Lechantre aleta utamu wa Real Madrid

Muktasari:
- Hata hivyo, kabla ya kuondoka jijini, kocha wake Mfaransa Pierre Lechantre alikuwa na kazi moja ya kutenga muda ili kuchungulia mikanda ya mazoezi na mechi za Real Madrid akitaka utamu wa wababe hao wa Hispania auhamishie Msimbazi.
SIMBA jana mara baada ya kumaliza mazoezi yao kwenye Uwanja wa Boko Veteran, fasta walikimbilia kambini Sea Scape Hoteli, kisha asubuhi ya leo Jumamosi inaanza safari ya Njombe kuiwahi Njombe Mji.
Hata hivyo, kabla ya kuondoka jijini, kocha wake Mfaransa Pierre Lechantre alikuwa na kazi moja ya kutenga muda ili kuchungulia mikanda ya mazoezi na mechi za Real Madrid akitaka utamu wa wababe hao wa Hispania auhamishie Msimbazi.
Simba inaifuata Njombe Mji watakaovaana nao Jumanne katika mechi ya kiporo cha Ligi Kuu Bara, ikisaka pointi tatu ili waikimbie zaidi Yanga waliolingana nao kwa sasa kila moja akiwa na alama 46.
Mechi hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Sabasaba, mjini Njombe lakini Lechantre alikuwa bize akichungulia video hizo za Los Blancos ili kupata maujuzi ya kumaliza mchezo mapema.
Lechantre alilidokeza Mwanaspoti, baada ya kuona ligi ina ushindani mkubwa aliamua kutenga muda kuangalia aina ya mazoezi, mbinu wanazotumia Real Madrid na kubeba baadhi ya maujuzi na kuwapatia wachezaji.
Alisema ili mtu aweze kufanikiwa ni lazima akubali kujifunza kwa waliomzidi hivyo, ameona ni vyema akachota vitu adimu.
“Falsafa na mfumo wetu ni kushambulia zaidi ili kupata mabao mengi kuliko ambayo tumefunga sasa licha ya kuwa vinara, lakini sijaridhika,” alisema.
“Nimeongeza mbinu za kushambulia pembeni kwa kutaka mabeki wa kushoto na kulia kwa kupiga krosi. Lingine ni wachezaji kupiga mashuti nje ya 18 na tumeanza kulifanyia kazi hilo katika mazoezi na tutaonyesha kwa vitendo kwa Njombe,” alisema Lechantre.
MBONDE ANA
SIKU 10
Beki wa kati Salim Mbonde aliyekuwa majeruhi wa goti, ameanza mazoezi na wenzake ila akapewa siku 10 za kujiweka fiti kabla ya kuunganishwa kikosini tayari kuanza kazi.
Lechantre alisema kurudi kwa Mbonde na Haruna Niyonzima kutaongeza nguvu ya kikosini na kusaidia kutimiza malengo ya kubeba ubingwa msimu huu.
“Mbonde amerudi vizuri, ila bado anatakiwa kufanya mazoezi peke yake na nimempa siku 10 ili kumuangalia zaidi na baada ya hapo atajiunga na wenzake.”