Stars yenye maskani yake Mtipa imekuwa kama kiwanda cha vipaji na miamba ya soka la Tanzania, Simba na Yanga ni moja ya wanufaika wa hilo na safari hii macho yote yanaelekezwa kwa mshambuliaji wa Burundi, Mossi Nduwumwe ambaye ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu ya NBC.
Mossi alijiunga na Singida Black Stars katika dirisha dogo la Januari akitokea Flambeau du Centre ya Burundi, lakini ndani ya nusu msimu tu amegeuka kuwa mmoja wa wachezaji waliotikisa zaidi Ligi Kuu ya NBC.
Akiwa amecheza mechi 21 pekee, alifunga mabao 17 na kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa msimu wa 2025/26, akiwapiku nyota waliokuwa wakipewa nafasi kubwa kama Feisal Salum wa Azam na Allan Okello wa Yanga.
Kinachoongeza uzito wa jina lake ni kwamba tayari historia inaonyesha Singida imekuwa njia ya moja kwa moja kuelekea Kariakoo.
Msimu uliopita katika vipindi viwili tofauti vya usajili, Simba iliwasajili Jonathan Sowah (mwanzoni mwa msimu), Clatous Chama na Nickson Kibabage (katikati ya msimu) kutoka Singida Black Stars.
Chama na Kibabage walikuwa sehemu muhimu ya kikosi kilichomaliza nafasi ya pili kwenye ligi wakiwa na pointi 70 nyuma kwa pointi mbili na Yanga ambao walitwaa ubingwa watano mfululizo na kufika fainali ya Kombe la CRDB, huku Sowah akikwama kutokana na changamoto za kinidhamu zilizomweka nje ya kikosi tangu Februari mwaka huu.
Yanga nayo haikubaki nyuma. Ndani ya msimu uliopita iliwapata Hussein Masalanga, Mohammed Damaro na Israel Patrick kutoka Singida Black Stars, huku kabla ya hapo ikiwa tayari ilinufaika na wachezaji kama Feisal Salum, Nickson Kibabage na Frank Assinki waliopita klabu hiyo.
Ni historia hiyo inayofanya wengi kuamini Mossi anaweza kuwa mchezaji anayefuata kuvaa jezi ya moja ya vigogo hao wa Kariakoo.
TAKWIMU ZAKE
Mossi hakutwaa tu kiatu cha ufungaji, bali alionyesha uwezo mkubwa wa kumalizia nafasi.
Ndani ya dakika 1,719 alizocheza katika mechi 21, alifunga mabao 17, ikiwa ni wastani wa bao moja kila baada ya dakika 101.
Katika msimu huo alifunga hat-trick mbili dhidi ya Dodoma Jiji na Fountain Gate huku pia akifunga mabao mawili dhidi ya Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar na Pamba. Takwimu hizo ndizo zilizompeleka kileleni mwa orodha ya wafungaji.
Hata hivyo, takwimu za mchango wa mabao zinaonyesha kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, ndiye aliyekuwa mchezaji hatari zaidi kwa ujumla msimu huu.
Feisal alifunga mabao 15 na kutoa asisti tisa ndani ya mechi 27, hivyo kuhusika moja kwa moja katika mabao 24 ya Azam. Akiwa ametumia dakika 1,775 uwanjani, alikuwa anahusika na bao moja kila baada ya dakika 74, rekodi bora zaidi katika ligi.
Kwa upande wa Yanga, Allan Okello naye alikuwa na msimu mzuri baada ya kufunga mabao 14 na kutoa asisti nane. Mchango wake wa mabao 22 ulimfanya ahusike na bao moja kila baada ya dakika 81.
Ingawa Feisal ameongoza kwenye mchango wa mabao, Mossi ndiye aliyethibitisha ubora wake wa kufunga kwa kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa ligi.
ANAFAA WAPI KARIAKOO?
Kwa Simba, ujio wa Mossi unaweza kuwa suluhisho la moja kwa moja kwenye safu ya ushambuliaji. Baada ya Jonathan Sowah kusimamishwa kutokana na utovu wa nidhamu, kocha Steve Barker mara kadhaa alilazimika kumtumia Elie Mpanzu kama mshambuliaji wa kati, licha ya kutokuwa nafasi yake ya asili.
Mossi ana uwezo wa kucheza kama mshambuliaji wa kati, pembeni au namba 10, jambo linaloweza kuipa Simba chaguo zaidi kwenye eneo ambalo lilikuwa na upungufu msimu uliopita.
Kwa upande wa Yanga, hoja ni tofauti kidogo. Mabingwa hao wameendelea kutengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini wakati mwingine wameonekana kukosa makali katika eneo la mwisho.
Uwepo wa mshambuliaji mwenye uwezo wa kutumia nafasi chache kama Mossi unaweza kuongeza makali zaidi kwenye safu yao ya ushambuliaji.
SAIDO, TAMBWE
Mafanikio ya Mossi yanaendeleza rekodi ya washambuliaji kutoka Burundi waliowahi kutwaa kiatu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu Bara.
Amissi Tambwe aliwahi kutwaa kiatu cha ufungaji akiwa Simba kwa mabao 19 msimu wa 2013/14 kabla ya kufanya hivyo tena akiwa Yanga kwa mabao 21 msimu wa 2015/16. Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ naye alitwaa tuzo hiyo msimu wa 2022/23 akiwa Simba baada ya kufunga mabao 17, idadi ambayo sasa imefikiwa pia na Mossi akiwa Singida Black Stars.
MSIKIE ANACHOSEMA
Akizungumzia mafanikio aliyoyapata, Mossi alisema: “Kwanza namshukuru Mungu kwa kunipa afya na nguvu za kucheza. Nilipofika Singida Black Stars sikuwa na presha ya kutwaa kiatu cha ufungaji, nilichokuwa nataka ni kuisaidia timu. Kadri mechi zilivyokuwa zinaendelea ndipo nilianza kupata kujiamini, nikaanza kufunga na mwisho wa siku nikamaliza msimu nikiwa mfungaji bora. Ni jambo ambalo linanipa furaha kubwa.
“Mafanikio haya sio yangu peke yangu. Nawashukuru wenzangu, benchi la ufundi na viongozi wa Singida Black Stars kwa kuniamini tangu siku ya kwanza. Bila wao isingewezekana kufunga mabao haya yote, kwa sababu mpira ni mchezo wa timu. Kila bao nililofunga limetokana na kazi ya pamoja, hivyo tuzo hii ni ya kila mmoja ndani ya klabu.”