Lwandamina ataja mashine saba
Muktasari:
Akizungumza na Mwanaspoti saa chache kabla ya kuondoka Ijumaa usiku, Lwandamina alisema anataka marekebisho makubwa katika kikosi chake ambapo kazi kubwa ni kujaza mapungufu ya nafasi katika kikosi chake.
KOCHA wa Yanga, Mzambia George Lwandamina, ameikabidhi kamati mpya ya usajili wa Yanga mashine mpya saba na akawaambia atatua Julai Mosi kuanza kazi.
Akizungumza na Mwanaspoti saa chache kabla ya kuondoka Ijumaa usiku, Lwandamina alisema anataka marekebisho makubwa katika kikosi chake ambapo kazi kubwa ni kujaza mapungufu ya nafasi katika kikosi chake.
KIPA WA MAANA
Amewaambia viongozi wamtafutie kipa wa maana wa kushindana na Deo Munishi ‘Dida’ na Benno Kakolanya. Na Mwanaspoti linajua kwamba viongozi wa Yanga wamempigia simu kipa wa African Lyon, Mcameroon Rostand Youthe.
“Nahitaji kipa mzuri mwenye uwezo mkubwa, lakini mbali na sifa hiyo, awe ni mtu mwenye ushindani ikiwezekana awe na uwezo kuliko atakaowakuta hapa, siwezi kusema nani anaachwa hayo ni mambo ya ndani yako katika ripoti ambayo ipo kwa uongozi,” alisema Lwandamina.
Ingawa hakutaka kufafanua kwa undani Mwanaspoti linafahamu kwamba mkongwe Ally Mustapha ‘Barthez’ anaachwa.
BEKI WA KUSHOTO
Ametaka kutafutiwa beki wa kukaba na kupandisha mashambulizi ya maana atakayekuja kusaidiana na Haji Mwinyi ambaye amebaini hakupatiwa ushindani wa kutosha na mkongwe Oscar Joshua.
“Nahitaji beki wa kushoto mzuri mwenye uwezo mkubwa wa kukaba kwa akili ya utulivu, lakini pia anayejua kupandisha mashambulizi, tulimtumia Mwinyi lakini hakupatiwa ushindani wa kutosha kuna wakati alibweteka timu ikaanguka.”
BEKI WA KATI KISIKI
“Kuhusu beki wa kati, ningependa kupatiwa beki kati mzuri mwenye uwezo wa kutumia mguu wa kushoto au atumie yote, ukiangalia mabao mengi ambayo Yanga imefungwa wakati nipo hapa na hata kipindi ambacho sipo, mengi yametokea upande wa kushoto,” alifafanua kocha huyo.
“Mfano ukiwa na beki wa kushoto Mwinyi (Haji) ikatokea akafanya makosa ya kupitwa hakuna mtu mwenye uwezo wa kutumia mguu wa kushoto kumsaidia kusahihisha makosa hayo, hapo ndipo ugumu unapokuja, mabeki wote wa kati wana uwezo mkubwa wa kutumia mguu wa kulia, ni hatari.”
KIUNGO MKABAJI/MCHEZESHAJI
“Ningependa kuwa na kiungo mpya mkabaji, nataka mtu mwenye uwezo mkubwa wa kukaba kwa nguvu awe na uwezo wa kupokonya mipira kwa nguvu akianzia miguuni, lakini pia kukabiliana na mipira ya juu na hata kuanzisha mashambulizi,” aliongeza kusema.
“Hii ni nafasi ambayo imetuangusha sana msimu huu kwa kukosa mtu ambaye tunamhitaji, hatukuwa na mtu mwafaka ambaye angeweza kuanza kukaba kwa nguvu kwanza yeye kabla ya mashambulizi kufika kwa walinzi wa kati, hakuna beki imara inayokosa kiungo mzuri mkabaji.
“Ukiacha nafasi hiyo pia ningependa kuona kiungo mchezeshaji hodari mwenye sifa kama hizo, lakini pia awe na uwezo wa kuchezesha vyema timu, lakini pia awe na uwezo wa kusaidia majukumu ya ukabaji vyema.”
MSAIDIZI WA MSUVA
“Tunahitaji pia msaidizi wa Simon (Msuva), binafsi nimefurahishwa na utendaji kazi wa huyu kijana, amekuwa ni chachu kubwa ya ushindi, lakini hebu jiulize anapokosekana kipi kinakosekana katika timu? Pia ningependa kupata mtu kama huyu, kuna watu tunao lakini wameshindwa kushindana na Simon katika kuwania namba hili tukiliacha linaweza kumfanya Msuva akapungua kiwango.”
MSHAMBULIAJI
WA KATI
“Tunahitaji kupata washambuliaji wawili wenye uwezo mkubwa wa kufunga, kuna watu wametuangusha katika nafasi hii, hebu kumbuka kuna lile bao ambalo Simon (Msuva) alilifunga kwa kichwa wakati tunacheza dhidi ya Toto hapa nyumbani mpaka akachanika, lilikuwa ni bao la juhudi za dhati za kujitolea.
“Ukilikumbuka bao lile hebu angalia nani anaweza kufunga bao kama lile la kujitolea kwa ajili ya timu? Tunahitaji watu wa namna hii katika nafasi hiyo, nahitaji kuona kuna washambuliaji ambao watatanguliza maslahi ya timu mbele kuliko mahitaji yao watu ambao msimu huu kuna watu walituangusha.”
Aidha Lwandamina katika kutafutwa kwa wachezaji hao ametaka kamati husika kuhakikisha wanapatikana wachezaji wenye uchu wa mafanikio kwa kutafuta ushindani na sio kutaka fedha za Yanga.
CHANGAMOTO
Habari za ndani ya Yanga zinasema kwamba kamati hiyo iko kwenye wakati mgumu kutokana na ukata kwani klabu haina akiba ya kutosha, ingawa wanapambana kumshawishi Mwenyekiti aliyejiuzulu, Yusuf Manji kurudi ili mambo yakae sawa.
Habari zinasema kwamba kamati hiyo imezungumza na wachezaji takribani kumi lakini bado haijawasainisha kwa vile wanataka fedha taslimu ambazo ni mtihani Yanga.
Imeelezwa kuwa matajiri wengine wa Yanga wanaogopa kuweka fungu kwani hawaelewi hali halisi ilivyo kwa Manji ambaye amepiga kimya akiendelea na maisha yake.
Yanga inaamini Manji anatikisa kibetiri, lakini ukimya wake na sifa za vigogo wa usajili wa Simba ndizo zinazowachanganya zaidi.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Yanga, Simba wenyewwe wameshaanza kucheka kwa kufanya usajili wa mastaa wakianza na John Bocco waliyemchomoa Azam.
YANGA YAPETA
Katika hatua nyingine, Yanga imefanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya Kombe la SportPesa baada ya kuifunga Tusker ya Kenya kwa penalti 4-2.
Yanga iliingia katika mchezo huo jana Jumatatu na sura nyingi mpya, lakini iliweza kuizuia Tusker ambao ni mabingwa wa Kenya wasipate bao lolote na mechi hiyo kumalizika kwa sare tasa.
Tusker walikosa penalti mbili hivyo kuipa ujiko Yanga ambayo sasa itakutana na AFC Leopards iliyoitoa Singida United pia kwa penalti 5-4 mapema jana kwenye Uwanja wa Uhuru.
Katika mchezo wa Yanga, iliingia na wachezaji wapya Mohammed Ally, Maka Edward, Mbaraka Jumanne, Samuel Greyson, Bakari Athuman, Said Mussa na Emmanuel Kichiba.
Nyota hao wengi ambao wanatokea timu ya vijana huenda wakapata usajili katika timu ya wakubwa kama wataendeleza viwango walivyoonyesha dhidi ya Tusker.
Chipukizi Maka ndiye aliyekuwa katika ubora wa juu zaidi ambapo alipiga pia mkwaju wa penalti.
Kichiba aliyetokea Mbao FC huenda akapatiwa usajili kwa jinsi alivyocheza.
Leo Jumanne, Simba itacheza na Nakuru All Stars ya Kenya kabla ya Gor Mahia kuivaa Jang’ombe Boys.