Ronaldo aendeleza moto, Ureno ikiweka rekodi mpya

Muktasari:
- Ureno imeweka rekodi ya kuwa taifa la kwanza kushinda taji la UEFA Nations League mara mbili mfululizo tangu kuanzishwa kwake.
MUNICH, UJERUMANI: Timu ya Taifa ya Ureno imeweka historia mpya katika soka la Ulaya baada ya kutwaa ubingwa wa UEFA Nations League kwa mara ya pili, ikiwa ndiyo timu pekee kufanikisha hivyo tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo.
Ureno imebeba taji hilo usiku wa Juni 8, 2025, baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 5-3 dhidi ya Hispania, kufuatia sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 120 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Munich, Ujerumani.
Katika mchezo huo wa fainali uliokuwa na ushindani mkali, Hispania walikuwa wa kwanza kupata bao la mapema kabla ya Ureno kurejea kwa kishindo.
Bao la kusawazisha lilifungwa na mshambuliaji nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo, katika dakika ya 61, akiweka timu yake mguu sawa na kusababisha mchezo huo kuingia muda wa nyongeza.
Baada ya dakika 30 za muda wa nyongeza kumalizika bila mshindi kupatikana, timu hizo ziliingia kwenye mikwaju ya penalti ambapo Ureno ilifunga penalti zote tano, huku Hispania ikikosa mkwaju mmoja, na kuipa Ureno ushindi wa 5-3.

Ushindi huo unaiweka Ureno kileleni mwa historia ya UEFA Nations League, ikiwa timu ya kwanza kutwaa taji hilo mara mbili tangu mashindano hayo yaanze mwaka 2018.
Ureno ilitwaa taji hilo kwa mara ya kwanza mwaka 2019 baada ya kuifunga Uholanzi kwa bao 1-0 kwenye fainali iliyopigwa Estádio do Dragão, nchini kwao.
Mabingwa hao wameongeza taji la tatu la kimataifa kwenye kabati lao, ikiwa ni pamoja na ubingwa wa EURO 2016.
Kwa upande wa Cristiano Ronaldo (40), mchezo huo uliendelea kudhihirisha thamani na mchango wake mkubwa kwa timu ya taifa. Bao lake dhidi ya Hispania lilikuwa la 938 katika maisha yake ya soka, na kuendeleza rekodi yake ya kuwa mfungaji bora wa muda wote duniani.
Ushindi huo pia unamfanya Ronaldo kuwa na mataji matatu ya kimataifa akiwa na Ureno – UEFA EURO 2016 na UEFA Nations League mara mbili – hatua inayothibitisha mchango wake mkubwa kwa mafanikio ya taifa hilo la pwani ya Ulaya.