Lunyamila kumaliza ukame wa mabao FC Juarez

Muktasari:
- Kabla ya Mazaltan msimu 2023/24 alikuwa akiitumikia Eastern Flames ya Saudi Arabia ambayo ilimaliza nafasi ya saba kati ya timu nane zinazoshiriki Ligi ya Wanawake nchini humo.
USAJILI wa nyota mpya Mtanzania, Enekia Lunyamila aliyetua FC Juarez huenda ukamaliza tatizo la ufungaji mabao katika klabu hiyo kutokana na rekodi zake nzuri alikotoka.
Mshambuliaji huyo wa timu ya Taifa ya wanawake ya Twiga Stars alisajiliwa na miamba hiyo ya Mexico wiki iliyopita akitokea Mazaltan ya nchi hiyo akijiunga na Watanzania wengine Opah Clement aliyetua msimu uliopita na beki Julietha Singano aliyeitumikia timu hiyo kwa takribani misimu mitatu.
Akiwa na Mazaltan Lunyamila alimaliza msimu akiwa na mabao sita kwenye ligi hiyo yaliyoisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya 15 kati ya 18 na nyota huyo wa timu ya taifa 'Twiga Stars' aliitumikia msimu mmoja tangu alipotambulishwa Julai mwaka jana kwa mkataba wa miaka miwili.
FC Juarez msimu uliopita katika mechi 17 za Ligi Kuu ilifunga mabao 21 ikiwa miongoni mwa timu zilizotikisa nyavu za wapinzani mara chache na ujio wa Mtanzania huyo akishirikiana na Opah aliyecheza mechi sita bila ya kufunga bao msimu ujao huenda ukaongeza kitu.
Hata kwenye vinara wa wafungaji ni kiungo Mghana, Grace Asantewaa ndiye aliyekuwa anaongoza kwa ufungaji akiweka kambani mabao saba mbele ya kinara Veronica Corral wa Pachuca FC aliyenyakua tuzo ya kiatu akifunga mabao 21.
Kabla ya Mazaltan msimu 2023/24 alikuwa akiitumikia Eastern Flames ya Saudi Arabia ambayo ilimaliza nafasi ya saba kati ya timu nane zinazoshiriki Ligi ya Wanawake nchini humo.
Licha ya chama lake kumaliza nafasi mbaya kwenye ligi lakini nyota huyo aliisaidia Flames kubaki ligi kuu akifunga mabao saba.