Makocha wanane nchini 'waula' Afrika

Makocha nane kati ya 26 nchini walioshiriki mafunzo ya kimataifa ya netiboli wametunukiwa vyeti vya Afrika daraja la kwanza.
Makocha hao ni Mussa Samson na Hafidh Tindwa wa Dar es Salaam, Benson George na Frola Odilo wa Dodoma, Everyne Ngonyani, Frola Patrick na Stephen Mzee wa Pwani pamoja na Aneth Kapinga wa Mtwara walitunukiwa vyeti vya Afrika daraja la kwanza ambavyo vinawapa fursa ya kufundisha timu za taifa katika nchi yoyote Afrika.
Makocha wengine wanane walitunukiwa vyeti vya daraja la dhahabu ambavyo vinawapa fursa ya kufundisha klabu mbalimbali nchini na wengine 10 wakitunukiwa vyeti vya daraja la fedha ambavyo ni kwa ajili ya kufundisha timu za shule kwenye mashindano ya Umisseta na Umitashumta.
Upande wa waamuzi, 10 walitunukiwa vyeti vya dhahabu na wengine waliosalia wametunukiwa vyeti vya fedha baada ya mafunzo yaliyokwenda sanjari na mtihani wa kuandika na wa vitendo ulioongozwa na wakufunzi, Mary Waya na Dk Rebecca Dulanya kutoka Malawi.
Mafunzo hayo ya siku nane yameyofanyika kwenye kituo cha michezo cha Filbert Bayi yakiandaliwa na Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) na kupewa sapoti na Taasisi ya Filbert Bayi iliyopo Kibaha, Mkuza mkoani Pwani.
Akifunga mafunzo hayo, mkuu wa idara ya Rasilimali watu kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Gerald Mwalekwa amewataka makocha na waamuzi kuitumia elimu waliyoipata kwa maslahi ya Chaneta na timu ya taifa.
"Chaneta wamekuwa na mwanzo mzuri kwenye hili, kama makocha na waamuzi wote 50 watayafanyia kazi yale wakiyofundishwa, hakuna shaka Tanzania itapiga hatua kimataifa," amesema.
Kiongozi huyo pia alimshukuru Filbert Bayi mwenyekiti wa Taasisi za FBF kwa sapoti yake kwenye mafunzo hayo licha ya kwamba hakuwa kwenye familia ya netiboli.
"Mzee wetu ni mwanariadha, lakini anatumia rasilimali alizonazo kusapoti na michezo mingine, kwa gharama ambazo mmenieleza amewatoza kwa siku zote mlizoishi na kwenye kituo hiki mkijifunza, na mazingira ya kituo niliyoyashuhudia, sehemu nyingine ingekuwa ni kubwa sana, lakini yeye ameamua kuwasaidia kwa kuwatoza gharama kidogo sana za uendeshaji, mzee wetu huyu azidi kubarikiwa na kuendelea kuwepo kutoa sapoti hii," amesema.
Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Dk Devotha Marwa amesema mipango ya netiboli kurudi kwenye levo ya kimataifa imeanza kuonyesha matunda.
Amesema hiyo ni kozi ya kwanza ya kimataifa ya netiboli kufanyika nchini na kuwa na muitikio mkubwa na kueleza kwamba wanakwenda kuleta mapinduzi ya mchezo huo ambao uliwahi kuiweka Tanzania kwenye wnafasi ya 14 duniani kabla ya kuporomoka mwishoni mwa mwaka 2013 na sasa ni wa 40.
"Mafunzo haya ni mwanzo wa kuelekea kwenye mafanikio, lakini pia Chaneta hatuna budi kumshukuru Mzee Bayi kwa sapoti yake, baada ya kumfuata na kumueleza mpango huu aliamua kutupa malazi, chakula, viwanja na ukumbi wa mafunzo kwa kuchangia gharama kidogo sana za uendeshaji tukijifunza katika mazingira bora na tulivu yenye mahitaji bora kwa mwanamichezo," amesema.
Mary Waya kocha wa zamani wa timu ya Taifa na mkufunzi wa kimataifa kutoka Malawi ameitaka Chaneta kuwatumia waamuzi na makocha wote 50 waliohitimu mafunzo hayo kwa majukumu mbalimbali ya mchezo wa netiboli nchini.
"Hawa wanane walioshinda Afrika ndio miongoni mwao wawe makocha wa timu ya taifa na wengine wowote hapa Tanzania, lakini pia wanaweza kufundisha timu yoyote ya taifa Afrika," amesema Waya.