Ligi ya Championship vita imehamia huku

Muktasari:
- Mtibwa Sugar ilikuwa ya kwanza kupanda Ligi Kuu Bara ikiwa na mechi mbili mkononi, kabla ya Mbeya City kuungana nao pia baada ya ushindi wa mabao 5-0, dhidi ya Cosmopolitan na kurejea tena baada ya kikosi hicho kushuka msimu wa 2022-2023.
WAKATI Ligi ya Championship ikibakisha mzunguko mmoja utakaopigwa Mei 10 ili kuhitimisha msimu wa 2024-2025, tayari Mtibwa Sugar na Mbeya City zimepanda Ligi Kuu, huku 'Wanajeshi wa Mpakani', Biashara United wakishuka daraja.
Mtibwa Sugar ilikuwa ya kwanza kupanda Ligi Kuu Bara ikiwa na mechi mbili mkononi, kabla ya Mbeya City kuungana nao pia baada ya ushindi wa mabao 5-0, dhidi ya Cosmopolitan na kurejea tena baada ya kikosi hicho kushuka msimu wa 2022-2023.
Ushindi huo kwa Mbeya City, umeifanya kufikisha pointi 65 katika mechi 29 ilizocheza nyuma ya Mtibwa Sugar iliyobanwa na sare ya kufungana mabao 2-2 na Transit Camp na sasa imefikisha pointi 68, ikiendelea kusalia kileleni mwa msimamo.
Sasa wakati timu mbili zikipanda Ligi Kuu Bara moja kwa moja na nyingine ikishuka daraja kwenda kushiriki First League, Mwanaspoti linakuletea uchambuzi wa vita ya Championship ilipohamia, ikiwa imebakia mzunguko mmoja ili kumalizia msimu.

GEITA, STAND ITA NZITO
Sare ya Stand United ya bao 1-1, dhidi ya Polisi Tanzania, imeifanya timu hiyo kujihakikishia nafasi ya kucheza mechi za mtoano 'Play-Off', kuisaka tena tiketi ya kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao, baada ya kufikisha pointi 60.
Stand iliyoshuka daraja msimu wa 2018-2019, inakabiliwa na vita kali ya kupambania nafasi hiyo na Geita Gold iliyoshuka msimu uliopita, ambayo tayari itamaliza nafasi nne za juu, kwani pointi zake 55, ilizonazo hazitofikiwa na timu yoyote.
Utamu huo kwa miamba hiyo ambayo imejihakikishia nafasi ya tatu na ya nne, utaanza kuonekana kwa mechi yao ya mwisho ya msimu huu, itakayopigwa Mei 10 na Stand itakuwa kwenye Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga kuikaribisha Geita Gold.
Mechi hii ya mwisho wa msimu baina ya miamba hii, itakuwa ni ya kisasi zaidi kwa 'Chama la Wana', Stand United iliyochapwa kwa mabao 3-1, mzunguko wa kwanza ilipokuwa ugenini Januari 12, 2025, kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita.
Mshindi wa jumla kwa miamba hiyo katika mechi za mtoano 'Play-Off', atasubiri yule wa Ligi Kuu Bara atakayepoteza kutoka nafasi ya 13 na 14 na kwa sasa ni Pamba Jiji na maafande wa Tanzania Prisons zinazopambania kubakia kwa msimu ujao.

ZA KUIFUATA BIASHARA UTD
Ukiachana na Biashara United iliyoshuka daraja baada ya sare ya bao 1-1, dhidi ya Geita Gold, kwa sasa ni timu moja tu inayosubiriwa kuungana na kikosi hicho cha 'Wanajeshi wa Mpakani', huku nyingine mbili zikipambania kwenye 'Play-Off'.
Timu iliyopo katika presha hiyo ni African Sports iliyo nafasi ya 15 na pointi 19, ikifuatiwa na Cosmopolitan yenye 20, huku maafande wa Transit Camp wakiwa na pointi 21, hali inayozidisha msisimko mkubwa wakati huu ikibakia mechi moja tu.
African Sport itaikaribisha Transit Camp mechi ya mwisho nyumbani na endapo itashinda itajihakikishia nafasi ya kucheza mtoano kusaka nafasi ya kubaki, japo ikipoteza safari yao ya Championship itaishia hapo na itaungana na Biashara United.
Wakati zikisubiriwa timu hizo zitakazoshuka moja kwa moja msimu ujao, tayari Gunners ya mkoani Dodoma ambao ndiyo mabingwa wa First League, wamekata tiketi ya kucheza Championship msimu ujao, ikiungana na Hausung FC ya Njombe.
Hausung ilikuwa ya kwanza kupanda kutoka kundi A, ikikusanya pointi 25, baada ya kushinda michezo saba, sare minne na kupoteza mitatu, huku Gunners iliyokuwa kundi B, ikimaliza na pointi 35, ikishinda 11, sare miwili na kupoteza mmoja.

VITA YA UFUNGAJI
Sehemu nyingine yenye mvuto ni vita ya ufungaji bora na anayeongoza hadi sasa ni Andrew Simchimba wa Geita Gold mwenye 18, huku nyota wa TMA, Abdulaziz Shahame akifunga 17 na mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Raizin Hafidh akiwa na 16.
Vita kwa nyota hao watatu ndiyo inayoonekana nzito zaidi ingawa wanaofuatia ni Naku James wa Mbuni FC ya Arusha aliyefunga mabao 11 sawa na Eliud Ambokile wa Mbeya City, huku Yusuph Mhilu wa Geita Gold akitupia nyavuni 10.

MSIKIE MUYA
Kocha wa Geita Gold, Mohamed Muya anasema baada ya kujihakikishia nafasi ya kucheza mechi za mtoano 'Play-Off', kwa sasa wanaendelea kupambana ili kuyatimiza malengo waliyojiwekea, licha ya ushindani mkubwa uliopo kutoka kwa wapinzani wao.
"Malengo yetu yalikuwa ni kupambana ili tupate nafasi ya kupanda Ligi Kuu Bara moja kwa moja kwa msimu ujao, ila kitendo cha kushindwa kufanikisha hilo, tunahamishia nguvu zetu zote kwenye mechi za mtoano ambazo ndio ngumu zaidi," anasema.