Makipa wote Simba wako vizuri

KOCHA wa makipa wa Simba, Mohammed Muharami ‘Shilton’ amesema kuwa viwango vya makipa wake watatu; Aishi Manula, Said Mohammed ‘Nduda’ na Emmanuel Mseja, vinampa wakati mgumu wa kuamua nani awe kipa namba moja wa timu hiyo.
Muharami ambaye amepewa jukumu la kuwanoa makipa wa timu hiyo akichukua nafasi iliyoachwa na Mkenya Iddi Salim aliyepigwa chini, ameliambia gazeti hili kuwa bado Simba haina kipa namba moja na atajulikana baada ya ligi kuanza.
“Hizi ni mechi za kirafiki tu ambazo lengo ni kuangalia uwezo wa kila mchezaji na ndio maana unaona kuna mechi anadaka Aishi na nyingine anadaka Nduda. Mseja bado hajaanza kupata nafasi, lakini sio kwamba kiwango chake kipo chini bali ni uamuzi tu wa kutaka kuwapima kwanza hawa wawili,” alisema Muharami.
“Na katika mechi na mazoezi ambayo makipa wote wamefanya, wameonyesha kiwango cha juu hivyo tungoje ligi ianze kisha zichezwe mechi kadhaa, baada ya hapo kipa namba moja atajulikana ila kwa sasa ni mapema mno kumtangaza.”
Muharami aliongeza kuwa uwepo wa makipa hao watatu, unawapa uhakika wa kuwa na safu imara ya ulinzi na kazi ngumu iliyopo sasa ni kuhakikisha viwango vyao vinaimarika maradufu badala ya kuporomoka.
“Ni jambo la kufurahisha kuona timu inakuwa na makipa watatu wazoefu na wenye kiwango cha juu kwani hata ikitokea mmoja anakosekana, timu inakuwa na uhakika wa kumtumia mwingine na akafanya vizuri,” aliongeza.
Makipa hao wote wamesajiliwa na Simba katika dirisha la usajili lililofungwa wiki chache zilizopita ambapo Manula ametokea Azam FC, Mohammed, akitokea Mtibwa Sugar huku Mseja akisajiliwa kutoka Mbao FC.
Manula msimu uliopita aliweka rekodi ya kutoruhusu bao katika mechi 15 za ligi kuu wakati Nduda alitwaa tuzo ya kipa bora wa mashindano ya nchi za kusini mwa Afrika (Cosafa) huku Mseja akinaswa baada ya kuonyesha kiwango bora katika mechi za mzunguko wa kwanza za Mbao FC msimu uliopita.