Kwa Simba hii...Atapigwa mtu nyingi, Chama afunguka kila kitu

Monday January 17 2022
Chama1 pic
By Charles Abel

USAJILI wa Clatous Chama umewakosha nyota wa zamani wa soka waliosema kama kiungo huyo atakuwa na ubora ule wa mwanzo na kuelewana na wenzake, basi timu pinzania zitashushiwa mvua za mabao siku moja.

Chama amerejea Simba juzi Ijumaa akitokea RS Berkane ya Morocco iliyomnunua kutoka Msimbazi katika dirisha kubwa na kushindwa kutumika kabla ya kuamua kurudi nchinikuchukua nafasi ya Duncan Nyoni aliyetemwa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, nyota hao wakiwamo walioicheza Simba waliliambia Mwanaspoti, kama Chama hajashuka kiwango na akazoea mapema mbinu na staili ya uchezaji kwa wenzake aliowakuta, safu ya ushambuliaji ya Simba itakuwa kali maradufu.

“Ujio wake una faida mbili kubwa, kwanza utasaidia kuiamsha Simba ambayo tangu alipoondoka ilionekana kushuka kasi yake, hivyo akishirikiana na wenzake timu itachangamka.

Kingine ataipa chachu katika harakati zake za kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali kupitia mabao atakayofunga na kupika, pia kuichezesha timu. Chama ni kipenzi cha Wanasimba, anajua wanataka nini kutoka kwake, hivyo ujio wake ni karata nzuri Simba,” alisema nyota wa zamani wa AFC Arusha, Ally Ruvu na kuongeza;

“Eneo la ushambuliaji litaimarika zaidi kwa Simba na linaweza kuwa na makali zaidi katika utengenezaji na kufunga mabao na ubunifu wa kupenya safu ngumu.”

Advertisement

Ruvu alisema ujio wa Chama unafanya kocha Pablo Franco kuwa na idadi kubwa ya kutosha ya wachezaji wanaoweza kupika mabao na kufunga na hata kupasua ukuta wa timu pinzani.

“Ni wazi kwamba katika mechi zinazohitaji wachezaji wenye ubunifu wa kupenya ukuta wa adui mbele, kocha Pablo atakuwa na nafasi kubwa ya kuwatumia Chama kucheza nyuma ya mshambuliaji wa kati na pembeni yake, Bernard Morrison na Pape Sakho ambao wana kasi na uwezo mkubwa wa kupiga chenga, pasi za mwisho na kufunga mabao huku benchi akiwa na ama Kibu Denis, Peter Banda ama Jimmyson Mwanuke wenye sifa hizo, alisema.

KamaPablo atataka kushambulia kwa namba kubwa ya wachezaji, anaweza kuwapanga Chama, Kagere, Sakho, Morrison na nyuma yao Rally Bwalya katika mfumo wa 4-4-2 ambao utamfanya awe na uhakika wa nyota watano karibu na eneo la adui na nyota wa zamani wa Simba, Mraage Kabange alikazia kwa kusema;

“Ni jambo lililo wazi, tangu alipoondoka Simba, kuna kitu kilipungua. Kina Bwalya, Sakho na Morrison japo ni wachezaji wazuri lakini hawakufikia kiwango cha Chama. Naamini ujio wake utaifanya Simba iwe na safu kali ya ushambuliaji mara mbili zaidi ya sasa na utasaidia kuwafanya wenzake kuwa bora zaidi.”

Naye Emmanuel Gabriel, straika wa zamani wa Simba alisema; “Sakho anajua kusaka mipira, kama kocha atampa uhuru wa kucheza au akaanzia pembeni na Chama akacheza kiungo ya juu, naiona Simba itatengeneza nafasi nyingi za kufunga kama ilivyokuwa msimu ulioisha.”

Alisema ujio wa Chama ni kuwa na uhakika wa timu kutengeneza nafasi nyingi za kufunga na endapo kama Sakho akikosekana ataziba pengo lake.

Naye kipa wa zamani, Steven Nemes alisema ujio wa Chama unaongeza nguvu wa upishi wa mabao, akisaidiana na Sakho kama kocha atajua namna ya kuwapanga.

“Sakho ana mpira mwingi sana mguuni, kocha anaweza akampanga kuanzia pembeni na Chama akacheza kama alivyokuwa anafanya siku zote kabla ya kuondoka kwenda nje,”alisema.

Chama anarejea wakati Sakho anaonekana moto kwani katika mechi saba mfululizo, alizocheza Simba, imepata ushindi mara sita na kutoka sare moja, huku ikifunga mabao 12 na kuruhusu nyavu mara mbili tu.

Katika hayo mabao 12 ya Simba, Sakho amehusika na mabao sita, akifunga matatu, kupiga pasi za mwisho mbili na kusababisha penalti iliyozaa bao moja.

Simba pia inajivunia kiwango bora cha nyota wake kutoka Malawi, Peter Banda aliyepo Fainali za Kombe la Afrika (Afcon) huko Cameroon kwani katika mchezo wa kwanza dhidi ya Guinea, winga huyo alikuwa miongoni mwa waliopata alama kubwa kwa kiwango bora akipewa alama 7.5 kati ya 10.

Hata hivyo, winga wa zamani wa Simba, Yusuph Mgwao ametoa tahadhali kuwa ujio wa Chama usiathiri maendeleo ya wachezaji wengine.

“Yule Sakho anacheza vizuri kwa sasa kama ilivyo kwa Kibu Denis ambaye ameonekana kuwa kipenzi cha kocha na anatimiza vyema majukumu uwanjani. Yupo Dilunga naye amekuwa bora. Ujio wa Chama ni fifte fifte, lakini jambo muhimu ni kuwalinda wachezaji wengine hasa walioanza vizuri,” alisema Mgwao.

Advertisement