Kwani sisi na wao lini?

Muktasari:
Masau Bwire alisikika akichonga sana kabla ya mchezo huo akijipiga kifua kuwa ni lazima wangemkimbiza Simba kwa fimbo tu, lakini mambo yaliwabadilikia kwa kufungwa mabao hayo, huku moja likitupiwa kambani na straika Laudit Mavugo.
MASHABIKI wa Simba jana Jumatano walipagawa Uwanja wa Uhuru. Hii ni baada ya chama lao kupata ushindi mujarabu wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting katika mechi ya Ligi Kuu Vodacom (VPL) Bara na kumfunga mdomo msemaji wa timu hiyo, Masau Bwire.
Masau Bwire alisikika akichonga sana kabla ya mchezo huo akijipiga kifua kuwa ni lazima wangemkimbiza Simba kwa fimbo tu, lakini mambo yaliwabadilikia kwa kufungwa mabao hayo, huku moja likitupiwa kambani na straika Laudit Mavugo.
Ni bao hilo la Mavugo lililowapa ushindi Simba ndilo lililowachizisha mashabiki wa Simba na kuulizana kwa kebehi; “Kwani sisi na wao tunacheza lini?” Wakimaanisha pambano lao na watani wao Yanga watalicheza lini ili kumaliza kazi mapema.
Hilo lilikuwa bao la pili la straika huyo aliyesajiliwa kutoka Vital’O ya Burundi katika ligi hiyo na kuzidi kuwapa mzuka mashabiki waliompachika jina la Mfalme mpya Msimbazi.
Timu hizo kongwe zinatarajiwa kuvaana katika pambano la 97 Oktoba Mosi, huku Simba ikiwa na kiu ya kutaka kulipa kisasi cha vipigo viwili mfululizo vya msimu uliopita mbele ya Yanga ambao jana walibanwa mbavu na Ndanda mjini Mtwara.
Simba wanaamini kama wakimalizana na Yanga kila kitu kwao kitakuwa tambarare na pia watazima ngebe za watani zao ambao wamewabatiza majina ambayo yamekuwa yakiwanyima raha mashabiki hao mitaani wakiitwa wa mchangani.
“Tuleteeni hao Vyura FC tumalize kazi....Hivi kwani tunacheza nao lini jamani Mavugo afanye yake?”
Hizo ni baadhi ya kauli za mashabiki hao wakishangilia ushindi wa pili wa timu yao ambao umeifanya ikamate nafasi ya tatu nyuma ya Mbeya City iliyoporomoshwa na Azam iliyokuwa jijini Mbeya na kuichapa Prisons kwa bao 1-0.
Katika mchezo huo wa jana, Simba ilitawala sehemu kubwa ya mchezo kwa kukosa mabao mengi ya wazi, japo Ruvu ndio waliokuwa wa kwanza kuandika bao dakika ya nane kupitia Abdulrahman Mussa kabla ya Ibrahim Ajib kusawazisha dakika tatu baadaye akimaliza krosi pasi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya mashambulizi makali na dakika tatu tu tangu kuanza kipindi hicho Mavugo alifunga bao jepesi akimalizia kazi ya Ajib akiwa amesalia na lango baada ya kipa wa Ruvu kutoka langoni kizembe. Ruvu ambayo ililianza pambano kwa kuibana Simba, ilijikuta ikimpoteza nyota wake, Jabir Aziz aliyeonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Mdhamiru Yasin aliyeingia kipindi hicho kumpokea Said Ndemla.
Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi saba na mabao matano na ikifungwa mawili, ikizidiwa na Azam na City zilizopo juu yao pia na pointi saba na mabao matano ya kufunga ila zimefungwa bao moja kila moja.
Simba: Vincent Angban, Malika Ndeule, Mohammed Hussein, Novaty Lufunga, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/ Jamal Mnyate, Said Ndemla/ Mdhamiru Yasin, Laudit Mavugo/Frederick Blagnon, Ibrahim Ajib na Mwinyi Kazimoto.
Ruvu Shooting:Abdallah Rashid, Damas Makwaya, Mau Bofu, Frank Msese, Shaibu Nayopa, Jabir Aziz, Abdulrahman Mussa, Shaaban Kisiga, Said Dilunga, Fully Maganga na Claide Wigenge/ Issa Kanduru.
AZAM FC YAINYOOSHA PRISONS
Kutoka Mbeya,
Godfrey Kahango anaripoti Azam iliandika ushindi wa pili mfululizo katika ligi hiyo kwa kuilaza Prisons bao 1-0, lililofungwa na Kipre Balou aliyeunganisha krosi pasi ya Shomari Kapombe.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Sokoine, Prisons ilionyesha upinzani mkali, lakini dakika ya 60 walisalimu amri kwa kuruhusu bao la Balou aliyetuliza gambani krosi ya Kapombe kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa wa Prisons.