Kuporomoka kwa Tanzania Prisons

Muktasari:

Kifukwe anasema wachezaji wanapata sapoti kubwa na wanapata haki zao kwa muda unaostahili, hivyo wana uhakika mambo yataendelea kukaa sawa muda sio mrefu.

UKIUTAZAMA msimamo wa Ligi Kuu Bara kabla mechi za jana Alhamisi huwezi kupata shida kuisaka sehemu ilipo Tanzania Prisons.

Inaweza kuwatia mashaka kidogo wapenzi wa timu hiyo kama msimu ujao itaendelea kuwapa uhondo wa katika uwanja wao wa nyumbani kama walivyozoea.

Lakini pamoja na timu hiyo kuburuza mkia, mabosi wake wala hawana presha unaambiwa, kwani wanadai muda sio mrefu wataanza kutembea vichapo ili kuirejesha heshima ya timu hiyo na kukaa kwenye mstari unaotakiwa.

Prisons ni moja kati ya timu kongwe mkoani Mbeya na katika Ligi Kuu ina mashabiki lukuki kutokana na uimara wake na ushindani iliokuwa ikiuonyesha miaka ya nyuma.

WAMEJIPANGA KINOMA

Katibu Mkuu wa Prisons, Ajabu Adam Kifukwe, kwanza anawatuliza mashabiki na kudai upepo uliwaendea vibaya katika mzuguko wa kwanza lakini kwa sasa kila kitu kimeanza kunyooka hasa baada ya kulifumua benchi la ufundi na kumtoa, Abdallah Mohammed na kumleta Kocha Mohammed Rishard ‘Adolph’.

Kifukwe anasema wameanza kurudi kwenye ushindani na sio wasindikiza tena.

“Kwenye soka kila kitu kinatokea kwa muda, hata yale ambayo hujayapanga yanakuja, hizo ndio changamoto za soka na haziwezi kukwepeka zaidi ya kujipanga.

“Mashabiki ndio nguzo yetu ya kujivunia mana hii ni timu yao na hakuna njia nyingine ya kuikimbia zaidi ya kuipa sapoti na hamasa kwenye michezo ili vijana wasijione wapweke na hapo itakuwa chachu ya wao kupambana na kupata matokeo mazuri.”

Kifukwe anasema wachezaji wanapata sapoti kubwa na wanapata haki zao kwa muda unaostahili, hivyo wana uhakika mambo yataendelea kukaa sawa muda sio mrefu.

MSIKIE KOCHA

Kocha Mkuu wa Prisons, Adolf Rishard anasema baada ya kuingia kwenye timu hiyo kikubwa anachokifanya ni kuimarisha wachezaji na kuwafanya kuwa wapambanaji.

“Hakuna litakaloshindikana kama tutaweka nia na kushirikiana kwa pamoja.

“Kikubwa katika dirisha dogo la usajili tuliongeza nguvu, ndio nimeanza kuwatumia baadhi ya wachezaji na wanasaidia kutafuta matokeo mazuri na kurudi kwenye nafasi za juu.”

MAVUNO YAO TPL

Katika michezo 22 ambayo Prisons imecheza, imefanikiwa kuvuna alama 17 tu, ikishinda mechi mbili dhidi ya Alliance FC iliposhinda mabao 2-0 sawa na ule mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar uliopigwa Januari 9, mwaka huu, katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Katika michezo mitano iliyopita imeshinda mmoja tu, sare tatu na imepoteza mchezo mmoja ilipochapwa na Lipuli FC bao 1-0 katika dimba la Samora Mjini Iringa.

Prisona haitaweza kukisahau kichapo cha funga mwaka cha Desemba 15 mbele ya KMC ilipolala kwa mabao 5-1 yaliyowekwa nyavuni na James Msuva aliyefunga mawili (69 na 86), Sadalah Lipangile (66), Emmanuel Mvuyakule (48) na Ally Msengi (73) wakati lile la kufutia machozi kwa Prisons likifungwa na Jumanne Elifadhili (60).

TUJIKUMBUSHE KIDOGO

Tanzania Prisons SC ni timu inayomilikiwa na Jeshi la Magereza Tanzania, makazi yake mkoani Mbeya na Sokoine ndio uwanja wao wa nyumbani. Timu inavaa jezi rangi ya kijani yenye mchanganyiko na nyeupe. Prisons miaka ya nyuma ilikuwa ikijulikana kama Chuo Rwanda SC chini ya Kocha Katikilo kabla ya mwaka ya 1995/96 kuitwa Tanzania Prisons SC ikashiriki Ligi Daraja la Kwanza, chini ya Kocha Hassan Mlilo na baadaye akaichukua kocha wa zamani wa Simba, Marehemu Paul West Gwivaa (1997).

Mwaka 1999 ikiwa chini ya Kocha Charles Boniface Mkwasa na msaidizi wake, Freddy Felix ‘Minziro’ ilibeba ubingwa wa Ligi Kuu.

Mwaka 2000 ilishiriki Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa) bahati mbaya ikatolewa hatua ya awali.

Pia, ilishiriki Kombe la Shirikisho kwa miaka miwili 2005 na 2006 na katika hatua zote haikufanya vizuri ilitolewa hatua ya awali. Mwaka 2009 ilishuka daraja na kufanikiwa kupanda mwaka 2011 chini ya Kocha Stephen Matata. Kwa sasa uongozi una mpango wa kuimarisha vikosi vya timu za vijana U-20,U-17 na U-15 juhudi zimeanza na tunaamini hapo baadaye itavuna matunda.

SAFU YA UONGOZI

Prisons ambayo leo Ijumaa iko uwanjani kule Kaitaba dhidi ya Kagera Sugar katika kuhakikisha haifanyi vibaya katika mechi zake zilizobaki imesuka safu yake ya kama hivi, makocha, Mohammed Adolf (Kocha Mkuu), Shaaban Kazumba (kocha msaidizi), Herry Boimanda Mensady (kocha makipa), Oraph Peter Mwamlima (kit meneja), Kilulu Masunga Ntobi (daktari), Simon Onifasi Metta,(meneja) na Katibu Mkuu ni Ajabu Kifukwe.