Kwa Mkapa kisasa zaidi, kuanza kuboresha haya...

YANGA ipo kwenye hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa imefanya vizuri zaidi kwenye michuano ya Afrika kuliko kipindi kingine chote ambacho imeshiriki michuano hiyo.
Hata hivyo, wakati timu hiyo ikiwa kwenye michuano hiyo, kwa upande wa  Simba ambao walitolewa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika wanawaza pia jambo lingine kwa kuwa baadaye mwaka huu watakuwa tena kwenye michuano mingine ikiwa ni timu pekee hapa nchini ambayo itashiriki michuano ya Super 8 toleo la kwanza.
Hii itakuwa ni historia kwa Simba SC kwa kuwa itakuwa kati ya timu nane Afrika nzima ambayo imepewa nafasi ya kushiriki michuano hiyo mikubwa ambayo inasimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika Caf kupitia kamati maalumu.
Caf ambao walifanya mkutano wao wa kawaida wa 44, Agosti 10 mjini Arusha walisema haya ni mashindano mapya na yatashirikisha timu kubwa zenye mafanikio kwenye michuano ya Caf lakini ikionekana kuwa wanataka timu zile zenye mashabiki wengi.
Awali Caf walitaja baadhi ya timu za Afrika ambazo zitashiriki michuano hiyo yenye fedha nyingi  ambapo zipo Al Ahly,  Zamalek, Pyramids, Al Masry, Wydad AC, Raja Athletic, RS Berkane, Esperance, Etoile Sportive Du Suhel na Orlando Pirates, Asec Mimosas ingawa baadaye nyingine zilitangaza kujitoa.
Bingwa wa michuano hiyo anatarajiwa kuvuna kitita kikubwa cha fedha, yakiwa yanatajwa ndiyo mashindano yenye fedha nyingi zaidi Afrika.
Hata hivyo, miezi kadhaa nyuma kamati maalumu ya kukagua maandalizi ya michuano hiyo ilitua hapa nchini na ilikuwa na kikao pamoja na mabosi wa Simba, Serikali na TFF na walifanya kazi ya kukagua miundombinu ambayo itatumika kwenye michuano hiyo.
Pamoja na mambo mengine kamati hiyo ilitoa ripoti ambayo imenaswa na Mwanaspoti ikionyesha baadhi ya mambo ambayo yanatakiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Mkapa ambao Simba watautumia kwenye michuano hii.
Ripoti hiyo inaonyesha kamati hiyo haikuridhishwa na mambo mengi kwenye uwanjani huo na kupendekeza ufanyiwe marekebisho makubwa, ikiwa ni siku chache baada ya serikali kutangaza pia kufanya marekebisho kwenye uwanja huo.
Baadhi ya mambo ambayo kamati hiyo imesema kuwa marekebisho hapo yanatakiwa kufanyika kwa wiki sita hadi nane, kuanzia Mei 15 mwaka huu, huku ikiamuru kuwa kwa kipindi hicho hawataruhusu mashindano yoyote kufanyika hapo.
Kamati hiyo imeeleza baadhi ya maeneo yanayotakiwa kufanyiwa marekebisho huku mengine zikiwemo taa kuzimika kwenye michezo miwili tofauti ya hivi karibuni kuwa  kama ifuatavyo:

Sehemu ya kuchezea (pitch)
Kamati hiyo imeshauri sehemu ya kuchezea kuwa hapo vizuri kwa ajili ya mashindano hayo na inatakiwa kufanyiwa marekibisho makubwa na kuweka (hybrid pitch), hizi ni nyasi asilia lakini zikiwa na mchanganyiko kidogo wa nyasi bandia.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali zinaonyesha uwekaji wa nyasi hizo ni wa haraka na unaweza kutumia kati ya siku sita hadi saba.
Hata hivyo, inaonekana ni nyasi bora kabisa kwa maendeleo ya soka kwani zina uwezo mkubwa kulinda afya za wachezaji wanaozitumia, zinawafanya wachezaji kuwa na hali ya kujiamini lakini kukimbia kwa kasi zaidi lakini zikiwafanya wachezaji kuwa na ubora wao kwa muda mrefu.
Taarifa inaonyesha ni nyasi ambazo zinaweza kudumu kwa miaka nane hadi 10 bila kubadilishwa lakini ikisema lazima taratibu zote zinazotakiwa kwenye nyasi hizo zifuatwe ikiwemo matundu maalumu ya kupitisha hewa na maji uwanjani yawepo.
Pia, kamati hiyo imesema mitambo ya umwagiliaji kwenye uwanja huo inatakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuhakikisha kila sehemu inapata maji ya kutosha kulingana na viwango.
Kamati hiyo, imesema eneo hili linatakiwa kukamilika Agosti 1, 2023.

Magoli na vibendera
Kamati hiyo imesema magoli yaliopo kwenye Uwanja wa Mkapa pamoja na vibendera kwenye eneo la kupigia kona vinatakiwa kubadilishwa.

MABENCHI YA WACHEZAJI, WAAMUZI
Kamati hiyo ya ASFL, imesema hairidhishwa na mabenchi wanayotumia wachezaji wa akiba kwenye Uwanja wa Mkapa, hivyo yanatakiwa kubadilishwa na kuwa ya kisasa zaidi.
Wamesema mabenchi ya wachezaji wa akiba yanatakiwa kuwa na siti 23, yakiwa yakiwa ya kisasa kulingana na standandi za Caf kwa sasa, lakini yawe umbali wa mita tano kutoka kwao hadi sehemu ambayo kocha anasimama.
Pia kunatakiwa kuwa eneo maalumu kwa ajili ya waamuzi ambalo linatakiwa kuwa na siti nne zikiwa na viwango vikubwa vya kisasa kuwe na eneo la kuzuia jua na mvua.


TAA
Kamati hiyo imesema kuwa taa zinazotakiwa kwenye uwanja wa Mkapa lazima ziendane na utaratibu wa Caf, wamesema taa za kiwango cha chini zinazotakiwa ziwe na Lux 1200 kuzunguka uwanja mzima wa Mkapa ambazo kwa sasa kwa Mkapa hazijafungwa, hivyo ni jambo linalotakiwa kabla ya michuano hiyo, pia lazima kuwe na jenereta la dharura ambalo linaweza kufanya kazi wakati linapotakiwa.
Taarifa hiyo imeonyesha kuna mfumo pia mbovu kwenye uwekaji wa taa hizo ambao wanaona unatakiwa kuwekwa upya ili kukidhi kutumika kwa michezo ya usiku.


VYUMBA VYA KUBADILISHIA NGUO
Nyaraka hiyo inaonyesha kamati hiyo imesema vyumba vya kubadilishia nguo kwa ajili ya wachezaji havipo kwenye viwango vinavyotakiwa, hivyo imeshauri mabadiliko makubwa yafanyike na kuvifanya kuwa vya kisasa zaidi.
Imesema mbali na sehemu ya vyumba pia sehemu ya vyoo haifai kutumika kwa ajili ya mashindano hayo makubwa, au wanatakiwa kutengeneza vyoo hivyo upya.
Pia wameshauri marumaru (tiles) zilizowekwa kwenye vyumba hivyo kubadilishwa kabla ya michuano hiyo kuanza.
Mambo hayo yanayotakiwa kufanyika kwenye vyumba ndiyo hayo ambayo imeshauriwa pia yanatakiwa kufanyika kwenye vyumba vya waamuzi na kufikia viwango vya Caf.


OFISI MAALUMU NA WAJUMBE WA CAF
Mabosi hao wa Caf, wamesema kwenye Uwanja wa Mkapa kunatakiwa kuwa na ofisi maalumu kwa ajili ya maafisa kutoka kwenye Shirikisho la Soka Afrika Caf na wamesema haipo kwa sasa.
Imeshauriwa ofisi hiyo inatakiwa kuwa na samani za kisasa ikiwa inatakiwa kutengenezwa kutokana na jinsi wanavyotaka, iwe na meza moja, kiti kimoja, machine ya kutolea kopi, friji, kiyoyozi.
Taarifa imesema ofisi hiyo inatakiwa kukamilika kabla michuano hiyo haijaanza.


OFISI YA MADAKTARI
Hii ni ofisi maalumu ambayo inatakiwa kuwepo kwenye Uwanja wa Mkapa na taarifa hiyo inasema iliyopo haina viwango vinavyotakiwa na Caf.
Hii inaelezwa itakuwa maalumu kwa ajili ya kuwapa huduma ya kwanza wachezaji pamoja na waamuzi.
Imesema ofisi hiyo inatakiwa kuwa na;
Meza moja, vifaa maalum kwa ajili ya matibabu ya dharura
vifaa kwa ajili ya upasuaji mdogo, vifaa kwa ajili ya kupima upumuaji, vitanda, sindano za dharura na dawa, mashine maalum kwa ajili ya vipimo vya moyo, vipimo kwa ajili ya presha, vipimo vya kupima sukari mwilini pamoja na vingine vingi.


DAWA YA KUONGEZA NGUVU
Kamati hiyo ya Caf, imeshauri pia uwanja huo unatakiwa kuwa na ofisi maalum kwa ajili ya kupima matumizi ya dawa za kuongeza nguvu michezoni.
Kamati hiyo inataka ofisi hiyo iwe karibu na vyumba vya kubadilishia nguo vya wachezaji.
Inatakiwa kuwa na sehemu maalumu kwa ajili ya wagonjwa kusubiri ambayo inaweza kumudu kuwa na watu nane kwa wakati mmoja, pia inashauriwa kuwa na choo cha kujitegemea kikiwa na funguo maalum, kunatakiwa kuwa na televisheni, vinywaji ambavyo havina kilevi, friji maalum pia maji yenye madini, sehemu ya kuweka taka, karatasi pamoja na chupa.
Kiongozi kwenye ofisi hiyo anatakiwa kuwa na meza moja ambayo itakuwa imezungukwa na viti vinne, beseni moja la kunawia mikono au matumizi mengine, ofisi hiyo inatakiwa kuwa na kabati maalum lenye ufunguo maalamu, maji yanatakiwa kuwepo muda wote kuwe na kioo maalum.