Kwa mziki huu, mtaenda kuwaambia.. Robertinho afunga busta

KOCHA Roberto Oliveira 'Robertinho' anajua ana dakika 90 ngumu mbele ya Raja Casablanca ya Morocco kwenye mechi ya Kundi C ya Ligi ya Mabingwa Afrika na fasta ameamua kuwafungia busta Waarabu ili kuwanyamazisha mapema katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Simba ni wenyeji wa mchezo huo utakaoanza saa 1:00 usiku, huku kocha huyo Mbrazili akija kivingine kwa kubadilisha kidogo kikosi chake na kuapa kutembeza bolu mwanzo mwisho ili kupata ushindi nyumbani baada ya awali kupoteza ugenini wiki iliyopita kwa Horota ya Guinea.
Kocha huyo jana aliwapigisha tizi mastaa wake tayari kwa mchezo huo, huku jeshi zima likionekana huenda leo likawa na mabadiliko na hata aina ya soka itakalocheza kulinganisha na mechi iliyopita jijini Conakry na kuchapwa bao 1-0.
Kikosi cha Simba kilifanya mazoezi ya mwisho jana Kwa Mkapa na Mwanaspoti lilishuhudia kwa muda wa dakika 15 na kubaini Mbrazili huyo alivyoamua kuwafungia busta Wamorocco.
Kulingana na mazoezi hayo Simba inaweza kuanza kipa, Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein, Joash Onyango, Henock Inonga kwa eneo la ulinzi, huku kiungo Mzamiru Yassin na Ismael Sawadogo.
Kiungo mshambuliaji, Saido Ntibazonkiza aliyekosekana mchezo wa kwanza dhidi ya Horoya, Clatous Chama na Pape Sakho wataanza pamoja huku mshambuliaji wa kati watapishana kati ya Jean Baleke na John Bocco kwani mmoja huenda akapewa nafasi ya kuanza.
Kwenye mchezo wa leo Simba itamkosa kiungo wa kikosi cha kwanza, Sadio Kanoute kutokana na adhabu ya kadi za njano jambo hilo limechangia kwa benchi la ufundi kubadilisha mfumo wa 4-3-3, uliyoanza nao kwenye mechi ya Horoya na leo itatumia 4-2-3-1.
Kwenye mazoezi ya jana Saido alionekana kuwa na morali kubwa akionyesha kiwango kizuri haswa yale mazoezi ya kucheza alifunga, kutoa pasi za mwisho na alikuwa hatari kutengeneza mashambulizi.
Nahodha wa Simba, John Bocco alisema mechi ya Horoya kuna mazuri waliyafanya na katika mazoezi ya kujiandaa na Raja wameyaendeleza ili kuyatumia katika mechi ya nyumbani na kupata ushindi.
Bocco alisema kuna makosa yalitokea ikiwemo kushindwa kutumia nafasi za kufunga mabao ilizopata ugenini ila kulingana na maandalizi yao hilo halitaweza kujirudia.
"Tunahitaji kushinda mechi ya Raja ili kupata pointi tatu za kwanza na kujiweka katika mazingira mazuri kwenye kundi na kuyaweka hai malengo yetu ya kufuzu hatua ya robo fainali," alisema Bocco na kuongeza;
"Pesa iliyowekwa na Rais, Samia Suluhu imeongeza morali kwa wachezaji na ameonyesha jinsi gani Simba inahitajika kufanya vizuri kwa manufaa ya Taifa."
Kocha Robertinho alisema kila mechi ina maandalizi yake tofauti kulingana na aina ya wapinzani wanaokwenda kukutana nao ila malengo yao makuu ni kufuzu kwenye hatua hiyo ikiwezekana na kwenda hadi fainali kutwaa taji hilo.
Robertinho alisema mechi ya kwanza ilianza na kucheza kwa malengo ya kujilinda ila katika mechi ya Raja kwa asilimia kubwa itacheza kwa kushambulia kwani hata wachezaji wengi ambao wataanza ni wale wenye asili na sifa ya kushambulia.
Alisema kukosekana kwa Kanoute si jambo zuri kwani kwenye mechi kubwa kama ya Raja kila kocha anahitaji kuwa na wachezaji wote wa kikosi cha kwanza ila uzuri akiwa Dubai kila nafasi moja alitengeneza wachezaji wawili kwahiyo pengo hilo litakwenda kuzibwa vizuri.
"Nimekuwa na wakati mzuri Simba nimekutana na wachezaji wazuri wenye vipaji, tumefanya maandalizi ya kutosha, nimewaeleza wachezaji hakuna matokeo mengine yoyote yanayohitajika kwenye mechi hii zaidi ya ushindi," alisema Robertinho na kuongeza;
"Mechi iliyopita kipindi cha pili timu ilikosa nafasi nyingi za kufunga pengine wakati huu labda tungekuwa tunazungumza mechi iliisha kwa sare ya bao 1-1, kama tungetumia nafasi zile kufunga ila hilo limeshapita na tumeyafanyia kazi."