LIVE: Mashabiki wafurika uzinduzi wa jezi mpya Simba, usalama waingilia kati

Mashabiki wafurika uzinduzi wa jezi mpya Simba

MASHABIKI wa Simba, kutoka sehemu mbalimbali wamejitokeza kwa wingi Sinza madukani, kwenye duka la Vunjabei ikiwa ni siku moja kabla ya kilele cha tamasha lao, Agosti 8.

Hakuna tena kusubiri kwa mashabiki wa Simba kwani ile siku yao maalumu ndio hiyo inawadia huku wakiwa na shauku ya kuona utambulisho wa majembe yao kwa ajili ya msimu ujao wa 2022/23.

Licha ya kuchelewa kutambulishwa kwa jezi hizo, mashabiki wa timu hiyo, wanaonekana kuwa na mwitikio mkubwa kulingana na umati uliojitikeza.

Pascal John ambaye ni mmoja wa mashabiki lialia aliyesimama kwenye foleni kwa dakika 45 baada ya uzinduzi, alisema huu ndio uzi sasa.

"Haiwezekani jezi iwe na nyumba nyumba kwani hii ni atlasi ya kucholea ramani, poleni sana Utopolo, huu ndio uzi sasa wa mabingwa na msimu huu mtatueleza," alisema.

Umati mkubwa wa mashabiki wa Simba waliopo hapa Sinza ni mkubwa kiasi cha watoa huduma wa duka la Vunjabei kuonekana kuzidiwa.

Wenye usafiri wanaonekana kukumbana na kadhia ya foleni hapa Sinza Madukani kutokana shughuli ya ununuaji jezi, imebidi watu wa usalama kuwa hapa ili zoezi liwe na amani.