Chama: Mtajua hamjui

Chama: Mtajua hamjui

BAADA ya kelele nyiingi. Mwamba katua Msimbazi. Simba imemtambulisha na kumshusha rasmi Jijini Dar es Salaam kipenzi cha mashabiki, Clatous Chota Chama.

Chama anatua akitokea Berkane ya Morocco ambayo maji yalizidi unga akaamua kurejea zake Bongo ambako alishajijengea ufalme wake Msimbazi. Amesisitiza kwamba kuondoka kwake Morocco siyo kwamba alishindwa bali ni changamoto za kimpira lakini atawaonyesha wanaombeza uwanjani kwamba watajua hawajui kwani ubora wake haujachuja.

Staa huyo ambaye habari za ndani zinasema alishindwa kuendana na mazingira ya ndani ya Berkane ya Kocha Florent Ibenge pamoja na hali ya hewa ya Morocco, hivyo akawabonyeza viongozi wa Simba wapambanie arudi kabla ya Yanga nao kuingilia dili hilo ingawa walikwama katikati kutokana na makubaliano ya mauziano ya Simba na Berkane.

Chama ambaye amekuwa akifanya mahojiano ya mara kwa mara na Mwanaspoti, jana alisema kwamba amekuja Simba kupiga kazi zaidi ya ile ya awali.

Alisema wakati anaondoka hapa ilikuwa mchezaji mkubwa anayetegemewa na wengi kutokana na kazi yake uwanjani amepanga kulifanya jambo hilo zaidi.

“Awali nilikuambia kila kitu kinakwenda kwa wakati na wakati wake umefika basi tusubiri nina imani nitafanya mambo mazuri katika timu kwenye mashindano yote,” alisema Chama na kuongeza;

“Malengo makubwa ni kuipigania timu katika mashindano yote ili kufanya vizuri pengine zaidi ya ilivyokuwa pale awali na hilo linawezekana bila shida yoyote.

“Haya mambo ya ushindani mahali popote katika kikosi lazima utakutana nayo, subiri muda ukifika haya yote yataonekana na nina imani nitaingia katika timu na mchango wa mafanikio nitautoa.

“Mara zote huwa natamani kucheza kwa mafanikio katika timu yoyote sitamani kuona nashindwa kulitimiza hilo sababu kujiamini katika uwezo wangu,” alisema staa huyo ambaye hataichezea Simba kwenye michuano ya kimataifa msimu huu.

“Kutokana na changamoto nilizokutana nazo naamini Tanzania nitatengeneza heshima kwa kufanya yale mazuri zaidi ya awali.”