Kichuya arusha taulo mapema Ligi Kuu

Muktasari:
- Kichuya aliyefunga mabao manne na asisti tatu alisema: “Panapo majaliwa ya uhai natamani msimu ujao niwe kati ya wachezaji watakaofanya vizuri zaidi kwa mabao na asisti, kwani kwa msimu huu nimechemsha kwa sababu ligi imeshaisha tayari.”
KIUNGO mshambuliaji wa JKT Tanzania, Shiza Kichuya ametupa taulo mapema kwa kusema kwa ugumu wa Ligi Kuu msimu huu ulivyo hana wa kulaumu na badala yake anapaswa kujipanga upya kwa msimu ujao wa 2025-2026 ili afanye vizuri na kutimiza malengo.
Kichuya aliyefunga mabao manne na asisti tatu alisema: “Panapo majaliwa ya uhai natamani msimu ujao niwe kati ya wachezaji watakaofanya vizuri zaidi kwa mabao na asisti, kwani kwa msimu huu nimechemsha kwa sababu ligi imeshaisha tayari.”
Nyota huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, Simba na Namungo alisema japo imezoeleka nje ya Simba, Yanga na Azam kuona haiwezekani mchezaji akaingia katika tano bora za wafungaji na asisti, ila kwake anaona hakuna kinachoshindikana mbele ya kujituma na kujiamini.
“Mfano mzuri ilikuwa kwa George Mpole aliyeibuka mfungaji bora wa mabao 17 msimu wa 2021/22 akiwa na Geita Gold, haikuwa kazi nyepesi ukilinganisha na Yanga ambayo alitoka Fiston Mayele akimaliza nafasi ya mfungaji wa pili kwa mabao 16, akiwa amezungukwa na wachezaji wenye viwango bora,” alisema Kichuya na kuongeza;
“Ninachosisitiza ni mchezaji kujitoa kwa kadri anavyoweza na kuondoa mtazamo kuona nje ya timu hizo ngumu kutoa mchezaji ambaye anaweza akaingia katika vinyang’anyiro vya tuzo ama kuchukua kabisa kama aliyekuwa kipa wa Coastal Union, Ley Matampi alikuwa kipa bora wa msimu mbele ya makipa wa Simba, Yanga na Azam.”
Mbali na hilo, Kichuya alisema matarajio yake katika mechi mbili zilizosalia dhidi ya Pamba na Mashujaa ni kuvuna pointi sita, huku akipambana kuona anaongeza idadi ya mabao ama asisti na kusogea pale alipo, licha ya kukiri mechi hizo zinatarajiwa kuwa na zenye ushindani.
JKT itaanza kuvaana na Pamba Jiji, Juni 18 kisha kumalizana na Mashujaa Juni 22 zote ikiwa ugenini.