Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KWA YANGA! HAWACHOMOKI

Muktasari:

Wachezaji ambao Yanga ina uhakika wa kuwabakiza hadi sasa ni kipa mahiri Beno Kakolanya, Simon Msuva, Amissi Tambwe, Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Andrew Vincent ‘Dante’, Hassan Kessy, Juma Abdul, Geofrey Mwashiuya (pichani), Obrey Chirwa, Emmanuel Martin, Oscar Joshua na Juma Mahadh.

SIMBA na Singida United zimeanza usajili wa mbwembwe ambao umeonekana kuwatisha mashabiki wa Yanga, lakini imebainika kwamba hata iweje kuna wachezaji 13 ambao hawawezi kung’oka Jangwani.

Wachezaji ambao Yanga ina uhakika wa kuwabakiza hadi sasa ni kipa mahiri Beno Kakolanya, Simon Msuva, Amissi Tambwe, Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Andrew Vincent ‘Dante’, Hassan Kessy, Juma Abdul, Geofrey Mwashiuya (pichani), Obrey Chirwa, Emmanuel Martin, Oscar Joshua na Juma Mahadh.

Katika kundi hilo, habari zinasema kwamba Mwashiuya alikuwa ananyemelewa na Simba na hata watu wake wa karibu walishafanya mazungumzo na Msimbazi kabla ya kuja kubaini kwamba mchezaji huyo amebakiza mkataba wa mwaka mmoja ambao hawezi kuuvunja mpaka Yanga waridhie.

“Hakuna ukweli wowote kuwa mimi nimemaliza mkataba na Yanga. Siwezi kujiunga na wala sijafanya mazungumzo na klabu yoyote ile kwa sababu bado nina mkataba wa mwaka mmoja uliobakia,” alisema Mwashiuya ambaye Yanga ilimsajili kutoka Kimondo ya Mbeya.

Wachezaji hao ambao mikataba yao imebakiza muda wa chini ya miezi sita kumalizika ni Donald Ngoma, Thaban Kamusoko, Vincent Bossou, Deus Kaseke, Matheo Anthony na Deogratias Munishi ‘Dida’ ambao Yanga inaweza kuwaongezea mikataba au kuwapotezea.

Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Athuman Kihamia, alitamba akisema: “Tunafanya usajili wa kisayansi na sio wa kupiga kelele kama wapinzani wetu wanavyofanya. Hao wachezaji wote ambao upande wa pili umewasajili, ni wa kawaida ambao uwezekano wa kupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga kwao ungekuwa mgumu.

“Tumepanga kufanya usajili wa kisayansi kwa kupata mchezaji ambaye kiwango chake kitaendana na fedha atakayopewa na ataitumikia timu kwa muda mrefu.

“Hatutaki kutumia fedha nyingi kwa wachezaji wenye uwezo wa chini.”

VIONGOZI WAGUNDUA

Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, alifunguka kwamba njia pekee ya kukamilisha usajili wao badala ya kutangaza kama awali kwa sasa utakuwa mwendo wa kimya kimya.

“Awali tulikuwa tunatangaza nani tunamhitaji, hilo limetuumiza baada ya nyota hao kurubuniwa na upande wa pili, nakuhakikishia kwamba tunaendelea kusajili isipokuwa hatutaweka wazi,” alisema Mkwasa ingawa hakutaka kutaja ni nyota gani wamepigwa bao na wapinzani wao.

Ila Mwanaspoti linafahamu kwamba Yanga ndiyo ilikuwa ya kwanza kufanya mazungumzo na Mwambeleko aliyekuwa beki wa Mbao na sasa yupo Simba pamoja na Waziri Junior na Mbaraka Yusuph ambao tayari wako mikononi mwa Azam.

Alipoulizwa je wanatishwa na usajili walioufanya Simba, alishangaa kwa kusema: “Kutishwa na usajili wa Simba, kivipi! Sisi ni kama wanajeshi hatuwezi kumhofia adui yetu ama kauli rahisi mpinzani wetu kipindi cha usajili ni cha vita ya ushindani kila mtu anataka kikosi chake kiwe kizuri. “Labda niweke wazi kwamba wachezaji chipukizi imekuwa ngumu kuwaamini kwa sababu ni rahisi kudanganywa na kuacha malengo, huwezi kufananisha na mkongwe ambaye anakuwa na umakini wa hali ya juu katika maamuzi yake.”