Lile pati la Mbeya City ndo leo

Muktasari:
- Shangwe hilo limepangwa kufanyika kwenye Ukumbi wa City Pub Kiotani ambapo wanachama, mashabiki na wapenzi wa Mbeya City watajumuika pamoja kujipongeza kwa kazi kubwa ya kuirejesha timu hiyo katika Ligi Kuu ikiwa ni misimu miwili tangu iliposhuka 2022-2023.
MASHABIKI wa Mbeya City Jumamosi hii watajumuika pamoja kwenye pati ya kuipongeza timu hiyo kupanda Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao, huku ikipambwa na burudani mbalimbali ikiwamo wasanii wakongwe wa muziki wa kizazi kipya.
Shangwe hilo limepangwa kufanyika kwenye Ukumbi wa City Pub Kiotani ambapo wanachama, mashabiki na wapenzi wa Mbeya City watajumuika pamoja kujipongeza kwa kazi kubwa ya kuirejesha timu hiyo katika Ligi Kuu ikiwa ni misimu miwili tangu iliposhuka 2022-2023.
Mbeya City imemaliza Ligi ya Championship ikiwa nafasi ya pili na pointi 68, baada ya kushinda mechi 20, sare nane na kupoteza mbili, nyuma ya Mtibwa Sugar iliyoibuka bingwa, kufuatia kukusanya pointi 71.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Mbeya City, Gwamaka Mwankota alisema shughuli hiyo itapambwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wa mkoani hapo na nje ya Jiji la Mbeya ambao wamekubali mualiko wa kujumuika na wana Mbeya City.
“Tutakuwa na mambo mengi ila kubwa zaidi ni wasanii kutoa burudani kwa wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wetu kwa kufanikisha azma yetu ya kurejea Ligi Kuu, niwaombe wadau wa Mbeya na mikoa ya karibu kujitokeza kwa wingi,” alisema.
Mwankota alisema awali walipanga kucheza mechi ya kirafiki japo baada ya kazi kubwa iliyofanywa na wachezaji wameona ni vyema wawape mapumziko, hivyo siku hiyo itakuwa ya kupata burudani kutoka kwa wasanii.
“Kiingilio tumeweka rafiki, tukiamini kila mmoja wetu ataweza kukimudu na kuhudhuria tukio hilo kubwa na la kihistoria, tumeweka burudani ili kuthamini mchango mkubwa uliofanywa na wachezaji wetu na benchi letu la ufundi,” alisema Mwankota na kuwataja wasanii watakaoliamsha katika pati hiyo ni Jay Moe, Ferooz, Dullayo, Mchizi Mox, Soggy Doggy, Afande Sele na Mb Dogg.