Kwa Henderson, De Gea ajiandae

Friday October 02 2020
de gea pic

MANCHESTER, ENGLAND. WACHEZAJI wa zamani wa Manchester United, Andy Cole na Darren Fletcher wamekoshwa na kiwango kilichooneshwa na golikipa wa timu hiyo, Dean Henderson katika mchezo wa Carabao Cup dhidi ya  Brighton na kusema David de Gea itabidi apambane kwa kuwa anaweza kupoteza namba katika kikosi cha kwanza.

Henderson aliokoa mchomo baada ya shuti kali lililopigwa na Leandro Trossard na kufanya amalize mchezo wa pili bila ya kuruhusu bao tangu arudi Man United akitokea Sheffield United ambapo alicheza kwa mkopo msimu uliopita.

Baada ya mchezo huo uliomalizika kwa Man United kushinda mabao 3-0, Cole alizungumza kupitia Sky Sports na kusema: “Amecheza vizuri katika mchezo wake wa pili, niliwahi kusema hapo awali kuwa kipa wa Manchester United sio kazi rahisi na hasa timu ikiwa inacheza vizuri kwa sababu unakuwa hupati mashambulizi mengi hivyo mashabiki wanategemea hayo machache unayokumbana nayo uwe unayaokoa, na yeye alifanya hivyo kwa kuokoa hatari mbili,” alisema.

Kwa upande wake, Fletcher alisema Henderson aliokoa hatari kubwa mbili ambazo zinaonyesha kuwa yeye ni bora, “Tulikuwa tunasema anaonyesha kiwango kikubwa Sheffield kwa sababu ya udogo wa timu hivyo muda mwingi huwa inazuia, lakini ameonyesha kwamba alikuwa habahatishi,” alisema.

Baada ya kurejea Old Trafford msimu huu, mchezo wake wa kwanza ulikuwa dhidi ya Luton ambapo Man United ilishinda kwa  mabao 3-0 wiki iliyopita.

Cole alipoulizwa uwezekano wa Henderson kumpindua De Gea na kuwa kipa namba moja alisema, De Gea ana nafasi kubwa ya kuendelea kusimama kama namba moja kwa sababu ya rekodi yake ya msimu uliopita. Lakini bado Hendersona amethibitisha kuwa ni kipa mzuri na atamsumbua sana.” 

Advertisement

 

Advertisement